Shahidi: Kahyoza alisema hajui kilichomsukuma kumpiga trafiki
Dar es Salaam. Shahidi wa nne wa Jamhuri katika kesi ya shambulio la mwili inayomkabili daktari bingwa wa magonjwa ya ndani wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH)–Mloganzila, Conrad Kahyoza, ameieleza Mahakama kuwa mshtakiwa huyo alimweleza hajui kilichomsukuma kumshambulia askari wa usalama barabarani (trafiki).
Shahidi huyo, PC 24315 Inspekta Machera wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Oysterbay, amesema Dk Kahyoza alimweleza kuwa siku chache kabla ya tukio hilo alikuwa amefiwa na mkewe na nyumba yake kuungua moto.
Inspekta Machera ametoa maelezo hayo leo Jumanne, Oktoba 27, 2026, wakati akitoa ushahidi katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, akieleza alivyomuuliza mshtakiwa kuhusu tukio hilo.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Abdul-Majid Mtukusye, shahidi huyo amesema siku ya tukio alikuwa zamu, akiongoza magari katika Barabara ya Bagamoyo, eneo la Mwenge, karibu na kituo cha daladala cha Mwenge Efatha.
Amesema saa 1:35 asubuhi, mwendesha bodaboda mmoja alimfikia na kumjulisha kuwa eneo la Lugalo kulikuwa na askari wa trafiki aliyekuwa chini akipigwa na raia.
Kutokana na taarifa hiyo, Inspekta Machera amesema alipanda bodaboda iliyompeleka eneo la tukio, ambako aliwakuta askari watatu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakiwa wamesimama, huku pembeni kukiwa na askari mmoja wa usalama barabarani na raia mmoja wakiwa wamekaa. Amesema alipowauliza wanajeshi hao kilichotokea, walimweleza kuwa askari wa usalama barabarani alikuwa ameshambuliwa na raia.
Kwa mujibu wa shahidi huyo, alipomuuliza askari aliyeshambuliwa kuhusu kilichotokea, alimweleza kuwa alikuwa amesimamisha magari matatu yaliyokuwa yakipita katika barabara ya huduma (service road), likiwamo gari la mshtakiwa.
Amesema askari huyo alimweleza kuwa baada ya kuchomoa ufunguo wa gari hilo, alipogeuka, Dk Kahyoza alimpiga ngumi na kumwangusha chini, kisha akaendelea kumshambulia.
Shahidi huyo amesema askari aliyeshambuliwa alimtaja mshambuliaji wake kwa jina la Conrad na kueleza kuwa alikuwa daktari.
“Samahani, afande, sijui nilichokifanya, lakini juzi nimetoka kufiwa na mke wangu na kuunguliwa na nyumba yangu,” amesema Inspekta Machera akimnukuu Dk Kahyoza.
Amesema baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote, wananchi waliokuwa eneo hilo walianza kupiga kelele wakilalamikia kitendo cha raia kumshambulia askari akiwa kazini.
Kutokana na hali hiyo, Inspekta Machera amesema alimchukua askari aliyeshambuliwa pamoja na Dk Kahyoza na kuwapeleka katika Kituo cha Polisi cha Survey, ambako mlalamikaji alifungua kesi, kabla yeye hajaondoka.
Wakati wa maswali ya dodoso kutoka kwa wakili wa utetezi, Yohana Kibingu, Inspekta Machera amesema askari hutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria, lakini hakuna kipengele kinachowaruhusu kuchomoa funguo za magari ya wateja wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao.
Hata hivyo, amekiri kuwa ujenzi wa barabara ulikuwa ukiendelea katika eneo hilo, huku akieleza kuwa kutumia barabara ya huduma kwa magari ni kosa kisheria kwa kuwa barabara hizo zimekusudiwa kutumiwa na watembea kwa miguu na wanafunzi.
Awali, shahidi wa tatu wa Jamhuri, J6102 PC Godwin, daktari wa Hospitali ya Polisi iliyopo Kilwa Road, aliieleza mahakama kuwa siku ya tukio alimchunguza mlalamikaji, Sajenti Andrew, aliyefikishwa hospitalini akiwa na Fomu ya Polisi Namba Tatu (PF3).
Amesema askari huyo alikuwa akitokwa na machozi na kumweleza kuwa alishambuliwa hadi kupoteza fahamu, huku akilalamikia maumivu makali katika kidole cha kati cha mkono wa kushoto.
Dk Godwin amesema wakati wa uchunguzi alimwona mgonjwa akiwa na uvimbe katika paji la uso. Pia, baada ya kumfanyia kipimo cha mionzi (X-ray), alibaini kuwa kidole cha kati cha mkono wa kushoto kilikuwa kimepinda.
Amesema alimpa dawa za kupunguza maumivu na kumshauri kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kufanyiwa kipimo cha CT Scan.
Dk Godwin amesema baada ya kutoa huduma ya uchunguzi na matibabu, alijaza fomu ya matibabu ambayo ameiwasilisha mahakamani na kupokelewa kama kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka.
Dk Kahyoza anadaiwa kumshambulia Sajenti Andrew Septemba 8, 2026, saa 1:30 asubuhi, katika Barabara ya Bagamoyo, eneo la Makongo, Dar es Salaam, wakati askari huyo akitekeleza majukumu yake. Anashtakiwa kwa kosa hilo chini ya kifungu cha 243(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, Toleo la mwaka 2023.
Mshtakiwa alipandishwa kizimbani na kusomewa shtaka hilo Septemba 10, 2026.
Kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi, Jacqueline Rugemalira itaendelea kesho Oktoba 28, 2026, ambapo mahakama inatarajiwa kupokea ushahidi wa shahidi wa tano na wa mwisho wa Jamhuri.
