Pale unapolazimika kujitenga na familia ili uwe mtu timamu
Dodoma. Mwezi huu ukiisha nitakuwa nimekamilisha mwaka sijazungumza kabisa na mtu yeyote wa familia yangu,” ananiambia Jonas, mtoto wa kiongozi mmoja wa dini kwenye mazungumzo yetu hvi karibuni mjini Iringa.
Jonas ni kijana wa miaka 30 anayeonekana kuwa mchangamfu ingawa ni mtulivu kwa haiba.
Tunazungumza mengi kama sehemu ya maandalizi ya ndoa anayotarajia kuifunga mwakani. Namuuliza kwa nini hasa hawasiliani na familia yake? Jonas anakunjua uso wake, “Nimechagua kuanza maisha mapya nje ya mzunguko wa sumu ya familia.”
Jambo hili linaweza kukushangaza ukilisikia kwa mtu. Unaposikia simulizi kama ya Jonas lazima unastuka kidogo. Unamwona kama mtu mwenye matatizo.
Hata nadharia nyingi za saikolojia zinakubaliana kuwa mtu timamu ni matokeo ya uhusiano na familia yake mwenyewe na kwamba kuhusiana kwa karibu na familia ndio msingi wa utu wa mtu.
Katika jamii nyingi, mtu anayejitenga na familia yake anachukuliwa kuwa tatizo. “Unawezaje kuwatupa watu waliokuzaa?” Tunayo hadi misemo inayosisitiza umuhimu wa familia, “Damu nzito kuliko maji,” “Damu ya familia haimwagiki”, “Mzazi ni Mungu wa pili duniani” na misemo mingine mingi inayotukumbusha kufungamana na familia.
Je, ni wakati wote tunalazimika kulinda uhusiano na familia? Vipi kama familia yako ni chanzo cha matatizo yanayokusumbua?
Simulizi ya Jonas inanikumbusha nadharia maarufu ya mshunuzi wa kale, Carl Jung, anayesema kuna wakati matatizo ya mtu ni familia yake mwenyewe.
Fikiria mazingira ambayo familia ndiyo inayobeba misimamo inayochochea tabia mbaya.
Fikiria familia ambayo inachukulia ukatili kuwa jambo la kawaida.
Fikiria familia zinazojitambulisha na tabia za ovyo ambazo kwa hakika zinachangia matatizo makubwa ya afya ya akili ya mwanafamilia.
Kitaaluma familia hizi huitwa familia mfu (dysfunctional families) kumaanisha familia zenye tabia zinazochangia maumivu, migogoro, mifarakano na hata kuzorota kwa afya ya akili za wanafamilia.
Carl Jung alifika mahali pa kufikiri watu wanaong’ang’ania uhusiano na familia za namna hii huendeleza matatizo kutoka kizazi kimoja kwenda kizazi kingine.
Kupitia kazi yake ya unasihi tiba, Jung aligundua wapo watu kama Jonas waliopona matatizo yao ya nafsi baada tu ya kufanya uamuzi wa kujitenga na familia zao.
Ujasiri wa kukata uhusiano na familia za namna hii inakuwa hatua muhimu ya mtu kushughulika na tabia mbaya za familia yake.
Jung ana dhana anayoiita family unconsciousness ambayo kimsingi inakuwa kama kivuli cha pamoja kinachoundwa na sheria, imani, mitazamo na mienendo inayoongoza namna wanafamilia wanavyotazama mambo, wanavyofanya uamuzi, wanavyoshughulikiana wao kwa wao na hata kuendesha maisha yao.
Katika kulielezea hili, Jung anasema familia huwa haziunganishwi na vinasaba pekee, bali dimbwi fulani la misimamo isiyoonekana, sheria zisizoandikwa ambazo kila mtu kwenye familia hulazimika kuzifuata kimya kimya akiamini ndio namna maisha yalivyo.
Hapa tunaweza kuwa na mifano ya vitu kama vitendo vya unyanyasaji na ukatili unaofanywa na wanafamilia dhidi yao wenyewe lakini ukichukuliwa kuwa jambo la kawaida na wakati mwingine ukipewa jina la “huu ndio utamaduni wetu,” au “Hii ndiyo nidhamu ya familia.” Inaweza pia kuwa tabia ya kupuuza mahitaji ya wanafamilia lakini kwa nje ikitetewa kama maadili na somo la mtoto kujifunza kujitegemea.
Jonas ananiambia, “Nyumbani ni kosa kusema waziwazi hata kama kila mtu anajua ukweli. Tunaogopa kuzungumza jambo ambalo tuna hakika litamkasirisha baba. Nyumbani kwetu baba hana sauti ya mwisho maana hakuna mwenye sauti.
Nikisema yeye ndiye mwenye sauti inayosikika na yeye peke yake ndiye anayefikiri nakuwa siko mbali na uhalisia. Hata unaposema umeumia baba ndiye anayeamua kama hayo maumivu uliyonayo ni ya kweli au unajidekeza.” Huu ni mfano wa namna familia zinavyoweza kuhahalisha ujinga wa binafsi wa mzazi na kuupachika jina la “uimara.”
Jonas ananionesha mfano wa sifa nyingine ya familia za namna hii tunayoweza kuiita uongo wa pamoja: “Baba yangu ni askofu anayeheshimika. Ukimwona anayoyafanya madhabahuni huwezi kuamini ni mtu katili anayeweza kufanya mambo ya aibu na wala asiombe msamaha yanapofahamika.”
“Kuna wakati baba alikuwa anampiga sana mama usiku. Ukithubutu kusema kitu asubuhi wewe mwenyewe unageuziwa kibao.
Kuna wakati hata mama mwenyewe alianza kuamini kuwa ukatili ule ulikuwa haki yake. Ukimtetea wewe ndiye unaonekana ni tatizo.”
Familia za namna hii wakati mwingine kwa nje huonekana ni za dini lakini wanafamilia wenyewe ndio wanaojua ukubwa wa pengo lililopo kati ya maneno na maana ya maneno hayo; tofauti ya tabia zinazoonekana hadharani na zile za siri na wanajua kwa hakika kile kinachoonekana kuwa umoja wa familia wakati mwingine kinafuga chuki, ugomvi, maigizo na hata utegemezi wa kifikra.
Jonas ananipa mfano, “nyumbani pale kuna vitu unakuwa unavijua vizuri lakini ukivisema hakuna anayevisema. Unapotaka kuongelea tatizo ambalo wote mnalijua, watu wanaona bora kubadilisha mada ili usiongelee kitu unachojua kinaharibu heshima ya familia.”
Unaweza kumlaumu mtu kama Jonas anayeamua kuondoka kwenye familia yake na ukahisi yeye ndiye tatizo lakini usichokijua ni kwamba mara nyingi watu kama Jonas wanakuwa wamechoka kuwa sehemu ya mzunguko wa udanganyifu na ukatili usioisha.
Familia za namna hii zinaweza kuwanyooshea kidole watu kama Jonas na kusema: “Unajitengaje na familia yako mwenyewe? Unamkataaje baba aliyekuzaa? Wewe ndiye mwenye shida” lakini kimsingi Jung aliwapachika kina Jonas jina la “mgonjwa aliyejitambua” (identified patient) kumaanisha mtu aliyegundua tatizo ambazo si kila mwanafamilia ameligundua na kuamua kufanya uamuzi mgumu kujinusuru.
Ukweli tusioukubali wengi wetu ni kwamba familia zetu wenyewe zinaweza kuwa chanzo cha matatizo yetu sugu. Kile tunachokitunza kwa uaminifu kama misimamo ya familia inaweza kuwa ndio uongo unaotufanya tugombane na watu wema ofisini, tushindwe kufanya uamuzi sahihi na wakati mwingine tabia hizo hizo za familia zikawa udongo unaotuzika kwenye kaburi la ‘maadili.’
Nilimuelewa Jonas. Ingawa ni kweli unaweza kujaribu kurekebisha hali ya mambo kwenye familia yako, kuna wakati kurekebisha ni kujichosha. Familia mfu huteswa na vidonda vya muda mrefu.
Kadri unavyojaribu kuvitibu ndivyo unavyozidi kugombana na mfumo unaovilea vidonda hivyo. Kuwa mtu halisi anayeweza kuanza upya, kwa hakika, kama ilivyo kwa Jonas, unahitaji kujitenga kiakili, kiroho, kihisia na hata kimwili wakati mwingine.
Kujitenga na familia za namna hii, Carl Jung anasema ni kujiokoa nafsi yako kutoka kwenye udanganyifu wa pamoja.
Huenda unapitia hali kama ya Jonas. Umefarakana na familia yako lakini kwa ndani unaamini umefanya uamuzi wa busara.
Umegombana na familia yako lakini ukitafakari unaona ilikuwa muhimu kufanya hivyo. Ingawa inaweza kukuumiza kuachana na watu uliozaliwa nao, watu unaochangia nao damu na nasaba, lakini inawezekana kabisa huo ukawa ndio mwanzo wa uhuru wa kweli na kubadilika kuwa binadamu timamu.

