Mgombea wa AAFP, aahidi kutatua kero za wakulima Chamwino
Chamwino. Mgombea ubunge wa Jimbo la Chamwino kupitia Chama cha Wakulima (AAFP), Exavery Mapunda, ameahidi kutatua changamoto zinazowakabili wakulima, zikiwamo ucheleweshaji wa malipo ya mazao na migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji.
Akizungumza na Mwananchi jijini Dodoma leo Alhamisi, Oktoba 22, 2026, Mapunda amesema wakulima wanakabiliwa na changamoto za kucheleweshewa fedha za mazao yao, hali inayowaathiri katika kuendesha shughuli zao za kiuchumi.
Amesema licha ya kuwepo kwa maofisa kilimo na maofisa ugani, bado kuna changamoto katika usimamizi wa shughuli za kilimo na mifumo ya ununuzi na uuzaji wa mazao.
Amesema wakulima wanahitaji mfumo ulio wazi unaowawezesha kuelewa namna bei za mazao zinavyopangwa na malipo yao yanavyofanyika ili wapate fedha zao kwa wakati.
“Nikipata nafasi ya kuwatumikia wananchi wa Chamwino, nitashughulikia kero hizo kwa lengo la kuhakikisha wakulima wanapata haki zao na shughuli za kilimo zinaendeshwa kwa utaratibu unaozingatia masilahi yao,” amesema Mapunda.
Kuhusu migogoro ya ardhi, amesema anataka kuwepo kwa utaratibu wa wazi wa kutenga maeneo ya wakulima, wafugaji na matumizi ya Serikali, huku mazingira yakilindwa ili kupunguza migogoro inayoweza kuzuilika.
Katika sekta ya elimu, Mapunda amesema atapigania kupunguza michango inayotozwa kwa wanafunzi wa shule za sekondari za Serikali, akieleza kuwa gharama hizo zinaongeza mzigo kwa wazazi na walezi, hasa familia zenye kipato cha chini.
Amesema juhudi hizo zitahusisha pia kushughulikia gharama zinazohusiana na mitihani ili kupunguza changamoto zinazowakabili wanafunzi na familia zao.
Aidha, ameahidi kuweka kipaumbele katika ujenzi na uboreshaji wa barabara, madaraja na shule ili kuboresha huduma kwa wananchi wa Chamwino, ambao kwa mujibu wake, sehemu kubwa hutegemea kilimo kujipatia kipato.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa AAFP, Yusufu Rashid, amewataka wananchi wa Chamwino kumchagua Mapunda, akisema jimbo hilo linahitaji kiongozi mwenye uthubutu wa kuwasemea wananchi wote bila kujali itikadi zao za kisiasa.
“Ni wakati sahihi wa kumchagua mgombea wa AAFP ili awaletee maendeleo ambayo mmeyasubiri kwa muda mrefu,” amesema Rashid.

