Bajaji zaanza kurejea mtaani Mbeya, daladala zalalamika

Bajaji zaanza kurejea mtaani Mbeya, daladala zalalamika

Mbeya. Bajaji jijini Mbeya zimeanza kurejea barabarani baada ya kusitisha huduma kwa takribani siku mbili kupinga kuondolewa katika barabara kuu ya Tanzam, huku wananchi wakimtaka Mkuu wa Mkoa wa Mbeya (RC), Jumanne Sagini, kusimamia msimamo wake wa kutaka vyombo vya usafiri kuzingatia sheria.

Hata hivyo, kurejea kwa bajaji hizo kumeambatana na malalamiko kutoka kwa baadhi ya madereva wa daladala, wanaodai kuwa wenzao wa bajaji wamekuwa wakiwaingilia wanapotekeleza majukumu yao, ikiwamo kuwashambulia na kuharibu vyombo vyao.

Jana Jumanne, Oktoba 20, 2026, bajaji jijini humo zilisitisha huduma zikieleza kutoridhishwa na hatua ya kuziondoa katika ruti ya barabara kuu ya Tanzam, hali iliyosababisha baadhi ya wananchi kupata shida ya usafiri.

Wakati huo, baadhi ya wananchi walilazimika kutembea kwa miguu kwenda kwenye shughuli zao, huku wengine wakitumia usafiri wa bodaboda na kulipa nauli kubwa kuliko walivyozoea.

Hivi karibuni, Sagini alitangaza kuwa vyombo vyote vya usafiri vinapaswa kuzingatia sheria za barabarani, akizitaka bajaji kuacha kutumia barabara kuu ya Tanzam katika mkakati wa kuboresha hali ya usafiri jijini humo na kudhibiti msongamano wa magari.

Leo, Oktoba 21, 2026, Mwananchi ilipotembelea baadhi ya vituo vya bajaji ilishuhudia vyombo hivyo vikiendelea na shughuli zake, ingawa idadi yake ilikuwa ndogo ikilinganishwa na ilivyozoeleka.

Maeneo yaliyokuwa na bajaji ni pamoja na Kabwe, katika njia ya kuelekea Isanga, barabara ya Shewa, Iyunga na baadhi ya njia zinazoelekea katikati ya jiji.

Wananchi walalamikia gharama za usafiri

Kusitishwa kwa huduma za bajaji kumeibua changamoto kwa wananchi waliokuwa wakitegemea usafiri huo kufika kwenye shughuli zao za kila siku.

Baadhi yao walilazimika kutembea kwa miguu, huku wengine wakikodi bodaboda kwa gharama zilizofikia Sh5,000 au zaidi, kutegemea makubaliano na umbali wa safari.

Kwa mfano, safari kutoka Kabwe hadi Uhindini, eneo lenye ofisi nyingi za umma, iligharimu kati ya Sh5,000 na zaidi kwa bodaboda ilihali siku za kawaida huwa ni kati ya Sh1,000 mpaka Sh2,000. Hata hivyo, gharama zilitofautiana kulingana na makubaliano kati ya abiria na madereva.

Katika kipindi hicho, baadhi ya wananchi pia walitumia matoroli kama njia mbadala ya usafiri.

Judith Mteleko amesema kukosekana kwa bajaji kumewaathiri wananchi wengi kwa kuwa usafiri huo ni muhimu katika kuwafikisha kwenye shughuli zao za kila siku.

“Binafsi nimekubaliana tupunguze hata vitambi. Daladala zenyewe hazipo, ni mwendo wa bodaboda tu na gharama zao kubwa,” amesema Judith.

Kwa upande wake, Jeremia John, maarufu kama JJ, amesema licha ya changamoto wanazokutana nazo wananchi, Sagini anapaswa kuendelea kusimamia msimamo wake ili kuhakikisha sheria zinafuatwa.

“Mkuu wa Mkoa tuko naye pamoja. Tutaumia kwa muda mfupi, ila huko mbele tutaheshimiana. Mbeya ni jiji, lakini bajaji waliifanya kuwa kichaka. Sheria izingatiwe,” amesema JJ.

Madereva wa daladala walia

Wakati wananchi wakieleza athari za kukosekana kwa bajaji, baadhi ya madereva wa daladala wamelalamikia kile walichodai kuwa ni kuingiliwa katika utekelezaji wa majukumu yao na madereva wa bajaji.

Dereva mmoja wa daladala, ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema amesikitishwa na madai ya madereva wa bajaji kuwavamia wakiwa na abiria na kuharibu vyombo vyao.

“Wao wanalazimisha kutuingiza kwenye mgogoro usiotuhusu. Sisi tukiwa na shida tunaimaliza wenyewe bila kuwaingilia wala kuwabughudhi,” amesema.

Amedai baadhi ya madereva wa daladala wamekuwa wakipigwa mawe na abiria kushushwa wakati wa matukio hayo, akisema hali hiyo haikubaliki kwa kuwa wananchi wanahitaji huduma za usafiri badala ya kushuhudia migogoro.

“Wanatupiga mawe, wanashusha abiria. Hii si sawa. Kila mmoja atimize wajibu wake. Wananchi wanahitaji kupata huduma wala si haya yanayoendelea,” amesema.

Dereva huyo amesema utaratibu uliowekwa na Serikali una manufaa kwa kuwa unawawezesha madereva wa bajaji kutoa huduma katika umbali mfupi kwa nauli ileile, hivyo amewataka kuendelea na shughuli zao kwa kuzingatia maelekezo yaliyotolewa.

Source link