Wanaume kliniki chachu wajawazito kuanza huduma mapema
3 mins read

Wanaume kliniki chachu wajawazito kuanza huduma mapema

Dar es Salaam. Ushiriki wa wanaume katika kliniki za wajawazito, unaweza kusaidia wanawake kuanza huduma za afya mapema, lakini hauonekani kuwa na mchango wa moja kwa moja katika matumizi ya huduma zote za afya ya uzazi na mtoto.

Hayo yamebainishwa na utafiti uliofanyika katika kituo cha huduma za afya ya msingi jijini Dar es Salaam, uliochunguza uhusiano kati ya ushiriki wa wanaume kliniki za wajawazito na matumizi ya huduma muhimu za afya ya uzazi na mtoto.

Utafiti huo uitwao: ‘Male Involvement in Antenatal Care, Women’s Reproductive and Child Health Service Utilisation, and Its Associated Factors: An Analytical Cross-Sectional Study in Dar es Salaam, Tanzania na kuchapishwa katika jarida la East Africa Health Research Journal (2026)’, ulihusisha wanawake 396 waliokuwa wamejifungua kati ya miezi mitatu na 18 iliyopita, na waliokuwa wakihudhuria kliniki za watoto chini ya miaka mitano au huduma za uzazi wa mpango.

Matokeo yanaonyesha kuwa wanawake walioandamana na wenza wao kliniki ya wajawazito, walikuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kuanza huduma hizo mapema ikilinganishwa na wale ambao hawakuandamana na wenza wao.

Kwa mujibu wa utafiti huo, wanawake walioshiriki kliniki ya wajawazito pamoja na wenza wao walikuwa na kiwango cha kuanza huduma mapema kilichokuwa juu kwa asilimia 36.

Hata hivyo, utafiti haukubaini uhusiano wenye umuhimu wa kitakwimu kati ya ushiriki wa wanaume kliniki za wajawazito na wanawake kuhudhuria huduma za baada ya kujifungua ndani ya siku saba au kutumia njia za kisasa za uzazi wa mpango.

Wanaume wengi walishiriki kliniki

Katika wanawake 396 walioshiriki utafiti, zaidi ya nusu, sawa na asilimia 54.3, walikuwa na umri wa miaka 25 hadi 34.

Utafiti ulibaini kuwa wanawake 265, sawa na asilimia 67, walikuwa wameandamana na wenza wao angalau mara moja wakati wa kliniki ya wajawazito.

Aidha, wanawake 245, sawa na asilimia 62, walisema wenza wao walihudhuria kliniki katika ziara yao ya kwanza.

Matokeo hayo yanaonyesha kuwa ushiriki wa wanaume katika kliniki za wajawazito, ulikuwa wa kiwango cha wastani katika eneo lililofanyiwa utafiti.

Watafiti walieleza kuwa uwepo wa mwenza unaweza kuwa na mchango katika kumsaidia mwanamke kutafuta huduma za afya mapema wakati wa ujauzito.

Hata hivyo, ushiriki huo haukuhusishwa na matumizi ya huduma nyingine zote zilizochunguzwa, jambo linaloonyesha kuwa kuandamana na mwanamke kliniki pekee, hakutoshi kuhakikisha anapata huduma zote muhimu za afya ya uzazi na mtoto.

Kwa mujibu wa utafiti huo, wanawake walioandamana na wenza wao kliniki walikuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kuanza huduma za kliniki za wajawazito mapema.

Hata hivyo, hakuna uhusiano wenye umuhimu wa kitakwimu uliobainika kati ya ushiriki wa wanaume na kuhudhuria huduma za baada ya kujifungua ndani ya siku saba au matumizi ya njia za kisasa za uzazi wa mpango.

Matokeo hayo yanaashiria umuhimu wa kuimarisha ushiriki wa wanaume katika huduma za afya ya uzazi, huku kukiwa na mikakati mingine inayohakikisha wanawake wanapata huduma kwa wakati na kuendelea kuzitumia baada ya kujifungua.

Utafiti huo pia unaonyesha umuhimu wa kuangalia mahitaji ya wanawake kwa upana, badala ya kutegemea uwepo wa wenza wao kama kipimo pekee cha mafanikio ya huduma za afya ya uzazi.

Kwa kuwa utafiti ulifanyika katika kituo kimoja cha huduma za afya ya msingi jijini Dar es Salaam, matokeo yake yanapaswa kutafsiriwa kwa kuzingatia mazingira hayo. Hivyo, hayawezi kuchukuliwa kuwa yanawakilisha moja kwa moja hali ya wanawake wote nchini Tanzania.

Watafiti wamependekeza kuwa juhudi za kuhamasisha ushiriki wa wanaume ziambatane na mikakati mipana zaidi ya kuboresha upatikanaji na matumizi ya huduma za afya ya uzazi na mtoto, ili wanawake na watoto wapate huduma zinazohitajika katika hatua zote muhimu.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *