Hospitali ya Mount Meru yaanzisha huduma za saratani
3 mins read

Hospitali ya Mount Meru yaanzisha huduma za saratani

Arusha. Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru imeanzisha huduma za uchunguzi na matibabu ya saratani, ikiwemo tiba kemikali (chemotherapy) hatua inayolenga kupunguza safari za wagonjwa wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini kwenda Hospitali ya Taifa kutafuta huduma hizo.

Hayo yamebainishwa leo Oktoba 30, 2026 na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mount Meru, Dk Alex Ernest wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maboresho yaliyofanyika katika hospitali hiyo, kuelekea maadhimisho ya miaka 100 tangu ianze kutoa huduma mwaka 1926.

Amesema kuanzishwa kwa kitengo cha patholojia kumeimarisha uwezo wa hospitali kubaini saratani mapema kupitia uchunguzi wa sampuli za wagonjwa, huku huduma za tiba kemikali zikitoa nafasi kwa wagonjwa kuanza matibabu ndani ya mkoa.

“Hii ni fursa kubwa ambayo mbali na wagonjwa kuokoa gharama za kutafuta tiba, lakini ugunduzi wa mapema na ukaribu wa huduma unampa uhakika wa kupona kabisa kwa gharama ndogo isiyohitaji safari ndefu,” amesema.

Dk Ernest amesema kuanzishwa kwa huduma hizo ni sehemu ya mabadiliko ya hospitali hiyo, ambayo yamehusisha uwekezaji katika miundombinu, vifaa tiba na kuongeza watumishi.

Amesema tangu mwaka 2020, Serikali imetoa zaidi ya Sh5 bilioni kwa ajili ya maboresho mbalimbali ya hospitali hiyo, yakiwemo upanuzi wa miundombinu na ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa.

Mganga mfawidhi wa hospital ya rufaa ya Mkoa Mount Meru, Dk Alex Ernest, akizungumza na waandishi wa habari.

“Maboresho mengine ni kuimarishwa kwa huduma za dharura, uchunguzi wa kisasa, huduma za endoscopy pamoja na kuwekwa kwa mtambo wa kuzalisha oksijeni uliogharimu zaidi ya Sh1.752 bilioni,” amesema.

Amesema mtambo huo umeimarisha upatikanaji wa oksijeni, hasa kwa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati ambao mara nyingi hukabiliwa na changamoto za upumuaji kutokana na mapafu kutokuwa yamekomaa.

Hospitali hiyo, pia, imekuwa ikiendesha kambi za huduma za afya katika maeneo ya mbali ili kusogeza huduma kwa wananchi ambao wanakabiliwa na changamoto ya kufika hospitalini.

Katika hatua nyingine, hospitali imeanzisha kituo cha mawasiliano kinachofanya kazi wakati wote, kikiwawezesha wananchi kupata taarifa na msaada kuhusu huduma za matibabu kwa kupiga simu bila malipo.

Dk Ernest amesema hospitali hiyo itaadhimisha miaka 100 kwa shughuli mbalimbali, zikiwemo kambi za uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza, huduma za macho na vipimo na tiba kwa watoto kuanzia Novemba mosi hadi 9, 2026.

“Pia, tutaendesha kampeni ya uchangiaji damu ili kusaidia wananchi wanaopata changamoto ya kuongezewa damu, hasa majeruhi wa ajali, wajawazito wanaojifungua na wagonjwa wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza,” amesema.

Amesema kwa sasa hospitali inahitaji kati ya chupa 450 na 550 za damu kila mwezi, hivyo amewahimiza wananchi kujitokeza kuchangia ili kusaidia kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo.

“Kilele cha maadhimisho hayo kinatarajiwa kufanyika Novemba 10, 2026, kikiongozwa na Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa,” amesema.

Neema Laizer, mkazi wa Arusha, amesema watu wengi wamekuwa wakitaabika na ugonjwa wa saratani hasa wanawake, hivyo kuomba Serikali ihakikishe hospitali zote za mikoa zinaanzisha kitengo hicho.

“Kuimarisha huduma za kinga, uchunguzi wa mapema na matibabu za ugonjwa wa saratani ni muhimu ili kupunguza madhara ya ugonjwa huo nchini, hivyo tunaomba Serikali iongeze uwekezaji katika hospitali zingine ili pia kupunguza foleni kwenye hospitali za Taifa,” amesema.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *