Wanne kortini tuhuma za kutapeli kwa kutumia majina ya Try Again, Mwanaid Majaar
4 mins read

Wanne kortini tuhuma za kutapeli kwa kutumia majina ya Try Again, Mwanaid Majaar

Dar es Salaam. Mfanyabiashara Joseph Mzava (23), maarufu Joe, na wenzake watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 31, yakiwemo ya kuongoza genge la uhalifu, kujitambulisha kwa majina ya watu maarufu na kujipatia Sh16 milioni kwa njia ya udanganyifu.

Mzava anadaiwa kujitambulisha kwa majina ya Salim Abdallah Mhene, maarufu Try Again, na Balozi Mwanaid Majaar, kwa lengo la kuwatapeli watu waliodhani wanachangia shughuli za kijamii.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, Mzava alidaiwa kutumia jina la Try Again, anayedaiwa kukusanya fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha watoto yatima, pamoja na jina la Balozi Mwanaid Majaar, aliyedaiwa kuchangisha fedha kwa ajili ya mkutano wa uwezeshaji wanawake viongozi uliotarajiwa kufanyika Julai 25, 2026.

Washtakiwa wengine ni Vernand Meshack (30), mfanyabiashara na mkazi wa Segerea; Frank Kusenha (30), maarufu kama Mrefu, fundi na mkazi wa Magore, Ukonga; na Edson Kamalamo (26), mkazi wa Kisalawe.

Washtakiwa wanne wanaokabiliwa na mashtaka 31 wakiwa chini ya ulinzi wa askari Polisi, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam. Picha na Hadija Jumanne

Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo leo, Oktoba 22, 2026, na kusomewa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi namba 23933 ya mwaka 2026 na Wakili wa Serikali Michael Shindai, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Salome Mshasha.

Kati ya mashtaka 31 yanayowakabili, 24 yanahusu matumizi ya laini za simu zilizosajiliwa kwa majina ya watu wengine, matatu ni ya kujitambulisha kwa njia isiyo halali, mawili ni ya kujipatia fedha kwa udanganyifu, moja ni la kuongoza genge la uhalifu na jingine ni la kutakatisha fedha.

Kabla ya kusomewa mashtaka, Hakimu Mshasha aliwaeleza washtakiwa kuwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Pia, shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Akiwasomea mashtaka hayo, Wakili Shindai alidai katika shtaka la kwanza kuwa washtakiwa kwa pamoja waliongoza genge la uhalifu kati ya Julai 1 na Agosti 14, 2025, katika eneo lisilofahamika ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuwahadaa watu na kujitambulisha kwa njia isiyo halali, kisha kujipatia Sh16 milioni.

Katika shtaka la pili, Mzava pekee yake anadaiwa Agosti 13, 2025, katika eneo lisilofahamika nchini, kutumia mfumo wa kompyuta kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp kujitambulisha kwa Hamis Masoud Pelle kuwa yeye ni Salim Abdallah Mhene, maarufu Try Again, kwa lengo la kumtapeli.

Katika shtaka jingine, Mzava anadaiwa Julai 2026, katika eneo lisilofahamika nchini, kutumia WhatsApp kujitambulisha kwa Seleiman Haji Suleiman kuwa yeye ni Balozi Mwanaid Majaar, akidaiwa kuwa na lengo la kumtapeli.

Vilevile, anadaiwa katika kipindi hicho kutumia mtandao huo kujitambulisha kwa Seleiman Haji Suleiman kuwa yeye ni Salim Abdallah Mhene, maarufu kama Try Again, wakati akijua kuwa si kweli.

Washtakiwa wanne wanaokabiliwa na mashtaka 31 wakiwa chini ya ulinzi wa askari Polisi, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam. Picha na Hadija Jumanne

Katika shtaka la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, Mzava anadaiwa Agosti 14, 2025, kujipatia Sh16 milioni kupitia akaunti ya benki ya Equity iliyokuwa kwa jina la Edson Kamalamo. Fedha hizo zinadaiwa kutoka katika akaunti ya CRDB ya Hamis Pelle baada ya Mzava kujitambulisha kuwa Try Again, aliyekuwa akikusanya fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha watoto yatima.

Pia, Mzava anakabiliwa na shtaka jingine la kujipatia fedha kwa udanganyifu. Anadaiwa Julai 21, 2026, kujipatia Sh1 milioni kupitia namba ya simu iliyosajiliwa kwa jina la Mwanaidi Samweli, kutoka kwa Suleiman Suleiman, baada ya kujitambulisha kuwa Balozi Mwanaid Majaar.

Kwa mujibu wa mashtaka, fedha hizo zilidaiwa kuchangwa kwa ajili ya mkutano wa uwezeshaji wanawake viongozi uliotarajiwa kufanyika Julai 25, 2026, wakati Mzava akijua kuwa madai hayo si ya kweli.

Mashtaka ya saba hadi ya 30 yanamhusu Mzava pekee yake. Anadaiwa Oktoba 6, 2026, katika eneo la Kwembe, Wilaya ya Ubungo, kutumia laini za simu zilizosajiliwa kwa majina ya watu wengine bila kutoa taarifa kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Shtaka la 31 linawahusu washtakiwa wote na ni la kutakatisha fedha. Wanadaiwa kutakatisha Sh16 milioni kati ya Julai 1 na Agosti 14, 2025, huku wakijua kuwa fedha hizo zilitokana na kosa la kuongoza genge la uhalifu.

Upande wa mashtaka ulieleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo mahakama iliahirisha kesi hadi Novemba 4, 2026, itakapotajwa tena.

Washtakiwa wote wamepelekwa mahabusu kutokana na shtaka la utakatishaji fedha linalowakabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *