Maswa. Mgogoro kati ya wachungaji wa Kikristo na viongozi wa kimila katika kijiji cha Sangamwalugesha, Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, umeingia katika hatua mpya baada ya wachungaji hao kutangaza maazimio ya kukataa kuongozwa na mamlaka za kimila katika shughuli za kijamii, hususan misiba.
Wachungaji hao wameitaka serikali ya wilaya hiyo kuingilia kati mgogoro huo, wanaodai umedumu kwa zaidi ya miaka mitano bila kupata ufumbuzi wa kudumu, wakionya kuwa kuendelea kwake kunaweza kuhatarisha amani na utulivu katika eneo hilo.
Akizungumza Oktoba 20, 2026 kwa niaba ya Umoja wa Wachungaji, Mchungaji Daudi Pagi wa Kanisa la PAGT Sangamwalugesha, amesema uamuzi huo ulifikiwa katika mkutano wao uliofanyika Oktoba 18, 2026 na kutangazwa katika mkutano wa hadhara uliohusisha wananchi na waumini wa madhehebu mbalimbali ya Kikristo.
Amesema wamechukua hatua hiyo kutokana na kile alichodai kuwa ni kulazimishwa kufuata taratibu za kimila za kabila la Wasukuma katika shughuli za kijamii, licha ya wao kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia imani na taratibu za dini zao.
Kwa mujibu wa Pagi, baadhi ya taratibu wanazopinga ni pamoja na shughuli za kuchimba makaburi, kunawisha mikono waombolezaji kabla ya kula chakula na kutenga chakula wakati wa misiba, kuwa za lazima kwa watu wanaoshiriki matukio ya misiba, wakiwamo wao wachungaji.
Amedai kuwa kutotekeleza taratibu hizo kumesababisha baadhi ya wachungaji kutengwa na wazee wa kimila, huku wengine wakidaiwa kufukuzwa wanapohudhuria misiba.
Pagi ameongeza kuwa wachungaji hao wanadaiwa kutakiwa kutoa kondoo mmoja mmoja ili watambuliwe na kuruhusiwa kushiriki shughuli za kijamii ambazo zinazosimamiwa na wazee wa kimila.
Mchungaji wa kanisa la PAGT, Daudi Pagi, akitoa maazimio ya kikao cha wachungaji wa dini ya kikristo juu ya kupinga vitendo vya wazee wa kimila katika kijiji cha Sangamwalugesha. Picha na Samwel Mwanga
“Tumekuwa tukifanya shughuli zetu kwa kufuata taratibu za dini zetu, lakini tunakabiliwa na masharti ya kimila ambayo tunaona yanatunyima uhuru wa kutekeleza majukumu yetu ya kiroho na kushiriki shughuli za kijamii,” amesema.
Amesema mgogoro huo uliwahi kufikishwa katika Mahakama ya Mwanzo ya Sangaitinje, wilayani Meatu, ambako juhudi za usuluhishi zilifanyika na wachungaji kuelekezwa kuendelea na majukumu yao huku wakiheshimiwa katika jamii.
Hata hivyo, amesema hali hiyo haikudumu licha ya suala hilo kufikishwa kwa viongozi mbalimbali wa Serikali kuanzia ngazi ya kata na tarafa.
Mzee wa kimila, Jacobo Lufunga amesema kuwa kwa mujibu wa utaratibu huo, mtu anayetaka kushiriki shughuli hizo kama mzee anatakiwa awe amefikia umri unaotambuliwa kuwa wa uzee.
Hata hivyo, mtu ambaye bado hajafikia umri huo lakini anataka kutambuliwa kama mzee anatakiwa kutoa kondoo mmoja.
“Utaratibu huo unahusu pia viongozi wa dini nao wanapaswa kufuata masharti yaliyowekwa ikiwa wanataka kutambuliwa katika kundi hilo la wazee ili wasishiriki katika majukumu hayo wanayoyakataa, maana wazee hizo shughuli sisi hatufanyi, tulizifanya tukiwa vijana,” amesema.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Sangamwalugesha, Modesta Ndelu amekiri kuwepo kwa mgogoro huo kwa muda mrefu, akisema changamoto imekuwa ni utaratibu unaotumiwa na wazee wa kimila kutambua watu wanaoshiriki katika shughuli zao.
Amesema kwa mujibu wa utaratibu huo, mtu anayetaka kushiriki shughuli hizo kama mzee anatakiwa awe amefikia umri unaotambuliwa kuwa wa uzee au la kutoa kondoo mmoja.
“Utaratibu huo kwa viongozi wa dini ambao ni wachungaji na wainjilisti umeleta mgogoro mkubwa na sisi kama Serikali tunajitahidi kuhakikisha hali hii isisababishe kuharibika kwa amani na mshikamano katika eneo letu hili,” amesema mtendaji huyo.
Katika mkutano wao, wachungaji hao wamepitisha maazimio saba, likiwamo kukataa kuongozwa na wazee wa kimila katika utekelezaji wa majukumu yao ya kidini na kutaka masuala ya utawala yaendeshwe kwa kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria za nchi.
Pia, wamepinga kutozwa kondoo kama sharti la kushiriki shughuli za kijamii na kutaka viongozi wa Kikristo wasilazimishwe kutekeleza majukumu ya kimila kama kuchimba makaburi, kunawisha waombolezaji na kutenga chakula msibani.
Maazimio mengine ni kuitaka serikali ya wilaya, hususan kamati ya ulinzi na usalama, kuingilia kati mgogoro huo, huku wakitaka wazee wa kimila kuacha utaratibu wa kuwatenga wachungaji na wainjilisti katika shughuli za kijamii.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wachungaji wa Kikristo Sangamwalugesha, Marco Malushu amesema Serikali inapaswa kulichukulia suala hilo kwa uzito na kutafuta suluhu kabla hali haijafikia pabaya.
Amesema tayari wameandika barua kwa ofisa mtendaji wa kata hiyo na kusambaza nakala katika maeneo mbalimbali ili mamlaka husika zipate taarifa kuhusu msimamo wao.
Madeleke John, mkazi wa kijiji hicho, amesema kuwa mila zinaweza kuwa na nafasi katika kuunganisha jamii na kuendesha shughuli za kijamii, lakini taratibu zake zinapaswa kueleweka na kukubaliwa na wahusika.
Mkazi mwingine wa eneo hilo, Francis Daniel amesema viongozi wa dini wanapaswa kuwa na nafasi ya kutekeleza majukumu yao ya kiimani na kushiriki misiba bila kulazimishwa kutekeleza taratibu zinazokinzana na imani zao.
Kwa upande wake, Rosemary Joseph amesema serikali, viongozi wa dini na wazee wa kimila wanatakiwa kukaa pamoja ili kuweka utaratibu unaoheshimu mila, imani za dini na haki za wananchi, badala ya kuruhusu tofauti hizo kuendelea kugawa jamii.
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Maswa, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Anna Gidarya amesema kwa hatua mgogoro huo ulipofikia, atakutana na pande husika kupata suluhisho ili shughuli za kijamii ziendelee kama kawaida.
“Suluhu ya kudumu inahitaji katika suala hilo, hivyo nitakutana na pande zote hizi mbili hivi karibuni kwa lengo la kuhakikisha kuwa tunakubaliana na utaratibu unaoweza kulinda mila za jamii bila kuathiri uhuru wa dini na mshikamano wa wananchi,” amesema.


