Ufaransa yaripoti mgonjwa wa kwanza wa virusi vya Shamonda
Dar es Salaam. Ufaransa imeripoti mgonjwa wa kwanza aliyeambukizwa virusi vya Shamonda, ambavyo awali vilijulikana kuathiri wanyama, hasa ng’ombe, hali iliyochochea uchunguzi kuhusu uwezekano wa virusi hivyo kuambukiza binadamu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mamlaka za Ufaransa Alhamisi, Oktoba 22, 2026, mgonjwa huyo alikuwa akipatiwa matibabu katika hospitali za umma za Lyon kutokana na ugonjwa mwingine mkali na alikuwa na kinga dhaifu sana ya mwili.
Mgonjwa huyo alifariki mapema Oktoba, ingawa uchunguzi unaendelea kubaini iwapo virusi vya Shamonda vilichangia kifo chake.
Shirika la Habari la Reuters limeripoti kuwa mamlaka za Ufaransa zinahisi huenda mgonjwa huyo aliambukizwa baada ya kung’atwa na mdudu aina ya Culicoides mashariki mwa nchi hiyo. Katika eneo hilo, virusi hivyo vilikuwa vikizunguka miongoni mwa wanyama wakati wa masika na kiangazi mwaka huu.
Katika taarifa yake, Wizara ya Kilimo ya Ufaransa imesema: “Kwa kuzingatia maarifa yaliyopo kuhusu virusi hivi, hakuna hatari ya kiafya kwa umma kwa ujumla iliyobainika hadi sasa.”
Wizara hiyo iliongeza kuwa mgonjwa huyo alikuwa katika hali ya kipekee kutokana na udhaifu mkubwa wa kinga ya mwili. Uchunguzi wa kitabibu, maabara na epidemiolojia unaendelea kubaini namna maambukizi yalivyotokea.
Virusi vya Shamonda ni sehemu ya kundi la Orthobunyavirus, linalohusisha virusi vinavyoweza kuenezwa kwa wanyama kupitia wadudu wadogo wanaouma.
Virusi hivyo vilitambuliwa kwa mara ya kwanza nchini Nigeria katikati ya miaka ya 1960 na baadaye kuripotiwa kwa vipindi tofauti kwa ng’ombe katika maeneo ya Afrika Magharibi, Mashariki na Kusini, pamoja na Japan.
Kwa mujibu wa Kituo cha Ulaya cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa (ECDC), virusi hivyo viligunduliwa kwa mara ya kwanza katika mifugo barani Ulaya wakati wa kiangazi cha mwaka 2026. Baadaye viliripotiwa katika nchi kadhaa za Ulaya, zikiwemo Ufaransa, Ujerumani, Austria na Italia.
ECDC imesema inaendelea kufuatilia hali hiyo kwa kushirikiana na mamlaka za Ufaransa na washirika wengine wa Ulaya ili kutathmini athari zinazoweza kujitokeza kwa afya ya umma.
Kituo hicho pia kimeeleza kuwa uchunguzi unaendelea kubaini namna mgonjwa huyo alivyoambukizwa na iwapo virusi hivyo vilichangia kifo chake.
Kwa upande wake, Shirika la Afya Duniani (WHO), katika taarifa iliyotolewa kwa Reuters, limesema uwezekano wa virusi hivyo kusababisha maambukizi mapana kwa binadamu ni mdogo, kwa kuzingatia taarifa zilizopo na namna virusi vinavyohusiana navyo huenezwa.
“Kwa kuzingatia taarifa zilizopo na maarifa kuhusu uenezaji wa virusi vinavyohusiana na hivi, hili ni tukio la maambukizi ya mtu mmoja na hakuna uwezekano mkubwa wa kusababisha kuenea zaidi kwa sasa,” WHO ilisema.
Mamlaka za Ufaransa zimezitaarifu WHO na ECDC kuhusu tukio hilo, huku uchunguzi ukiendelea kwa kushirikisha wataalamu wa afya ya binadamu, wanyama na mazingira.
Licha ya kugunduliwa kwa mgonjwa huyo, mamlaka zimesisitiza kuwa hadi sasa hakuna hatari iliyobainika kwa umma kwa ujumla. Hata hivyo, uchunguzi unaendelea kufafanua namna maambukizi yalivyotokea na iwapo kuna mazingira yanayoweza kuruhusu virusi hivyo kuathiri binadamu wengine.

