SMZ yapandisha kima cha chini cha mshahara sekta binafsi
Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imetangaza kupandisha kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi wa sekta binafsi kutoka Sh347,000 hadi Sh450,000 kwa mwezi kwa walio na mikataba ya maandishi, sawa na ongezeko la asilimia 30. Viwango hivyo vitaanza kutekelezwa Januari 1, 2027.
Akitangaza Oktoba 31, 2026, Waziri wa Kazi, Ajira, Vijana na Uwezeshaji, Ali Suleiman Ameir, amesema hatua hiyo inalenga kuboresha masilahi na haki za wafanyakazi kwa kuzingatia hali ya uchumi na gharama za maisha.
Amesema wafanyakazi wenye mikataba ya maandishi katika taasisi ndogo zilizoainishwa kwenye kanuni wataongezewa mshahara kutoka Sh250,000 hadi Sh300,000 kwa mwezi, sawa na asilimia 20. Kwa wafanyakazi wa kutwa, wenye ujuzi watalipwa Sh35,000 kwa siku kutoka Sh30,000, huku wasio na ujuzi wakipangiwa Sh30,000 kutoka Sh25,000.
Wafanyakazi wa majumbani wanaoishi kwa waajiri wao watalipwa Sh110,000 kwa mwezi kutoka Sh100,000, na wasioishi kwa waajiri kutoka Sh120,000 hadi Sh130,000. Kwa wafanyakazi wa kigeni, kiwango kipya ni Dola za Marekani 1,500 kwa mwezi kutoka Dola 1,000.
Waziri Ameir amesema waajiri wamepewa miezi mitatu kujiandaa kurekebisha bajeti, mifumo ya mishahara na mikataba ya ajira kabla ya viwango hivyo kuanza kutekelezwa Januari mosi, 2027.
Amesisitiza kuwa viwango vilivyotangazwa ni vya chini na havimzuii mwajiri kumlipa mfanyakazi zaidi kulingana na mkataba. Hatua hiyo inafuatia Serikali kupandisha kima cha chini cha mishahara kwa watumishi wa umma kutoka Sh300,000 hadi Sh500,000 kwa mwezi, kuanzia Oktoba mwaka huu, ili kuendana na gharama za maisha na kuongeza morali ya utumishi.
Akiambatana na tangazo hilo, Waziri Ameir amemuagiza Kamishna wa Kazi kuhakikisha kila mfanyakazi wa sekta binafsi anakuwa na mkataba wa ajira ifikapo Desemba mwaka huu, akisema hatavumilia mfanyakazi kufanya kazi bila mkataba.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Salama Mbarouk Khatib, amesema mshahara si mfumo wa malipo pekee, bali ni nyenzo muhimu ya kujenga uhusiano mzuri kati ya Serikali na sekta binafsi. Kamishna wa Kazi, Rashid Khamis Othman, amesema Zanzibar inaongozwa na Sheria ya Ajira Namba 11 ya mwaka 2005, sehemu ya tisa, vifungu vya 91 hadi 107, vinavyoeleza utaratibu wa kuanzishwa kwa Bodi ya Mishahara yenye jukumu la kuishauri Serikali.
