Muuguzi mstaafu aendelea kuhudumia jamii baada ya miaka 40 kazini
4 mins read

Muuguzi mstaafu aendelea kuhudumia jamii baada ya miaka 40 kazini

Iringa. Upendo wake kwa taaluma ya uuguzi ndio uliomfanya Mariam Mohamed kuichagua na kuitumikia kwa miaka 40, akitumia sehemu kubwa ya maisha yake kuwahudumia wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.

Mariam, mwenye umri wa miaka 70, anasema aliipenda sana taaluma hiyo, jambo lililompa msukumo wa kuendelea kutekeleza majukumu yake hadi alipostaafu baada ya miongo minne ya utumishi.

Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni nyumbani kwake, eneo la Gangilonga mkoani Iringa, Mariam amesema uamuzi wake wa kuingia katika taaluma ya uuguzi ulitokana na mapenzi aliyokuwa nayo kwa kazi hiyo.

Anasema katika kipindi chote cha utumishi wake alipata nafasi ya kushiriki shughuli mbalimbali zilizolenga kuboresha huduma za afya na kuongeza uelewa wa wananchi.

Miongoni mwa mambo anayoyakumbuka zaidi ni kushiriki kuandaa semina zilizolenga kuelimisha jamii kuhusu masuala ya afya.

Anasema semina hizo zilikuwa sehemu muhimu ya shughuli zake za kitaaluma kwa kuwa zilitoa nafasi ya kuwafikia wananchi na kuwapatia elimu kuhusu masuala mbalimbali ya afya.

Kwa mujibu wa Mariam, jukumu la muuguzi halikuishia kuwahudumia wagonjwa hospitalini pekee, bali pia lilihusisha kushiriki shughuli za kuelimisha jamii.

Katika miaka yake ya utumishi, Mariam alifanya kazi katika kipindi ambacho Mkoa wa Iringa ulikuwa bado haujagawanywa ili kupatikana Mkoa wa Njombe, hali iliyofanya safari yake ya kikazi kuhusisha vipindi tofauti vya kiutawala katika eneo hilo.

Miaka hiyo 40 ilimpa nafasi ya kushiriki katika utoaji wa huduma za afya katika mazingira mbalimbali, akitumia taaluma yake kuwahudumia wananchi waliohitaji huduma za uuguzi.

Anasema katika safari hiyo kulikuwa na nyakati za furaha na changamoto, lakini kila alipofanikiwa kumsaidia mgonjwa, aliona thamani ya kazi aliyokuwa akiifanya.

“Kuna mambo mengi ambayo nimeyaona katika kipindi changu cha kazi na wakati mwingine unakutana na changamoto, lakini unapomuona mgonjwa anapata nafuu, unapata faraja na kuona kwamba kazi yako ina maana katika maisha ya watu,” anasema Mariam. Kwa kuwa alikuwa muuguzi mkunga, anasema kuwahudumia wagonjwa na kuhakikisha wanapata huduma salama ni sehemu muhimu ya safari yake ya kitaaluma.

“Furaha kubwa kwa mhudumu wa afya ni kuona wagonjwa wanakuwa salama na hizo ni kumbukumbu ambazo mtu hawezi kuzisahau kirahisi baada ya kuzitumia sehemu kubwa ya maisha yake,” anasema Mariam.

Baada ya kustaafu, Mariam anaendelea na maisha yake kwa kujishughulisha na biashara ya duka pamoja na shughuli mbalimbali za nyumbani.

Hata hivyo, kustaafu kwake hakumaanishi kuachana kabisa na taaluma aliyoitumikia kwa miaka 40, kwani bado hutumia ujuzi wake wa uuguzi kuwasaidia watu wanaomzunguka wanapokutana na changamoto za kiafya.

Anasema hata akiwa katika shughuli zake za kila siku mtaani, anapokutana na mtu anayehitaji msaada wa kiuguzi, hujitahidi kumsaidia kwa kutumia uzoefu alioupata katika kipindi chote cha utumishi wake.

Kwa mujibu wa Mariam, uuguzi kwake si kazi inayopaswa kufanywa hospitalini pekee, bali ni wito wa kuwajali na kuwasaidia watu unaoendelea hata baada ya kustaafu rasmi. “Unaweza kustaafu na kuacha kwenda kazini kila siku, lakini huwezi kuacha moyo wa kumjali mtu na hata nikiwa mtaani, nikikutana na mtu mwenye changamoto na ninapoweza kumsaidia kwa ujuzi wangu, nafanya hivyo,” anasema.

Anaongeza kuwa uzoefu alioupata katika miaka hiyo umemfanya aendelee kuwa karibu na jamii, hasa pale watu wanapohitaji ushauri au msaada unaohusiana na taaluma yake.

“Nimeitumikia taaluma hii kwa miaka 40, kwa hiyo siwezi kujifanya kwamba nimeisahau kwa sababu tu nimestaafu, hivyo bado ninajivunia kuwa muuguzi na ninathamini nafasi ya kusaidia wengine,” anasema Mariam. Katika maisha yake ya familia, Mariam ana watoto wanne ambao kwa sasa ni watu wazima.

Atambuliwa kwa mchango wake

Hivi karibuni, historia yake ya utumishi katika taaluma ya uuguzi ilitambuliwa wakati wa Wauguzi Gala 2026 iliyofanyika Oktoba 25, 2026 katika Ukumbi wa Royal Palm Hall mkoani Iringa.

Katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, alimzawadia Sh500,000 kama ishara ya kutambua na kuthamini mchango wake katika sekta ya afya. Kamati ya maandalizi ya Wauguzi Gala nayo ilimkabidhi zawadi kwa kutambua miaka yake ya utumishi katika taaluma ya uuguzi.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa zawadi hizo, Mariam alisema: “Namshukuru Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa kutambua mchango wangu na kutimiza ahadi yake ya kunipatia fedha hizi na nimefurahi kuona utumishi wangu wa miaka 40 katika taaluma ya uuguzi umetambuliwa.”

Kwa Mariam, kutambuliwa huko ni sehemu ya kumbukumbu ya safari ndefu ya taaluma aliyochagua kuipenda na kuitumikia, huku akiendelea kuonyesha kuwa kustaafu hakujamuondolea utayari wa kuwasaidia watu katika jamii.

Kwa upande wake, Ofisa Muuguzi wa Mkoa wa Iringa na mwakilishi wa Chama cha Wauguzi Mkoa wa Iringa (Tana), Moses Tawete, alimpongeza Mariam kwa kutambuliwa kwa mchango wake katika taaluma ya uuguzi, huku akiiomba Serikali kuendelea kuthamini mchango wa wauguzi katika jamii.

“Nasi siku zote tumekuwa watu wa kazi na kutoa huduma, hivyo tunahitaji nasi kupewa furaha,” alisema Tawete.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *