Rais Mwinyi atangaza ufadhili wanafunzi watakaopata daraja la kwanza Zanzibar
4 mins read

Rais Mwinyi atangaza ufadhili wanafunzi watakaopata daraja la kwanza Zanzibar

Unguja. Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi ametangaza kuanzia mwakani, Serikali itatoa ufadhili kamili wa masomo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wote watakaopata Daraja la Kwanza lenye alama tatu hadi tano katika mitihani ya taifa, bila kujali fani wanayosoma.

Rais Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Oktoba 21, 2026 katika hafla maalumu iliyofanyika Ikulu ya Zanzibar kwa ajili ya kuwatambua na kuwapongeza zaidi ya wanafunzi 3,000 waliofanya vizuri zaidi katika mitihani ya taifa ya kidato cha nne na cha sita, kwa miaka mitatu kuazia mwaka 2024 hadi 2026.

Hafla hiyo ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya kuimarisha sekta ya elimu kama msingi wa kujenga uchumi imara na ustawi wa wananchi.

Akizungumzia uamuzi huo mpya Rais amesema, “Ningependa nitangaze leo hapa kwamba kuanzia mwakani wanafunzi wote watakaopata division one ya pointi tatu mpaka tano wote bila kujali fani, watapewa scholarship ya Serikali.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akizungumza katika hafla yakuwapongeza na kula nao chakula wanafunzi waliofaulu mtihani kidato cha nne na sita mwaka 2024/26 Ikulu Zanzibar

“Kwa hivyo kwa wale wa form four mlio hapa hakikisheni mnapata division one ya tatu mpaka tano alafu wewe utakuwa huna mkopo, wewe utasomeshwa na Serikali,” alisema.

Mbali na ahadi hiyo ya mwakani, Rais Mwinyi ametangaza kuwa kwa mwaka huu Serikali inatoa ufadhili wa masomo ya shahada ya kwanza kwa wanafunzi 143 waliopata daraja la kwanza ngazi ya juu katika kidato cha sita kupitia mpango wa SMZ Scholarship.

Aidha, alibainisha kuwa bajeti ya mikopo ya elimu ya juu imeongezeka kutoka Sh35 bilioni mwaka 2025/2026 hadi Sh45 bilioni kwa mwaka wa fedha 2026/2027, sawa na ongezeko la takriban asilimia 29.

Pia, alipongeza Benki ya CRDB kwa kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi watano waliotoka katika mazingira magumu.

Akiwasilisha taarifa ya ufaulu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Khamis Abdalla Said alieleza kuwa kiwango cha ufaulu wa kidato cha nne kimezidi kuimarika kutoka asilimia 82 mwaka 2024 hadi kufikia asilimia 92 mwaka 2025.

Baadhi ya wanafunzi waliofaulu mitihani yao kidato cha nne na sita mwaka 2024/26 wakiwa katika hafla ya kuwapongeza Ikulu Unguja Zanzibar.

“Wanafunzi waliopata daraja la kwanza mwaka 2024 walikuwa ni 1,150 sawa na asilimia 4.4 ya wanafunzi wote waliofanya mtihani. Na sasa imepanda hadi wanafunzi 1,434 kwa mwaka 2025 sawa na asilimia 6.9,” amesema

 Aliongeza kuwa idadi ya walipata daraja la sifuri ilipungua kutoka wanafunzi 4,700 sawa na asilimia 18 mwaka 2024 hadi wanafunzi 2,022 sawa na asilimia 10 mwaka 2025.

Kuhusu kidato cha sita, Katibu Mkuu alisema ufaulu wa jumla ulikuwa wanafunzi 4,830 sawa na asilimia 99.75 mwaka 2025 na wanafunzi 5,908 sawa na asilimia 99.53 mwaka 2026.

Alifafanua kuwa wanafunzi waliopata daraja la kwanza waliongezeka kutoka 992 sawa na asilimia 19.04 mwaka 2025 hadi 1,344 sawa asilimia 25.46 mwaka 2026. 

Katibu Mkuu pia alieleza kuwa Rais Mwinyi alinunua kompyuta mpakato (laptop) 4,000 kati ya mwaka 2023 na 2025 kwa ajili ya waliopata daraja la kwanza, na mchakato wa manunuzi unaendelea kwa wanafunzi 1,434 wa kidato cha nne (2025) na 1,344 wa kidato cha sita (2026).

“Katika wiki tatu zilizopita, Serikali imetoa Sh12.5 bilioni za mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi zaidi ya 11,000 huku wanafunzi 344 wakifadhiliwa masomo ya vyuo vya ndani na Dk Mwinyi tangu aingie madarakani,” amesema Said.

Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Mohammed Musa, alipongeza uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Nane katika miundombinu, zana za kisasa na masilahi ya walimu. 

Baadhi ya wanafunzi waliofaulu mitihani yao kidato cha nne na sita mwaka 2024/26 wakiwa katika hafla ya kuwapongeza Ikulu Unguja Zanzibar.

Waziri Lela alibainisha mafanikio ya kampeni ya kutokomeza daraja la sifuri akisema: “Unapoangalia takwimu mwaka 2020 wakati serikali ya awamu ya nane inaingia madarakani wanafunzi ambao walikuwa wakipata division zero (daraja sifuri) ilikuwa asilimia 42.5 kwa kidato cha nne… lakini jitihada za Serikali yako ndani ya miaka hii mitano tumefanikiwa kuishusha mpaka asilimia 10 kwa mwaka huu wa 2026”.

Waziri ameongeza kuwa wanafunzi waliopata Division One kidato cha nne walikuwa asilimia 1.2 tu mwaka 2020 lakini wameongezeka hadi asilimia 6.9 mwaka 2026. 

Kwa upande wa kidato cha sita, ufaulu wa daraja la sifuri amesema ulipungua kutoka asilimia 1.1 mwaka 2021 hadi asilimia 0.47 mwaka 2026.

Amewasihi wanafunzi kuendelea kujituma akisisitiza kuwa safari ya utaalamu na ubobezi ndiyo kwanza imeanza.

Mmoja wa wanafunzi waliopata ufaulu huo, Ali Suleiman Ali ambaye pia amepata Samia Scholarship kwenda Algeria, ameshukuru jitihada zinazochukuliwa na Serikali kuboresha miundombinu na kuimarisha sekta ya elimu akitaja umekuwa chachu ya mafanikio yao.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *