Musoma. Ukosefu wa mitaji, masoko na teknolojia ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili vijana wanaotaka kuwekeza katika kilimo misitu, huku wadau wakitaka kuimarishwa kwa huduma za ugani, utafiti wa mbegu bora na upatikanaji wa masoko ya uhakika.
Wito huo umetolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gerald Kusaya wakati akifungua Kongamano la 11 la Kilimo Misitu, linalolenga kujadili fursa za uwekezaji kwa vijana.
Kusaya amesema licha ya jitihada zinazofanywa na Serikali, sekta hiyo bado inakabiliwa na changamoto zinazohitaji ushirikiano wa wadau ili kuongeza uzalishaji na kujenga mnyororo wa thamani.
Amesema mitaji na teknolojia ni miongoni mwa nyenzo muhimu katika kufanikisha uwekezaji, lakini upatikanaji wake bado ni changamoto kwa vijana wanaotaka kujishughulisha na sekta hiyo.
“Wadau wote tukiungana tukahakikisha utafiti unafanyika, mitaji inapatikana, matumizi sahihi ya teknolojia kutangaza bidhaa na kutafuta masoko pamoja na mambo mengine, hakika kutakuwa na mnyororo wa thamani katika sekta hii ya kilimo misitu,” amesema.
Ameongeza kuwa vyuo vikuu, wabia wa maendeleo na taasisi nyingine zina nafasi muhimu katika kutatua changamoto hizo, akisema Mkoa wa Mara una fursa nyingi zinazoweza kutumiwa kukuza sekta hiyo.
Wito huo unakuja wakati vijana wakitaka fursa za uwekezaji katika kilimo ziambatane na hatua za vitendo zitakazowasaidia kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kujiajiri.
Mmoja wa washiriki wa kongamano hilo, Joel Matiku amesema uwekezaji kwa vijana ni muhimu kwa maendeleo ya taifa, hivyo maazimio ya mikutano kama hiyo yanapaswa kutekelezwa.
“Kuwekeza kwa vijana ni kuwekeza katika mustakabali wa maendeleo ya taifa, hivyo hili jambo linatakiwa kutekelezwa kwa vitendo na si kuishia kwenye makongamano pekee,” amesema.
Akitoa taarifa kuhusu kongamano hilo, Meneja wa Shirika la Vi Agroforestry nchini, Martha Olotu amesema zaidi ya watu 8,000 wanatarajiwa kushiriki katika kongamano hilo la kimataifa linalolenga kufungua fursa za uwekezaji na biashara kwa vijana.
Amesema kongamano hilo linakusudia kubaini fursa zinazoweza kutekelezeka katika sekta hiyo na kuchangia ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, usalama wa chakula na maendeleo endelevu, hususan maeneo ya vijijini.
Olotu amesema kilimo misitu kinaweza kuboresha rutuba ya udongo, kuimarisha upatikanaji wa maji, kurejesha bioanuwai na kuongeza kipato cha wananchi wa vijijini.
Ameeleza kuwa kongamano hilo ni sehemu ya juhudi za kuunga mkono uhifadhi wa mazingira, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha usimamizi endelevu wa ardhi.
Amesema programu ya mageuzi ya usimamizi wa mazingira inalenga pia kuunga mkono dhamira ya kupanda miti bilioni 10 ifikapo mwaka 2030, huku kilimo misitu kikitajwa kuwa miongoni mwa njia zinazoweza kusaidia kufikia malengo hayo.
Kwa upande mwingine, baadhi ya washiriki wameitaka Serikali kuweka sera madhubuti za kulinda mazao ya asili yaliyo katika hatari ya kutoweka, yakiwamo maboga, mchicha, njugumawe, karanga na uwele.
Mwakilishi wa Shirika la Tabio, Girantha Girantha amesema mazao hayo yana manufaa kwa afya ya binadamu na rutuba ya ardhi, hivyo yanapaswa kuendelezwa ili yasipotee kutokana na msisitizo unaowekwa katika mazao ya kisasa.
Amesema dhana kwamba mazao ya asili hayazai vya kutosha si sahihi, akieleza kuwa yakilimwa kwa kufuata kanuni bora za kilimo, ikiwamo matumizi ya mbolea za asili, yanaweza kutoa mavuno mazuri.


