Tisa wadakwa tuhuma mauaji ya mwanafunzi Pemba
2 mins read

Tisa wadakwa tuhuma mauaji ya mwanafunzi Pemba

Unguja. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba limewakamata watuhumiwa zaidi ya 20 kwa tuhuma mbalimbali kufuatia msako na doria zilizofanyika kisiwani humo.

Miongoni mwa waliokamatwa katika msako huo ulioanza Septemba 23, hadi Oktoba 21, 2026 ni pamoja na watuhumiwa tisa wanaohusishwa na tukio la mauaji ya mwanafunzi Raiyan Hemed Amour (15).

Katika taarifa kwa umma iliyotolewa leo na Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, upelelezi unaendelea na utakapokamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, William Mwampaghale  kifo cha mwanafunzi huyo kilitokea Oktoba 2, 2026, aliporipotiwa kupotea.

Siku mbili baadaye, Oktoba 4, 2026 saa 3:20 asubuhi, mwili wake ulipatikana katika kichaka huko kijiji cha Kwale Mpona, Shehia ya Finya, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba ukiwa umekatwa kiganja cha mkono wa kulia kwa kutumia kitu chenye ncha kali.

Oktoba 5, 2026 Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba lilitangaza kuanza uchunguzi wa tukio hilo.

Raiyan alikuwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Kizimbani, Wilaya ya Wete na mkazi wa Kijiji cha Kwale Mpona, Shehia ya Finyu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa siku hiyo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, mwanafunzi huyo aliondoka nyumbani kwao Oktoba 2, saa 12:00 asubuhi kwenda shuleni, lakini hakurejea.

Kamanda alisema baadaye siku hiyo, saa 3:20 usiku, baba mzazi wa Raiyan alifika katika Kituo cha Polisi Wete kutoa taarifa ya kupotea kwa mtoto wake na jalada la uchunguzi likafunguliwa.

Alisema mwili wa mwanafunzi huyo ulibainika baadaye ukiwa ndani ya kichaka na kiganja cha mkono wa kulia kikiwa kimekatwa kwa kutumia kitu chenye ncha kali.

Mwili huo ulipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Wete, Kinyasini kwa ajili ya uchunguzi wa kitabibu na baadaye ulikabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya taratibu za mazishi.

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar ililaani kifo cha mwanafunzi huyo, ikikitaja kuwa ni kitendo cha kikatili na kisicho cha kibinadamu.

Wizara ilivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina na kwa haraka ili kubaini waliohusika na kuwachukulia hatua za kisheria.

Pia, iliitaka jamii kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa muhimu zinazoweza kusaidia uchunguzi wa tukio hilo.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *