Mbeya UWSA yaanza kuunganisha maji kwa mkopo
2 mins read

Mbeya UWSA yaanza kuunganisha maji kwa mkopo

Mbeya. Wananchi wa Mtaa wa Inolo na Uyole jijini Mbeya, wameanza kunufaika na huduma ya maji safi na salama kwa mkopo, baada ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mbeya (Mbeya UWSA) kuanza kuwaunganishia huduma hiyo kwa utaratibu unaowawezesha kulipa gharama kwa awamu ndani ya miezi mitatu.

Utaratibu huo unalenga kuwawezesha wananchi, hususan wa kipato cha chini, kupata huduma ya maji bila kikwazo cha kulipa gharama  za kuunganishiwa kwa wakati mmoja.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alilolitoa Oktoba 16, 2026, wakati wa ziara ya kikazi ya Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, mkoani Mbeya.

Katika ziara hiyo, Aweso alitakiwa kueleza mikakati ya Serikali ya kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa maji katika Bonde la Uyole.

Awali, Aweso alikiri kuwepo kwa changamoto ya maji, akieleza kuwa mahitaji ya eneo hilo ni lita milioni 12 kwa siku, huku uzalishaji ukiwa lita milioni nane hali inayosababisha upungufu wa lita milioni nne.

Kutokana na hali hiyo, aliziagiza mamlaka husika kuweka utaratibu wa kuwaunganishia wananchi huduma ya maji kwa mkopo ili kurahisisha upatikanaji wake.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Oktoba 21, 2026, baada ya uzinduzi wa huduma hiyo, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Mbeya UWSA, Neema Mwangwala amesema mamlaka hiyo imeanza kutekeleza agizo hilo kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi.

Amesema utaratibu huo unawapa wananchi fursa ya kuunganishiwa maji bila kulipa gharama zote za awali kwa mara moja, huku wakipewa miezi mitatu ya kurejesha malipo hayo kwa awamu.

“Utaratibu huu unalenga kuwawezesha wananchi kupata huduma ya maji safi kwa urahisi bila kulazimika kulipa gharama za awali kwa awamu moja kama ilivyozoeleka. Tunaamini huduma hii itamkomboa mwananchi wa kipato cha chini,” amesema Mwangwala.

Katika hatua nyingine, amewataka wananchi kuepuka kutoa fedha taslimu kwa mtumishi yeyote wa mamlaka hiyo kwa ajili ya kupata huduma, akisisitiza kuwa malipo yote yanapaswa kufanyika kupitia namba ya malipo (Control Number) inayotolewa na mamlaka hiyo.

Kuhusu gharama za kuunganishiwa maji, Mwangwala amesema zinategemea umbali wa eneo la mteja, huku akieleza kuwa taarifa kamili kuhusu gharama hizo zitatolewa baada ya kukamilika kwa hatua husika.

Kwa upande wake, mkazi wa Kata ya Inolo, Neema Aloyce, ameishukuru Serikali na Mbeya UWSA kwa kuanzisha utaratibu huo, akisema utasaidia kupunguza changamoto ya maji iliyokuwa ikiwakabili wananchi wa maeneo hayo.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *