Moto wateketeza vyumba 10 vya nyumba Arusha
3 mins read

Moto wateketeza vyumba 10 vya nyumba Arusha

Arusha. Vyumba 10 vya nyumba moja iliyopo Mtaa wa Pangani, Kata ya Kati, jijini Arusha vimeteketea kwa moto uliotokea usiku, huku mali zote zilizokuwamo ndani ya vyumba hivyo zikiungua na kusababisha hasara kwa wakazi.

Tukio hilo lilitokea katika eneo maarufu la Crystal Street, Bondeni ambapo taarifa za awali zilidai kuwa huenda ulisababishwa na hitilafu ya mtungi wa gesi uliokuwa ukitumika kupikia katika moja ya vyumba vya nyumba hiyo.

Akizungumza katika eneo la tukio usiku wa Ijumaa Oktoba 30,2026, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Arusha, Osward Mwenjejele alisema walipokea taarifa ya moto huo saa 2:04 usiku na askari walipofika walikuta umesambaa kwa kiwango kikubwa.

Alisema nyumba hiyo ina zaidi ya vyumba 14, lakini 10 ndivyo vilivyoteketea kabisa, huku juhudi za askari wa zimamoto zikifanikiwa kuzuia usisambae kwenye jengo la ghorofa lenye familia zaidi ya 20, maduka na maghala ya wafanyabiashara yaliyopo jirani.

Mwenjejele alisema uchunguzi wa kubaini chanzo halisi cha moto unaendelea, ingawa hatua za awali zilionyesha uwezekano wa mitungi ya gesi iliyokuwamo ndani ya nyumba hiyo kuwa sehemu ya chanzo cha tukio hilo.

Mwonekano wa mabaki ya nyumba iliyoteketea kwa moto Mtaa wa Pangani, Kata ya Mjini Kati jijini Arusha usiku wa kuamkia leo Jumamosi chanzo cha moto huo ikidaiwa ni mtungi mdogo wa gesi. Picha na Filbert Rweyemamu

Alitaja changamoto kubwa iliyokwamisha juhudi za kuzima moto kuwa ni ukosefu wa njia nzuri ya kufika kwenye nyumba hiyo, baada ya njia iliyokuwa ikitumika kuzuiwa na kuwekwa ngazi ambazo zilifanya magari ya zimamoto kushindwa kupita moja kwa moja.

Alisema hali hiyo iliwalazimu askari kuvuta mabomba ya maji kwa umbali wa takribani mita 100 kupitia eneo la mto ili kufika kwenye sehemu iliyokuwa ikiungua, huku akibainisha kuwa magari mawili ya zimamoto yalitumika katika operesheni hiyo.

Aidha, aliwataka wananchi wanaotumia gesi majumbani kuwa makini kwa kuhakikisha wanasimamia mapishi yao, wanatumia mitungi na vifaa vilivyothibitishwa ubora wake na kuepuka kuacha majiko yakiwaka wakati hawapo nyumbani.

Alifafanua kuwa matumizi ya mitungi midogo isiyokidhi viwango pamoja na vifaa visivyo imara vinavyounganisha mtungi na jiko vinaweza kuongeza hatari ya kuvuja kwa gesi na kusababisha moto au mlipuko.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Kati, Kirenga Swai, alisema tukio hilo ni janga kwa wakazi walioathirika na kuwataka wananchi kujifunza umuhimu wa kuzingatia usalama katika matumizi ya gesi.

Alisema serikali ya mtaa itarejea eneo hilo kushirikiana na wahusika na kuangalia namna ya kuwasaidia waathirika, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia mpangilio wa majengo na kuweka njia za kutosha kwa ajili ya magari ya zimamoto na uokoaji.

Mmoja wa waathirika wa moto huo, Christina Mmasi alisema alikuta chumba chake kikiwa tayari kimeteketea baada ya kurejea kutoka kwenye shughuli zake, huku akieleza kuwa hakuweza kuokoa mali yoyote.

Alisema alikuwa ameondoka nyumbani asubuhi na kuacha fedha kiasi cha Sh500,000 mezani ambazo alikusudia kulipa mkopo, lakini nazo ziliungua pamoja na mali nyingine.

“Mimi sikuwepo nyumbani,niliondoka saa tisa mchana kwenda kwenye utafutaji, majirani na mwenye nyumba walinipigia kuwa nyumba inaungua,wakati nafika naona gari la zimamoto linakuja  huku, nachungulia nikaona nyumba yote imeungua sijaweza kuokoa kitu,”alisema Christina

Mkazi mwingine wa eneo hilo alisema taarifa alizozipata zilionyesha kuwa moto ulianza baada ya mtungi wa gesi kuhusishwa na hitilafu wakati wa kupika, huku baadhi ya majirani wakijaribu kuuzima kwa kutumia maji, hatua ambayo haikufanikiwa kuudhibiti.

Licha ya hasara kubwa iliyotokea, hakuna mtu aliyeripotiwa kujeruhiwa au kupoteza maisha katika tukio hilo.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *