Mama alivyokataa mila, uchawi kupambania afya ya mwanawe
9 mins read

Mama alivyokataa mila, uchawi kupambania afya ya mwanawe

Winfrida Wambura hakuwahi kufikiria kuwa safari ya kumpeleka binti yake hospitalini kwa dalili za kupumua kwa shida ingemfikisha katika hospitali maalumu ya moyo, mamia ya kilomita kutoka nyumbani kwake Rorya, Mkoa wa Mara.

Alianza kuwa na wasiwasi alipomwona Catherine, aliyekuwa na miezi mitano, akipumua kwa kasi, kutokwa na jasho hata wakati wa baridi na kuchoka haraka anaponyonya.

Lakini wakati akitafuta majibu ya hali ya mtoto wake, baadhi ya watu katika jamii walimweleza kuwa huenda ugonjwa huo ulihusishwa na uchawi au mila za kumpa mtoto jina, wakimshauri kumpeleka kwa waganga wa jadi.

Winfrida, fundi cherehani na mama wa watoto wanne, hakukata tamaa. Aliendelea kutafuta matibabu hospitalini, uamuzi ambao hatimaye ulimwezesha binti yake kufanyiwa upasuaji wa moyo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma.

“Nimemzaa binti yangu Machi 2025, lakini miezi mitano baadaye nilianza kuogopa nilipomwona mtoto wangu akipata shida ya kupumua na kuchoka wakati wa kunyonya,” anasema.

Alimpeleka Catherine katika zahanati ya eneo lao, ambako mhudumu wa afya alishauriana na madaktari wengine kabla ya kumpeleka kwa daktari aliyekuwa akitembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mwalimu Nyerere Memorial.

Baada ya madaktari wapatao watano kumfanyia uchunguzi, walibaini kuwa Catherine alihitaji huduma maalumu za moyo ambazo hazikupatikana katika hospitali hiyo.

Alipewa rufaa kwenda Kituo cha Tiba cha Bugando, Mwanza, ambako alifika Septemba 2025.

Huko, madaktari waligundua kuwa alikuwa na tundu moyoni na kumpa dawa za kutumia kila siku, huku akitakiwa kwenda kliniki kila mwezi.

“Nilihuzunika sana nilipoambiwa kuwa binti yangu ana tundu moyoni. Ukiwa mama, unakuwa na wasiwasi kama mtoto wako ataishi na maisha yake ya baadaye yatakuwaje. Lakini nilipoona watoto wengine wakipata matibabu Bugando, nilipata matumaini kuwa Catherine naye angeweza kusaidiwa,” anasema.

Winfrida anasema imani yake ilimsaidia kukabiliana na hali ya kutokuwa na uhakika, huku uzoefu wa familia nyingine zilizokuwa hospitalini, ukimpa nguvu ya kuendelea kutafuta matibabu.

Aprili 2026, alipata taarifa kuwa timu ya madaktari kutoka Italia ingefanya upasuaji wa moyo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma.

Hata hivyo, hakuwa na bima ya afya, hivyo ilimbidi kutafuta fedha za safari na matibabu. Aliwaomba ndugu na jamaa wamchangie, huku baba wa Catherine, ambaye haishi na familia hiyo, akichangia kiasi kikubwa cha gharama za matibabu.

Hatimaye familia ilisafiri kwenda Dodoma, ambako Catherine alifanyiwa upasuaji wa moyo Mei 27, 2026.

“Kwangu, kupata nafasi ya kufanyiwa upasuaji ilikuwa faraja kubwa. Nilikuwa nimetumia miezi mingi kuwa na wasiwasi kuhusu binti yangu, hivyo nilishukuru kwamba hatimaye angeweza kupata matibabu aliyohitaji,” anasema.

Baada ya upasuaji, madaktari walimweleza kuwa sehemu ndogo ya tundu hilo ilikuwa bado wazi, lakini ilitarajiwa kufunga taratibu kadiri Catherine alivyokuwa akikua na kuendelea kutumia dawa.

Winfrida alirudi na binti yake hospitalini kwa uchunguzi wa ufuatiliaji Julai na Agosti. Hata hivyo, safari ya matibabu haikuishia hapo.

Dalili kwa watoto zinazoweza kupuuzwa

Daktari na mshauri wa masuala ya afya katika taasisi ya One New Heart Tanzania, Dk Lioba Joseph, anafafanua ugonjwa wa moyo wa kuzaliwa nao, kuwa ni hitilafu ya kimuundo katika moyo au mishipa mikubwa ya damu ambayo huwepo tangu mtoto anapozaliwa.

“Ugonjwa wa moyo wa kuzaliwa nao unaweza kuathiri kuta zinazotenganisha vyumba vya moyo, valvu za moyo au mishipa mikubwa ambayo damu hupitia,” anasema.

Takwimu za kimataifa zinaonyesha kuwa takribani watoto wanane kati ya kila watoto 1,000 wanaozaliwa hai huwa na ugonjwa wa moyo wa kuzaliwa nao.

Hata hivyo, ukubwa wa tatizo barani Afrika huenda ukawa mkubwa kuliko unavyokadiriwa kutokana na watoto wengi kukosa huduma za uchunguzi wa mapema wa echocardiographia (vipimo vya moyo kwa kutumia mawimbi ya sauti).

Utafiti wa miaka sita uliofanywa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ulibaini kuwa magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo yalichangia asilimia 80 ya wagonjwa wa moyo miongoni mwa watoto waliofanyiwa uchunguzi katika kituo hicho cha rufaa cha kitaifa.

Utafiti huo uliochapishwa mwaka 2024 katika jarida la Global Heart, uliangalia watoto 6,058 waliofanyiwa uchunguzi wao wa kwanza wa echocardiographia kati ya mwaka 2017 na 2022.

Kati yao, watoto 3,198 waligundulika kuwa na magonjwa ya moyo, wakiwamo 2,559 waliokuwa na magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo.

Matokeo hayo yanaonyesha ukubwa wa tatizo miongoni mwa watoto waliofanyiwa uchunguzi katika kituo hicho maalumu cha rufaa, na hayapaswi kutafsiriwa kuwa ndiyo kiwango cha ugonjwa wa moyo wa kuzaliwa nao kwa watoto wote nchini Tanzania.

Dk Joseph anasema wazazi na wahudumu wa afya wanapaswa kuzingatia dalili zinazoendelea kwa muda mrefu ambazo zinaweza kuashiria kasoro ya moyo.

“Kwa mtoto mchanga, dalili muhimu za hatari ni pamoja na kupumua kwa kasi au kwa shida, kushindwa kunyonya au kula vizuri, kuchoka na kutokwa na jasho wakati wa kunyonya, kutoongezeka uzito vizuri, kupata maambukizi ya kifua mara kwa mara na midomo, ulimi au ngozi kuwa na rangi ya samawati au kijivu,” anasema.

Anasema baadhi ya watoto wanaweza kuonekana wenye afya licha ya kuwa na tatizo la kimuundo katika moyo. Wakati mwingine dalili kama kupumua kwa kasi na kushindwa kunyonya vizuri,  zinaweza kudhaniwa mwanzoni kuwa ni magonjwa mengine ya utotoni.

“Ujumbe muhimu kwa wazazi ni kwamba mtoto si lazima aonekane mgonjwa sana ili awe na ugonjwa wa moyo wa kuzaliwa nao. Uchunguzi wa mapema unaweza kubaini matatizo kabla ya madhara kutokea,” anasema.

Dk Joseph anaonya kuwa kasoro kubwa za moyo zinaweza kusababisha moyo kushindwa kufanya kazi vizuri, shinikizo la damu kwenye mishipa ya mapafu, upungufu wa oksijeni mwilini na utapiamlo iwapo utambuzi na matibabu vitachelewa.

Hata hivyo, anasema kuchelewa kugundua ugonjwa huo hakumaanishi moja kwa moja kuwa matibabu hayatafanikiwa, akiongeza kuwa watoto wengi wanaweza kupata matokeo mazuri wanapopata huduma sahihi.

“Kila mtoto anastahili nafasi ya kukua akiwa na moyo wenye afya. Ugonjwa wa moyo wa kuzaliwa nao unaweza kutibiwa mara nyingi, lakini kadiri tunavyoutambua mapema, kuugundua na kumunganisha mtoto na huduma zinazofaa, ndivyo nafasi ya kuzuia madhara na kuokoa maisha inavyoongezeka,” anasema.

Kwa Winfrida, kupata nafasi ya upasuaji ilikuwa mafanikio makubwa, lakini kuhakikisha Catherine anaendelea kupona kumekuwa na changamoto.

Anasema biashara yake imekuwa mbaya, hali inayomfanya ashindwe kumudu gharama za kusafiri kwa ajili ya uchunguzi wa ufuatiliaji na kununua dawa.

Kutokana na hali hiyo, alikosa kumpeleka Catherine katika miadi ya uchunguzi iliyopangwa Septemba. Anaeleza kuwa dawa za mtoto huyo ziliisha karibu mwezi mmoja uliopita, na tangu wakati huo, Catherine amekuwa akilia, akipata homa na kuonyesha dalili za maumivu katika eneo la kidonda cha upasuaji.

“Niliweza kumfikisha binti yangu kwenye upasuaji, lakini sasa ninahangaika kutafuta fedha za dawa na miadi ya uchunguzi. Nataka aendelee kupata matibabu, lakini fedha hazipatikani kila wakati tunapozihitaji,” anasema.

Dalili hizo zinahitaji mtoto huyo kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu haraka, huku chanzo chake kikiwa bado hakijabainishwa.

Mwanzilishi mwenza na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uendeshaji wa One New Heart Tanzania, Godfrey Maro, anasema changamoto zinazokabili familia mara nyingi hazikomei katika kupata utambuzi wa ugonjwa au kufanikisha upasuaji.

“Tatizo si utambuzi pekee, bali pia kinachotokea baada ya mtoto kugundulika kuwa na ugonjwa,” anasema.

Anaeleza kuwa familia zinaweza kushindwa kupata matibabu, kutokana na upungufu wa wahudumu wa afya wenye ujuzi, vifaa vya uchunguzi na huduma maalumu, pamoja na gharama za kusafiri kwenda hospitali za rufaa.

“Huduma za moyo zinapopatikana katika vituo vichache tu, familia kutoka mikoa mingine hulazimika kusafiri mamia ya kilomita ili kupata utambuzi au kumuona daktari bingwa. Hii inamaanisha gharama zaidi za usafiri, muda mwingi wa kukaa mbali na kazi na ugumu wa kurudi kwa ajili ya matibabu na uchunguzi wa ufuatiliaji,” anasema Maro.

Anaongeza kuwa Tanzania inahitaji kuimarisha uchunguzi katika vituo vya afya vya msingi na hospitali za mikoa, kuboresha mifumo ya rufaa, kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya na kupanua upatikanaji wa huduma maalumu za moyo.

“Tunapaswa kupunguza mzigo wa kifedha kwa familia. Gharama za usafiri, malazi, vipimo na matibabu zinaweza kuwazuia watoto kupata huduma kwa wakati,” anasema.

Maro anatoa wito wa kuwepo kwa takwimu za kitaifa zinazoaminika zinazoonyesha idadi ya watoto wanaozaliwa na kasoro za moyo, wanaogundulika na kutibiwa, pamoja na wale wanaoshindwa kupata huduma.

Anasema bila rejista kamili ya kitaifa, haiwezekani kutoa idadi sahihi ya watoto wanaosubiri matibabu.

Licha ya changamoto hizo, Winfrida anataka wazazi wengine wafahamu kuwa kutafuta huduma za kitabibu kunaweza kuleta mabadiliko mtoto anapokuwa na dalili zinazotia wasiwasi.

“Wazazi hawapaswi kukata tamaa au kuruhusu hofu na simulizi za uchawi kuwazuia kutafuta matibabu. Mtoto anapokuwa mgonjwa, mpelekeni hospitalini na waacheni wataalamu wa afya wamfanyie uchunguzi. Ingawa imani inaweza kuwapa nguvu, ni lazima pia kutafuta matibabu sahihi,” anasema.

Uzoefu wake unakumbusha kuwa kushinda shinikizo la jamii na kupata nafasi ya upasuaji kunaweza kubadilisha safari ya matibabu ya mtoto, lakini kupona kunaweza kuhitaji msaada endelevu hata baada ya upasuaji.

Kwa Catherine, hatua inayofuata ni kurejea hospitalini na kufanyiwa uchunguzi wa dalili anazoonyesha sasa. Kwa mama yake, azma iliyowapeleka kutoka Rorya hadi kupata matibabu maalumu Dodoma, bado ni muhimu katika jitihada zake za kuhakikisha binti yake anaendelea kupata nafuu.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *