ACT yaeleza inavyojipanga kushika dola Zanzibar, Tanzania
Pemba. Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu amesema ujenzi wa majengo ya kisasa ya ofisi za chama hicho kisiwani Pemba ni ishara ya dhamira na hatua madhubuti zinazochukuliwa na chama hicho kujiandaa kushika dola Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Dorothy ameyasema hayo Oktoba 30, 2026, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutembelea miradi ya ujenzi wa ofisi za chama hicho Wete, ikiwemo Ofisi ya Jimbo la Wete iliyopo Jadida, Tawi la Mlindo, Tawi la Pandani katika Jimbo la Pandani, pamoja na jengo la Tawi la Mzambarau Takao katika Jimbo la Mtambwe.
Amesema dhamira ya ACT Wazalendo kushika dola ndiyo inayochochea juhudi za kujenga ofisi bora zitakazowezesha chama kuimarisha shughuli zake na kujiandaa kutekeleza majukumu ya uongozi kwa ufanisi.
“Majengo haya ya kisasa ni kielelezo cha kwamba ACT Wazalendo tuko serious kushika dola. Hatuwezi kusema tunataka kuongoza nchi wakati hata ofisi zetu hazina hadhi. Hii ni ishara ya maandalizi ya kweli,” alisema Doroth.
Aidha, Dorothy aliwataka viongozi na wanachama wa chama hicho kufanya kazi kwa mshikamano na umoja ili kuendelea kukijenga na kukiimarisha chama.
“Mimi najivunia Wete. Nawaombeni sana muendelee kuwa wamoja ili mzidi kuimarisha chama chetu, kwani ndicho tumaini la Watanzania,” amesema.
Ameeleza kuwa Wete ni eneo linalopaswa kuwa mfano katika shughuli za chama, akibainisha kuwa majengo hayo yanaonesha hatua kubwa iliyofikiwa na ACT Wazalendo katika kuimarisha miundombinu yake.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Mkoa wa Wete, Juma Khamis Ali, amemweleza Kiongozi wa Chama kuwa mkoa huo una matawi 120 na kwamba atahakikisha yote yanajengwa kwa viwango vya kisasa ili kuongeza ufanisi katika shughuli za chama.
“Haya uliyoyapitia leo, ifikapo Februari yote yatakuwa yamekamilika. Nakuomba ujiandae kuja tena kwa ajili ya ufunguzi rasmi,” amesema Juma.
Naye, Naibu Katibu wa Oganaizesheni, Mafunzo na Chaguzi wa chama hicho, Khamis Ali Salum amesema majengo ya kisasa ya ofisi za ACT Wazalendo ni kielelezo cha hatua zinazopigwa na chama hicho katika maandalizi yake ya kushika dola Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Dorothy yupo kisiwani Pemba kwa ziara ya kikazi ya siku mbili yenye lengo la kukagua maendeleo ya chama, ikiwemo kufungua mkutano mkuu wa Mkoa wa Wete unaofanyika leo katika ukumbi wa Dolphin uliopo Bopwe mkoani humo.
