Simulizi ya mtoto aliyetoa maoni mabadiliko Katiba, sasa mfanyabiashara
Dar es Salaam. Akiwa na miaka 14, Nathan Kimaro alitembea kilomita saba kwa miguu kutoka nyumbani hadi eneo la mkutano wa kupokea maoni kuhusu mabadiliko ya Katiba mwaka 2014. Alikuwa na mapendekezo 15 aliyotaka kuyawasilisha mbele ya Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Tukio lake, lilizua gumzo katika vyombo vya habari. Gazeti la Mwananchi, lilichapisha habari yake, likionesha maajabu ya mtoto wa miaka 14 aliyetoa maoni katika jukwaa ambalo watu wenye umri wa zaidi ya miaka 18 pekee ndio waliruhusiwa.
Miaka 13 baadaye, Kimaro ambaye sasa ana umri wa miaka 27, amekutana tena na Mwananchi, safari hii akiwa mfanyabiashara anayejihusisha na biashara na uwekezaji katika sekta mbalimbali, akitazama upya safari yake.
Katika mahojiano yake na Mwananchi, anasimulia namna alivyopata ujasiri wa kusimama mbele ya tume, changamoto alizopitia tangu utotoni na hatua zilizomfikisha katika shughuli za biashara anazofanya sasa.
Kimaro, anasema wakati huo alisikia matangazo ya gari yaliyokuwa yakitangaza uwepo wa mkutano wa kupokea mapendekezo kuhusu Katiba mpya. Bila kusita, aliamua kwenda kushiriki kwa sababu aliamini alikuwa na jambo la kuiambia nchi yake.
“Nilikuwa mtoto wa miaka 14, lakini nilikuwa na jambo la kuiambia Taifa langu. Nilikuwa natazama mbele sana, kwa sababu niliona maoni nitakayotoa labda yatanisaidia vizuri kuja kuishi wakati huu,” anasema.
Anakumbuka alivyotembea umbali wa kilomita saba hadi eneo la mkutano, alikokuta umati mkubwa wa watu wenye mitazamo tofauti kuhusu mabadiliko ya Katiba, huku ulinzi ukiwa mkali.
Anasema watu walikuwa na sababu tofauti za kuhudhuria mkutano huo, wengine walitaka kusikiliza, wengine kutoa maoni, huku mjadala wa muundo wa Muungano wa Serikali tatu ukiwa miongoni mwa hoja zilizotawala.
Alipofika eneo hilo, anasema wananchi walipanga foleni, wakisubiri zamu zao za kuwasilisha maoni mbele ya kamati. Alikuwa ameandika mapendekezo saba kwenye karatasi, lakini baadaye akaongeza mengine.
Jumla yake, anasema alikuwa na mapendekezo 15 aliyoyabeba kichwani na moyoni, akiamini kila moja lilikuwa na umuhimu katika kujenga taifa linalowajali watoto na vijana.
Hata hivyo, alipofika mbele ya msimamizi, alikataliwa kuzungumza kwa sababu ya umri wake.
“Akaniambia, wewe mtoto, pisha wakubwa zako. Niliumia sana, nikajiuliza kwa nini nipishe wakati nimekuja kutoa maoni,” anasema.
Baada ya kusubiri, hatimaye alipata nafasi ya kuwasilisha hoja zake. Miongoni mwa mapendekezo yake yalikuwa kuanzishwa kwa wizara maalumu ya watoto na vijana ili Serikali ishughulikie mahitaji ya makundi hayo kwa karibu zaidi.
Wakati huo, masuala hayo yalikuwa chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto. Kimaro aliamini kuanzishwa kwa wizara maalumu kungeongeza umakini katika kushughulikia changamoto za watoto na vijana.
Pendekezo lake la pili lilihusu kupunguza umri wa kugombea urais kutoka miaka 40 hadi 35.
Anasema wakati huo alifikiria kwamba angefikia umri huo na kupata nafasi ya kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Nikasema nitafanya shughuli zangu, nisome kwa bidii, halafu nitakapofikisha miaka 35 nitagombea urais na kufanya mabadiliko,” anasema akikumbuka namna wananchi walivyolipokea pendekezo hilo kwa shangwe na vicheko.
Pia, alipendekeza kuanzishwa kwa chama cha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, kitakachowawezesha watoto kuchagua viongozi na kuwa na jukwaa la kuzungumzia changamoto zinazowakabili katika mazingira ya shule.
Anasema alichochewa na malalamiko kuhusu vitendo vya ukatili vinavyodaiwa kufanywa na baadhi ya walimu dhidi ya wanafunzi, pamoja na masuala ya usahihishaji wa mitihani yaliyokuwa yakiibua maswali.
“Nilijiuliza nani atazungumza kwa niaba yetu. Kuna chama cha walimu, chama cha wafanyakazi na vyama vingine. Nikasema na sisi tuwe na chama chetu kitakachotoa sauti kwa niaba ya watoto,” anasema.
Pendekezo jingine lilihusu maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika. Alitaka Rais wa Jamhuri ya Muungano ahudhurie maadhimisho hayo ili kusikiliza changamoto za watoto na kuona namna zinavyoweza kushughulikiwa.
Anasema hakuridhishwa na hali ya maadhimisho mengi kuishia kwenye hotuba na picha, huku baadhi ya changamoto za watoto zikiendelea. Alitaka mijadala hiyo iambatane na hatua za kisheria na kiutendaji.
Pia, aligusia sheria ya ndoa iliyokuwa ikiruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa na miaka 15 katika mazingira fulani, akiona kuna mkanganyiko kati ya utambuzi wa mtoto kisheria na ulinzi anaopaswa kupata.
Safari yake ya kuwasilisha maoni hayo, anasema, ilijengwa na mazingira aliyokulia. Kimaro anasema alizaliwa katika familia yenye maisha ya kawaida, akiwa mtoto wa pili katika familia ya watoto wawili, akilelewa na mama yake.
Mama yake, anasema, alikuwa mtumishi kabla ya kujishughulisha na biashara. Kimaro alianza kujitegemea akiwa kidato cha kwanza, baada ya kumaliza darasa la saba na kuondoka nyumbani.
Katika kipindi hicho, anasema alifanya biashara mbalimbali ikiwamo kuuza samaki na miwa, pamoja na kufanya usafi kwenye nyumba za watu. Akiwa amemaliza darasa la saba, alifungua duka la bidhaa mbalimbali.
Anasema pia alinunua kiwanja chake cha kwanza akiwa kidato cha pili, jambo linaloonesha namna alivyokuwa na shauku ya kujenga maisha tangu akiwa mdogo.
“Nilijifunza kwamba hakuna mtu atakayeishi maisha yangu kwa niaba yangu; si Serikali, mzazi, ndugu wala ukoo. Nilizikabili changamoto hizo kwa sababu niliona ni sehemu ya maisha,” anasema.
Kimaro, anasema changamoto hizo zilimfundisha unyenyekevu na kumjenga katika mtazamo wa kutafuta mafanikio kupitia juhudi, badala ya kutumia mali na mwonekano kuonyesha uwezo wake kwa watu wengine.
Anapozungumzia maisha yake ya sasa, anasema amejikita katika biashara. Anahusika na kampuni ya Access Store iliyopo Arusha, Orient Energies na shughuli za ujenzi, huku pia akiwa na hisa katika kampuni nyingine.
Anasema anaangalia fursa za uwekezaji katika sekta ya mafuta, majengo na maeneo mengine ya uchumi. Anaeleza kuwa biashara kwake si njia ya kujipatia kipato pekee, bali pia nafasi ya kuchangia maendeleo ya Taifa.
Kupitia shughuli zake, anasema anashiriki katika kutoa ajira, kulipa kodi na kusaidia jamii, akiamini mafanikio ya mtu yanapaswa kuwa na matokeo yanayovuka maisha yake binafsi.
“Siwezi kuwa huru kifedha kama walioko karibu yangu au jamii yangu hawajapata uhuru wa kifedha,” anasema, akieleza falsafa yake ya kushirikisha jamii katika matokeo ya mafanikio anayoyapata.
Kwa mtazamo wake, mtu anaweza kulichangia Taifa bila kuwa na cheo cha kisiasa au kushika nafasi ya uongozi serikalini. Anasema uraia mwema na uwajibikaji vina nafasi kubwa katika maendeleo ya nchi.
Anataja mchango wa wafanyabiashara na watu binafsi katika kujenga uchumi, kutoa ajira na kusaidia jamii, akisema raia anaweza kuandika historia kupitia shughuli zake za kila siku.
Akikumbuka kijana aliyesimama mbele ya kamati miaka 13 iliyopita, Kimaro anasema anamshukuru kwa kutokata tamaa, kuwa na ujasiri na kutumia nafasi aliyopata kueleza matarajio yake kwa taifa.
“Namshukuru kwa kutumia maisha aliyokuwa nayo wakati ule kuchangia taifa lake. Nilikuwa mtoto kama watoto wengine, lakini nilikuwa nimebeba mzigo wa kutamani nchi yangu iwe mahali pazuri pa kuishi,” anasema.
Kwa sasa, anasema anaendelea na shughuli zake za biashara huku akiamini kuwa mchango wa mtu kwa taifa hauhitaji lazima nafasi ya kisiasa, bali dhamira, uwajibikaji na utayari wa kutumia fursa alizonazo.
