Serikali, WHO waja na mikakati kuikabili Ebola, magonjwa ya mlipuko
4 mins read

Serikali, WHO waja na mikakati kuikabili Ebola, magonjwa ya mlipuko

Mbeya. Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) imekuja na mikakati ya kuwajengea uwezo wataalamu wa afya kutambua mapema viashiria vya magonjwa ya milipuko, kujikinga na kudhibiti maambukizi yanayoweza kuingia nchini.

Hatua hiyo inalenga kuimarisha utayari wa vituo vya kutolea huduma za afya, hususan katika maeneo yenye mwingiliano mkubwa wa watu kutoka ndani na nje ya nchi, ili kuhakikisha wagonjwa wenye viashiria vya magonjwa ya kuambukiza wanabainika mapema na kupata huduma bila kuhatarisha usalama wa wahudumu na wananchi wengine.

Mikakati hiyo imeenda sambamba na kutoa mafunzo ya siku tano kwa wataalamu 35 kutoka vituo sita vya kutolea huduma za afya mkoani Mbeya, vikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na Hospitali ya Rufaa ya Kanda.

Akizungumza na Mwananchi leo Oktoba 31, 2026 wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura kutoka Wizara ya Afya, Dk Michael Kilemeji amesema lengo ni kuimarisha uwezo wa wataalamu wa afya kama sehemu ya maandalizi ya nchi katika kukabiliana na ugonjwa huo.

Amesema wamekusudia kuwajengea wataalamu uwezo wa kutambua na kuhisi viashiria vya magonjwa ya kuambukiza, kuchukua tahadhari zinazostahili na kutumia mbinu sahihi za kujikinga wanapohudumia wagonjwa.

“Tunahakikisha vituo vyetu vya kutolea huduma vinakuwa na uwezo wa kutambua wagonjwa wenye viashiria vya magonjwa ya kuambukiza na kutumia mbinu sahihi za kujikinga na maambukizi,” amesema.

Amesema umuhimu wa maandalizi hayo unatokana pia na nafasi ya vituo vya afya katika kuzuia kusambaa kwa magonjwa, kwa kuwa mgonjwa anaweza kufika kupata huduma bila kutambua kuwa ana ugonjwa wa kuambukiza.

Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na udhibiti katika maeneo ya mipakani, ikiwemo kuweka utaratibu wa kukusanya taarifa za wageni wanaoingia nchini.

Mbeya kitovu cha tahadhari

Akifafanua sababu za kuchagua Mbeya kuwa eneo la mafunzo hayo, Dk Kilemeji amesema mkoa huo una nafasi muhimu kutokana na kuwa lango la mawasiliano na nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ikipakana na Malawi na Zambia.

Amesema mwingiliano wa watu wanaovuka mipaka na wanaotoka maeneo mbalimbali unaifanya Mbeya kuwa miongoni mwa maeneo yanayohitaji kuimarishwa zaidi katika mifumo ya tahadhari na udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza.

“Mkoa wa Mbeya ni lango la SADC na unapokea wageni kutoka mataifa mbalimbali. Hata hivyo, Tanzania ipo salama, lakini hali hiyo haituzuii kuendelea kujiimarisha katika viwanja vya ndege, bandari, mipaka rasmi na isiyo rasmi,” amesema.

Amesema mafunzo hayo yamehusisha washiriki kutoka halmashauri za mkoa huo, kwa utaratibu wa kila halmashauri kupata wataalamu wawili ili watumie maarifa waliyoyapata kuimarisha utayari katika maeneo yao.

Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Nemes Iliya amesema kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, shirika hilo limeweka mikakati ya pamoja ya kuwajengea uwezo wataalamu ili wajikinge na kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza.

Amesema kuenea kwa magonjwa ya milipuko katika mataifa mbalimbali ya Afrika kunahitaji nchi kuimarisha mifumo yake ya maandalizi, ufuatiliaji na udhibiti wa maambukizi.

Ameeleza kuwa baadhi ya nchi zilizokumbwa na wagonjwa ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Uganda na Kenya, huku kukiwa na taarifa ya kisa kimoja nchini Nigeria.

Amesema hali hiyo ni tahadhari kuwa kisa cha ugonjwa wa kuambukiza kinaweza kujitokeza katika eneo lolote, hivyo ni muhimu kuimarisha uwezo wa wahudumu wa afya kuanzia ngazi ya jamii hadi hospitali za rufaa.

Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya WHO na Serikali unalenga kuhakikisha wataalamu wanapata maarifa ya kinadharia na vitendo kuhusu namna ya kujikinga, kutambua viashiria na kuchukua hatua stahiki wanapokutana na mgonjwa anayeshukiwa kuwa na ugonjwa wa kuambukiza.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Elizabeth Nyema amesema mafunzo hayo yamewajengea wataalamu uwezo wa kujilinda wanapohudumia wagonjwa na kuandaa mifumo ya utoaji huduma pale anapobainika mgonjwa mwenye viashiria vya ugonjwa wa kuambukiza.

Amesema jambo la msingi ni kuhakikisha wahudumu wanakuwa salama huku wagonjwa wakiendelea kupata huduma bila kusababisha maambukizi kusambaa kutoka kituo kimoja cha afya kwenda kingine.

Ameeleza kuwa wakati mwingine mgonjwa anaweza kufika kituoni akiwa na viashiria vya ugonjwa bila kubainika mapema, kisha kuendelea na safari yake kwenda maeneo mengine, hali inayoweza kuongeza hatari ya maambukizi kusambaa.

“Ni muhimu watoa huduma wajue namna ya kujikinga na pia kuhudumia wagonjwa. Unaweza kupata mteja mwenye changamoto bila kujua, akahudumiwa na kuendelea na safari kwenda halmashauri nyingine. Hilo si jambo zuri, hivyo tunapaswa kujiimarisha katika maeneo yetu,” amesema.

Kutokana na hali hiyo, Dk Nyema amezitaka halmashauri kuhakikisha wataalamu walioshiriki mafunzo hayo wanatoa mrejesho kwa wenzao katika vituo vingine vya afya ili maarifa yaliyopatikana yawafikie wahudumu wengi zaidi.

Amesema hatua hiyo ni muhimu zaidi kwa Mkoa wa Mbeya kutokana na kupakana na nchi za Malawi na Zambia, hivyo kuhitaji mifumo imara ya tahadhari na udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *