Wanawake 55 Tanga wagundulika na saratani ya matiti
4 mins read

Wanawake 55 Tanga wagundulika na saratani ya matiti

Tanga. Wanawake 55 wamegundulika kuwa na saratani ya matiti mkoani Tanga kati ya Januari na Agosti 2026, huku wengi wao wakibainika kuwa katika hatua za tatu na nne za ugonjwa huo, hali inayosisitiza umuhimu wa uchunguzi wa mapema.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Burian amesema hayo leo Jumatano, Oktoba 21, 2026, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu juhudi za kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa uchunguzi wa awali wa saratani ya matiti.

Amesema programu maalumu ya uchunguzi itafanyika kuanzia Oktoba 28 hadi 30, 2026, katika maeneo yaliyochaguliwa mkoani humo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha utambuzi wa mapema wa ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa takwimu za huduma za afya, wanawake 45,068 walifanyiwa uchunguzi wa awali wa matiti kati ya Januari na Agosti mwaka huu, ambapo 1,457 walibainika kuwa na matokeo yasiyo ya kawaida yaliyohitaji uchunguzi zaidi.

Ameongeza kuwa wanawake 1,018 walipata huduma za uchunguzi wa kina, vikiwamo vipimo vya picha na uchukuaji wa sampuli kulingana na mahitaji ya kitabibu.

Dk Burian amesema ugonjwa huo unapogundulika mapema na mgonjwa kupata matibabu sahihi, uwezekano wa kupata matokeo mazuri ya matibabu huongezeka.

Hata hivyo, amesema changamoto kubwa katika mapambano dhidi ya saratani ya matiti ni baadhi ya wagonjwa kuchelewa kufika katika vituo vya afya, hali inayosababisha ugonjwa kugundulika katika hatua za mwisho na kufanya matibabu kuwa magumu zaidi.

“Saratani ya matiti inaweza kumpata mwanamke au mwanaume, hivyo amewataka wananchi kuzingatia afya zao na kuwahi kupata huduma za uchunguzi wanapoona mabadiliko yasiyo ya kawaida kwenye matiti,” amesema Dk Burian.

Amezitaja dalili zinazopaswa kuzingatiwa kuwa ni uvimbe kwenye titi au kwapani, mabadiliko ya ukubwa au umbo la titi, mabadiliko ya ngozi au chuchu, chuchu kuvutika ndani kwa namna isiyo ya kawaida na kutoka kwa majimaji yasiyo ya kawaida kwenye chuchu, hasa yenye damu.

Amesema huduma za uchunguzi wa awali wa saratani ya matiti zinapatikana katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga (Bombo), hospitali za halmashauri na vituo vya afya.

Amewahimiza wananchi kutumia huduma hizo na kujitokeza kwa wingi katika zoezi maalumu la uchunguzi litakalofanyika Oktoba 28 hadi 30 mwaka huu.

Kwa upande wake, kiongozi wa programu ya uchunguzi wa awali wa saratani ya matiti Mkoani Tanga, Dk Rashed Suleiman amesema historia ya ugonjwa huo katika familia ni miongoni mwa vihatarishi vinavyoweza kuongeza uwezekano wa mtu kupata saratani ya matiti.

Amesema mtu mwenye ndugu wa karibu, kama mama au shangazi, aliyewahi kuugua saratani ya matiti anaweza kuwa katika hatari kubwa zaidi, akieleza kuwa sababu za kurithi huchangia takribani asilimia tano ya wagonjwa wa ugonjwa huo.

Ametaja vihatarishi vingine kuwa ni umri mkubwa, hasa kuanzia miaka 50, kuanza hedhi kabla ya kufikisha miaka 12 na kutokoma hedhi.

Amesema ingawa saratani ya matiti huathiri zaidi wanawake, wanaume pia wanaweza kupata ugonjwa huo, wakichangia kati ya asilimia mbili na tano ya wagonjwa.

Naye Dk Sande Wanyika, mtaalamu wa ufundi kutoka shirika lisilo la kiserikali la JHPIEGO, amesema shirika hilo, kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, limefanikisha mafunzo kwa watoa huduma za afya kuhusu uchunguzi wa saratani ya matiti.

Amesema mafunzo hayo yamejumuisha kuwajengea uwezo wataalamu wa uchunguzi wa picha ili waweze kutambua dalili za awali za ugonjwa huo.

“Tunafahamu ya kwamba saratani ya matiti ni moja kati ya magonjwa yanayowaathiri kina mama na pia ni saratani inayosababisha vifo vingi endapo mtu atachelewa kupata matibabu. Ndiyo maana tukaona umuhimu wa kushirikiana na Serikali katika programu hii,” amesema Wanyika.

Ameeleza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuimarisha uwezo wa watoa huduma za afya kutambua dalili za ugonjwa mapema na kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma zinazostahili kwa wakati.

Wataalamu hao wamewahimiza wananchi kutopuuza mabadiliko yasiyo ya kawaida kwenye matiti na kuwahi katika vituo vya afya kwa uchunguzi.

Wamesisitiza kuwa si kila uvimbe kwenye titi ni saratani, lakini ni muhimu kupata tathmini ya kitaalamu ili kubaini chanzo cha mabadiliko hayo na kuchukua hatua zinazofaa.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *