Viongozi wa vijiji Mtama, watuhumiwa kupewa fedha na wafugaji  
3 mins read

Viongozi wa vijiji Mtama, watuhumiwa kupewa fedha na wafugaji  

Mtama. Baadhi ya viongozi wa serikali za vijiji na wenyeviti wa vitongoji katika Halmashauri ya Mtama wanatuhumiwa kupokea fedha kutoka kwa wafugaji wanaoingiza mifugo katika maeneo yao, hali inayodaiwa kuchangia kuongezeka kwa mifugo inayoingia bila kufuata utaratibu.

Malalamiko hayo yameibuliwa leo Jumatano Oktoba 21, 2026, katika Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mtama.

Baadhi ya madiwani wameeleza wasiwasi wao kuhusu ongezeko la mifugo inayoingizwa katika maeneo ya vijiji bila utaratibu unaoeleweka, jambo linalozua changamoto kwa wananchi.

Wakizungumza kikaoni hapo, madiwani hao wamesema ongezeko la mifugo katika maeneo yao limeibua maswali kuhusu ufuatiliaji wake, vibali vya kuingia na hatua zinazochukuliwa na viongozi wa maeneo husika kudhibiti hali hiyo.

Diwani wa Namupa, Mohamed Kuokota amesema zaidi ya mifugo 500 imeingizwa katika kata yake, huku kukiwa na maswali kuhusu ilikotoka na utaratibu uliofuatwa kuifikisha katika eneo hilo.

Amesema hali hiyo inazua changamoto kwa wananchi, hasa pale mifugo inapokosa maeneo maalumu ya malisho na vyanzo vya maji vinavyotosheleza mahitaji ya wafugaji na jamii nyingine.

Pia, ameeleza wasiwasi wake kuhusu matumizi ya chanzo kimoja cha maji kwa binadamu na mifugo, akionya kuwa hali hiyo inaweza kuhatarisha afya za wananchi endapo usafi wa maji hautazingatiwa na hatua stahiki za kinga hazitachukuliwa.

“Niwaombe wenye mamlaka zinazohusika kufuatilia hali ya upatikanaji wa maji safi na salama, pamoja na kuweka utaratibu utakaosaidia kupunguza mwingiliano wa binadamu na mifugo ili kujiepusha na magonjwa ya mlipuko,” amesema Kuokota.

Diwani wa kata ya Nahukahua, Nguachi Hamza, akitoa malalamiko kwenye baraza la madiwani kufuatia kuingiza mifugo katika kata yake bila utaratibu maalum

Naye Diwani wa Nahukahuka, Nguachi Hamza ameeleza malalamiko yake kuhusu ongezeko la mifugo katika eneo lake, akisema hali hiyo inasababisha usumbufu kwa wananchi na kuongeza uwezekano wa kutokea kwa migogoro kati ya wakulima na wafugaji.

Amesema wakulima wanahitaji maeneo ya kutosha kwa ajili ya shughuli za kilimo, huku wafugaji wakihitaji maeneo ya malisho na maji kwa ajili ya mifugo yao.

Ameeleza kuwa kukosekana kwa mipango mizuri ya matumizi ya ardhi kunaweza kuongeza malalamiko na kuvuruga mahusiano kati ya makundi hayo mawili yanayotegemea ardhi kwa shughuli zao za kiuchumi.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Lindi, Udhaifa Rashidi amesema Serikali imeweka mikakati ya kukabiliana na mifugo inayoingizwa kiholela katika maeneo mbalimbali, akibainisha kuwa suala hilo linahitaji usimamizi na ufuatiliaji wa karibu kutoka kwa viongozi wa ngazi za vijiji na vitongoji.

Katibu Tawala Wilaya ya Limdi, Udhaifa Rashidi, akizungumza na madiwani baada ya kujitokeza kwa malalamiko ya kuingiza mifugo kwenye maeneo yao

Rashidi amewatahadharisha wenyeviti wa vijiji na viongozi wengine wa maeneo hayo dhidi ya kupokea fedha kutoka kwa wafugaji kwa namna inayoweza kuwawezesha kuendelea kukaa katika maeneo ambayo hawajaruhusiwa kisheria.

Amesema Serikali ina taarifa kuhusu malalamiko ya baadhi ya viongozi kudaiwa kupokea fedha kutoka kwa wafugaji na zinafanyiwa kazi ili kubaini ukweli na kuchukua hatua stahiki kwa watakaobainika kuhusika.

Ameonya kuwa viongozi wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa badala ya kufanya maamuzi kwa masilahi binafsi.

“Niwaombe viongozi kushirikiana na mamlaka zinazohusika katika kuhakikisha mifugo inayoingia katika maeneo yenu inafuata taratibu zinazotakiwa,” amesema Rashidi.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *