Mradi wa maji wa Sh300 bilioni watoa matumaini
Same. Kwa takribani miongo miwili, wakazi wa Kijiji cha Ishinde, Wilaya ya Same, Mkoa wa Kilimanjaro, wamekuwa wakitumia saa kadhaa kutafuta maji, muda ambao ungeweza kutumika kwa masomo, kilimo, biashara na shughuli za nyumbani.
Awali, baadhi ya wanakijiji walitembea kwa saa nne hadi tano kutafuta dumu moja la maji lenye ujazo wa lita 20.
Leo, umbali huo umepungua kwa baadhi ya wakazi kutokana na hatua zilizochukuliwa na Serikali kupitia Mradi wa Maji wa Same-Mwanga-Korogwe.
Hata hivyo, kwa wakazi wengi, hasa wa vitongoji vitatu kati ya vitano vya kijiji hicho, upatikanaji wa maji ya uhakika bado ni changamoto ya kila siku.
Mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Sh300 bilioni, uliozinduliwa Machi mwaka jana, unatarajiwa kuzalisha lita milioni 103 za maji kwa siku utakapokamilika, kutoka lita milioni 51.5 zinazozalishwa kwa sasa. Awamu ya kwanza ya mradi huo inahudumia takribani watu 100,000 katika mikoa ya Kilimanjaro na Tanga.
Kwa sasa, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi huo, huku tarehe za kuanza na kukamilika kwake zikiwa hazijajulikana. Mradi mzima utakapokamilika, unatarajiwa kuwahudumia takribani watu 450,000 ifikapo mwaka 2038.
Kijiji cha Ishinde kina vitongoji vitano; Ishinde Stendi, Kibaoni Igongo, Kigogo, Kisakeni na Morondwe. Wakati wakazi wa Kibaoni na Ishinde Stendi wameanza kuona maboresho, wengine bado hukaa siku kadhaa bila kupata maji ya uhakika.
Kwa familia hizo, changamoto si kutafuta maji pekee. Uhaba huo unaathiri mahudhurio ya watoto shuleni, matumizi ya fedha za kaya, uwezo wa wakulima kuzalisha mboga na muda ambao wananchi wanaweza kutumia katika shughuli za kuwaingizia kipato.
Katika Kitongoji cha Morondwe, wakazi hutegemea mfumo wa maji unaotumia nishati ya sola uliotolewa na Serikali.
Hata hivyo, mwanga wa jua unapokuwa hafifu, mfumo huo hushindwa kusukuma maji ya kutosha. Katika siku kama hizo, baadhi ya wakazi hulazimika kutumia Sh6,000 kununua madumu matano ya maji.
Kwa Mariam Mshana(75), ambaye ameishi Morondwe tangu alipofunga ndoa mwaka 1975 kutafuta maji bado ni kazi ngumu.
Anakumbuka kipindi ambacho wakazi walitumia hadi saa tano kwenda na kurudi Vumari kutafuta dumu moja la maji lenye ujazo wa lita 20.
“Katika umri wangu, siwezi kuchota maji mengi. Nikibeba dumu moja, nalazimika kupumzika mara mbili au tatu kabla sijafika nyumbani. Katika familia ya watu watano, tunahitaji zaidi ya madumu matano kwa siku,” anasema.
Anasema uhaba huo pia unaathiri watoto, baadhi yao huenda shuleni wakiwa wamevaa nguo chafu kutokana na kukosekana kwa maji ya kutosha nyumbani, huku wengine wakikosa kabisa kwenda shule.
Mshana anasema juhudi za awali za kuboresha upatikanaji wa maji hazikudumu, kwa kuwa miundombinu ilipoharibika, mambo yalikuwa yale yale.
Kilimo, kipato chadhoofika
Mwenyekiti wa kitongoji cha Morondwe, Juma Mshana anasema eneo hilo lina ardhi yenye rutuba, lakini wakazi hawawezi kuitumia kikamilifu tangu mradi wa maji uliodhaminiwa na Rotary Club uliposimama.
Pia, anasema kukosekana kwa huduma ya maji ya uhakika kumewalazimu wakazi kutumia muda mwingi kutafuta maji, badala ya kuutumia katika kilimo na shughuli nyingine za kuwaingizia kipato.
“Tungekuwa na majisafi na salama, wakazi wasingekuwa na sababu ya kushindwa kushiriki katika shughuli za Serikali. Kutojua ni lini tutapata maji au kwa nini hatuyapati kunaua morali ya watu kushiriki katika shughuli nyingine za kijamii,” anasema.
Katika Kitongoji cha Kisakeni, changamoto ya upatikanaji wa maji inaendelea kujitokeza licha ya juhudi zilizofanywa na Serikali.
Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Sesilia Mgala anasema Serikali iliweka tangi la maji la jamii nje ya Mradi wa Maji wa Same-Mwanga-Korogwe, lakini huduma hiyo hukosekana kwa siku tatu au nne mfululizo.
“Mradi wa Maji wa Same-Mwanga-Korogwe ulipoanzishwa, wengi wetu tuliweka miundombinu muhimu majumbani kwa sababu tulitarajia kupata maji. Kwa bahati mbaya, eneo letu halikuunganishwa na mradi huo. Katika umri wangu wa miaka 62, nitaendeleaje kutembea kwa takribani saa moja kwenda kuchota ndoo ya maji?” anahoji.
Uhaba huo pia unaathiri wakulima na wafugaji, wanaokabiliwa na ugumu wa kumwagilia mazao na kupata maji ya kutosha kwa mifugo yao.
Deusdedit Mchala, mkazi wa eneo la Mareti, Kisakeni, anasema takribani familia 16 zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji.
“Hatuwezi kujenga nyumba za kisasa kwa sababu ya ukosefu wa maji. Hali ya sasa ya uchumi na kupanda kwa gharama za maisha kumeifanya kuwa ngumu zaidi kwetu,” anasema.
Anasema wakati mwingine watoto huenda shuleni wakiwa wamevaa sare chafu kutokana na ukosefu wa maji, huku akionya kuwa hali hiyo inaweza kuongeza hatari za kiafya wakati wa milipuko ya magonjwa.
Katika Kitongoji cha Kigogo, uhaba wa maji umegeuka kuwa mzigo wa kifedha kwa kaya zinazolazimika kulipia maji na usafirishaji wake.
Katika mahojiano na gazeti dada la Mwananchi, The Citizen, yaliyofanyika Agosti 2026, Flomina Mgonja alisema tangu Aprili 26, wakazi walikuwa hawajapata maji na walilazimika kulipa Sh3,000 kusafirisha ndoo tano za maji kwa pikipiki.
“Hapo awali tulikuwa na maji yaliyodhaminiwa na Rotary Club, lakini mradi huo uliisha wakati mradi wa sasa ulipoanza, jambo lililotuacha na kiu na kutufanya tutumie fedha na muda mwingi kutafuta maji,” anasema.
Mgonja anasema uhaba huo umeathiri pia kilimo cha bustani, baadhi ya wakazi wameacha kulima na kuuza mboga kwa sababu hawana maji ya kutosha kumwagilia mazao yao.
Akizungumzia hali hiyo, Mhandisi Emmanuel Maghembe wa Mradi wa Maji wa Same-Mwanga-Korogwe, anasema tatizo la maji Kigogo lilisababishwa na kuharibika kwa pampu, na Serikali ilitumia Sh10 milioni kurejesha huduma hiyo.
Kuhusu Kisakeni, anasema baadhi ya kaya zilizo katika maeneo ya mwinuko bado hazijafikiwa na miundombinu ya maji.
Pamoja na changamoto zinazowakabili wakazi wa baadhi ya vitongoji, hali ya upatikanaji wa maji katika maeneo mengine ya Ishinde imeimarika.
Godfrey Mbwambo, mkazi wa Ishinde Stendi anasema upatikanaji wa majisafi na salama umeboreshwa kwa jumla, ingawa baadhi ya kaya bado hulazimika kutembea umbali fulani kutafuta maji.
“Ninafurahi kwamba upatikanaji wa majisafi na salama katika Kitongoji cha Ishinde Stendi umeboreshwa, lakini bado baadhi ya wakazi wanaotembea kwa dakika 30 kwenda kuchota maji, hasa wale ambao nyumba zao hazijawekewa miundombinu ya maji,” anasema.
Kwa upande wake, Maghembe anasema awali Ishinde haikuwa imejumuishwa katika awamu ya kwanza ya mradi.
Hata hivyo, baadaye Serikali ilielekeza maofisa kupanua huduma hiyo hadi vijiji vilivyo katika eneo la katikati ya Same na Mwanga.
Anasema Morondwe iko eneo la Ishenge, ambalo limejumuishwa katika awamu ya pili ya mradi na maandalizi ya utekelezaji tayari yameanza.
Anasema maeneo kama Mareti hayakuwa na wakazi wakati mradi ulipoundwa, lakini sasa yanaendelea kukua na hivyo yanahitaji kujumuishwa katika awamu ya pili.
Baadhi ya changamoto za upatikanaji wa maji katika maeneo hayo zinahusishwa pia na teknolojia inayotumiwa kusukuma maji.
Mtaalamu wa hali ya hewa, Ramadhan Shaba anasema jiografia ya milima ya Ishinde inaweza kuathiri kiwango cha mwanga wa jua kinachofika katika maeneo mbalimbali ya kijiji hicho.
Shaba anasema hewa yenye unyevunyevu inapopanda juu ya milima inaweza kupoa na kutengeneza mawingu, hali inayopunguza mwanga wa jua unaofika ardhini.
Anasema hali ya mawingu huwa ya kawaida zaidi katika miezi yenye mvua, hasa kuanzia Oktoba hadi Mei.
Anasema kwa jamii zinazotegemea mifumo ya maji inayoendeshwa kwa nishati ya sola, mawingu mazito na mvua vinaweza kupunguza nishati inayofika kwenye paneli za sola na hivyo kupunguza kiwango cha maji kinachoweza kusukumwa.
Shaba anasema mifumo hiyo inapaswa kubuniwa kwa kuzingatia hali ya hewa ya eneo husika na kuungwa mkono na uwezo wa kutosha wa kuhifadhi maji pamoja na mifumo mbadala ya uhakika.
Akizungumzia hatua zilizochukuliwa kukabiliana na changamoto hiyo, Maghembe anasema mradi mpya umeundwa kutoa huduma ya maji ya uhakika kupitia mfumo wa umeme wenye uwezo mkubwa wa kusukuma maji na uliounganishwa na Gridi ya Taifa.
“Tumeunganishwa na Gridi ya Taifa inayopita Iyungi na Hale. Lengo kuu ni kuhakikisha wananchi wote wanapata maji kupitia mradi huu, hata pale umeme unapokatika, isipokuwa pale hitilafu inapokuwa kwenye gridi ya Taifa,” anasema.

