Ziara ya Ndejembi Mbeya, njia 106 zafunguliwa
2 mins read

Ziara ya Ndejembi Mbeya, njia 106 zafunguliwa

Mbeya. Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) Mkoa wa Mbeya umeanza kufungua barabara za pembezoni mwa mradi wa ujenzi wa njia nne unaoendelea ili kuondoa changamoto za foleni kwa watumiaji wa njia hizo.

Hii ni hatua ya utekelezaji wa agizo la Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi wakati wa ziara yake jijini Mbeya Oktoba 16 na 17, akielekeza kufunguliwa kwa njia za pembezoni ili kuruhusu shughuli za kiuchumi kufanyika vyema kwa wananchi.

Ikumbukwe miongoni mwa miradi mikubwa na ya kimkakati inayotekelezwa jijini Mbeya ni pamoja na ujenzi wa barabara ya njia nne yenye urefu wa kilomita 29 kutoka Nsalaga hadi Ifisi unaogharimu Sh 138 bilioni.

Meneja wa Tanroads Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Suleman Bishanga amesema katika kutekeleza maagizo ya serikali, tayari maeneo 106 yamefunguliwa ili kuruhusu shughuli za uchumi zinaendelea.

Amesema katika kuhakikisha ujenzi huo unaendelea na kukamilika kwa wakati, wamemuagiza mkandarasi kufanya kazi usiku na mchana ili kumaliza changamoto ya barabara hiyo kwa watumiaji.

“Hapa tulipo ni eneo la Stendi ya Kabwe, ambalo ni sehemu ya mradi wa ujenzi wa barabara ya njia nne, Makamu wa Rais alitoa maelekezo kwamba njia zote ambazo wananchi wanatumia zifunguliwe,” amesema Bishanga.

“Tayari maeneo 106 yamefunguliwa yanaendelea kufanyiwa kazi katika hatua mbalimbali ikiwamo kuyajazia ili yaweze kupitika, tunaendelea kutekeleza vyema maagizo ili kuondoa adha kwa wananchi na kazi inaenda pamoja,” ameongeza.

Kwa upande wake, Frank Kamara ambaye ni mhandisi Tanroads, amesema ujenzi unaendelea vyema ambapo upande wa eneo la Inyala wanatarajia kupanua ili kuondokana na ajali zilizokuwa zikijitokeza mara kwa mara.

“Kwanza tunaboresha eneo hili tukijenga daraja kwa lengo la kutanua sehemu hii ambayo ilikuwa changamoto kwa ajali, tumefanya uamuzi wa kutenganisha njia kati ya magari makubwa, madogo na kwa watembea kwa miguu,” amesema mhandisi huyo.

Naye, Gerina Mhando amesema ujenzi wa daraja hilo umefikia asilimia 75, akieleza kuwa kasi iliyopo matarajio yao ni kabla ya kuanza kunyesha mvua, shughuli itakuwa imekamilika.

“Tunafanya kazi usiku na mchana, ujenzi kwa sasa wa daraja hili upo asilimia 75 na matarajio yetu ni kabla hizi mvua tuwe tumemaliza ili kuruhusu shughuli za wananchi kuendelea,” amesema Gerina, mhandisi wa Tanroads.

Mmoja wa wananchi jijini Mbeya, Esau Msuya amepongeza juhudi zinazofanywa na serikali, akieleza kuwa ziara ya Makamu wa Rais, Ndejembi imekuwa na manufaa kwa wananchi.

“Mfano, hizi barabara za Ilomba na vivuko vimefanyiwa kazi, tunashukuru serikali kwa utekelezaji huu na tunatarajia kuona ujenzi ukikamilika na kuondoa changamoto hizi,” amesema Msuya.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *