Tume yaanza kusaka waliopanga, kufadhili ghasia za Oktoba 29
Dar es Salaam. Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, imeanza kuchunguza watu waliopanga, kufadhili, kuratibu na kushiriki katika ghasia zilizotokea kipindi hicho, baada ya kukamilisha uchunguzi wa awali kuhusu matumizi ya nguvu katika kudhibiti vurugu hizo.
Hatua hiyo inaashiria kuanza kwa uchunguzi unaolenga kubaini wahusika na nafasi ya kila mmoja katika matukio hayo, huku tume ikiwataka wananchi na taasisi zenye taarifa au vielelezo vinavyoweza kusaidia uchunguzi kuviwasilisha.
Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Shaban Lila akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne, Oktoba 27, 2026 jijini Dar es Salaam, amesema tume imekamilisha ukusanyaji wa ushahidi katika wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam na sasa imeanza kutekeleza hadidu ya rejea inayohusu kuwabaini waliohusika kupanga, kufadhili, kuratibu na kufanya ghasia wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
“Kwa upande wa Dar es Salaam, tume sasa imeanza kukusanya taarifa ambazo zitaiwezesha kutekeleza hadidu ya rejea namba moja, inayohusu kuwabaini wahusika katika kupanga, kufadhili, kuratibu na kufanya ghasia wakati ule wa uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba mwaka 2025,” amesema Jaji Lila.
Jaji Lila amesema kazi ya tume inaongozwa na hadidu za rejea zinazobainisha maeneo yanayopaswa kuchunguzwa, ikiwemo kubaini wahusika wa ghasia na kuchunguza malalamiko kuhusu namna vurugu zilivyodhibitiwa.
Amesema katika hatua ya awali, tume ilijikita katika hadidu za rejea zinazohusu matumizi ya nguvu wakati wa kudhibiti vurugu, malalamiko ya watu kupigwa risasi za moto nje ya maeneo ya ghasia, watu kupotea na wengine kupata majeraha makubwa.
Eneo jingine lililochunguzwa ni malalamiko kuhusu watoto, watu wenye ulemavu na wenye hali mbalimbali za kiafya walioathirika na vurugu hizo.
Aidha, tume ilichunguza malalamiko ya matumizi ya nguvu kupita kiasi na madai ya kutofuatwa kwa taratibu na miongozo iliyowekwa kisheria katika kudhibiti vurugu na ghasia.
“Katika kudhibiti vurugu na ghasia, zipo taratibu na sheria ambazo zimewekwa na zinapaswa kufuatwa. Kwa hiyo, yalikuwepo malalamiko kwamba baadhi ya taratibu na miongozo iliyowekwa haikufuatwa wakati wa kudhibiti ghasia zile,” amesema.
Kwa mujibu wa Jaji Lila, tume imefanyia kazi hadidu hizo za rejea Dar es Salaam na sasa inaendelea na uchunguzi unaolenga kubaini watu waliohusika katika kupanga, kufadhili, kuratibu na kutekeleza ghasia hizo.
Hata hivyo, uchunguzi huo unaendelea kwa kuzingatia taarifa na ushahidi unaowasilishwa kwa tume, huku malalamiko yaliyopokelewa yakiwa ni sehemu ya mambo yanayohitaji kuchunguzwa na kubainishwa.
Jaji Lila amesema tume imepokea taarifa kuhusu mazingira ya maeneo yaliyotokea ghasia na uvunjifu wa sheria, pamoja na ushahidi kuhusu nguvu iliyotumika katika kudhibiti hali hiyo.
Amesema mwitikio wa wananchi katika wilaya zilizotembelewa umekuwa mzuri, huku akisisitiza kuwa kukamilika kwa mikutano ya ukusanyaji ushahidi katika wilaya hizo hakumaanishi kuwa wananchi wamezuiwa kuwasilisha taarifa zaidi.
Ameeleza kuwa wananchi ambao hawakupata nafasi ya kuwasilisha ushahidi wakati tume ilipofika katika maeneo yao wanaweza kuendelea kufika kwenye ofisi za tume na kutoa taarifa zao.
“Katika kufanya uchunguzi huu, tume itaendelea kuwasikiliza wananchi wenye ushahidi mbalimbali. Tutapokea vielelezo kutoka kwa wananchi na vyombo mbalimbali, zikiwemo taasisi za Serikali na binafsi,” amesema mwenyekiti huyo wa Tume.
Ametoa wito kwa wananchi na taasisi zote zenye taarifa zinazoweza kusaidia uchunguzi kuziwasilisha ili kuiwezesha tume kutekeleza majukumu yake.
Tume hiyo ilianza kutekeleza majukumu yake Agosti 7, 2026, baada ya kuundwa na Rais Samia Suluhu Hassan ikiwa ni utekelezaji wa pendekezo la ripoti ya Tume ya Jaji Othman Chande iliyopendekeza kuundwa kwa tume ya kuchunguza matukio ya jinai yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi.
