Mama wa pacha wanne Geita aomba msaada wa malezi
3 mins read

Mama wa pacha wanne Geita aomba msaada wa malezi

Geita. Gharama za maziwa mbadala, matibabu na mahitaji ya watoto wachanga zimekuwa changamoto kwa Kefrine Mhande, mkazi wa Kata ya Nyamalimbe, Wilaya ya Geita, aliyejifungua watoto pacha wanne na sasa anaomba msaada wa Serikali na wadau.

Mhande ameiomba jamii kumsaidia kupata bima za afya kwa watoto hao, maziwa mbadala na mahitaji mengine muhimu ili kupunguza gharama za malezi ya watoto hao wanne.

Amesema idadi ya watoto hao inahitaji maandalizi na gharama kubwa, hivyo msaada wa wadau utakuwa muhimu katika kuhakikisha wanapata mahitaji yao.

Mhande alijifungua watoto hao katika Hospitali ya Manispaa ya Geita Alhamisi, Oktoba 22, 2026, baada ya kufika hospitalini hapo saa 2:30 usiku. Alijifungua kwa njia ya kawaida saa 3 usiku.

Mbali na kuomba bima za afya na maziwa mbadala, mama huyo ameomba msaada wa mavazi na mahitaji ya watoto yatakayohitajika watakapofikia umri wa kwenda shule.

Pamoja na changamoto hizo, amemshukuru mume wake kwa kuwa karibu naye wakati wa ujauzito, kujifungua na malezi ya watoto hao.

“Mume wangu amenifariji mno na amekuwa mboni ya jicho langu, maana niliona mzigo ni mkubwa. Angekuwa mbali ningejisikia upweke, lakini kwa sasa tuko wote, tunatiana moyo na kufarijiana,” amesema.

Kefrine Mhande mkazi wa Nyamalimbe,mama aliyejifungua watoto mapacha wanne katika Hospitali ya Manispaa ya Geita, ikiwa ni uzao wake wa pili.

Mume wake, Zengo Lutego, ameiomba Serikali na wadau wengine kujitokeza kusaidia familia hiyo, hasa katika upatikanaji wa bima za afya na maziwa mbadala.

“Msaada ambao tunaomba kwa Watanzania na Serikali kwa ujumla ni bima ya afya kwa watoto. Lakini pia kwa sababu wako wengi, maziwa ya mama pekee hayatatosha, atahitaji maziwa mbadala ambayo nayo yatahitaji gharama. Gharama hiyo sitaweza kuihimili kwa watoto wote,” amesema Lutego.

Pia amewataka wanaume kuwasaidia wake zao wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua, ikiwemo kuwasindikiza hospitalini wanapohisi uchungu na kuwapa msaada katika malezi.

Daktari wa Kitengo cha Watoto katika Hospitali ya Manispaa ya Geita, Dk Caroline Muya, amesema watoto hao wanaendelea kupata huduma za kitabibu na hospitali itaendelea kuwafuatilia katika kipindi chote watakachokuwa chini ya uangalizi wake.

Amesema watoto wawili walizaliwa wakiwa na changamoto ya upumuaji na walipatiwa msaada wa kitabibu, huku hali zao zikiendelea vizuri.

Dk Muya amesema watoto hao walizaliwa kabla ya wakati, katika wiki ya 32 ya ujauzito badala ya wiki ya 38 iliyotajwa katika taarifa ya awali kama muda wa kuzaliwa.

Ameeleza kuwa watoto hao wamepata huduma ya oksijeni na sasa wanaendelea na huduma ya Kangaroo Mother Care inayohusisha kumweka mtoto mchanga kwenye mgusano wa ngozi kwa ngozi na mama au mlezi ili kusaidia ukuaji na ongezeko la uzito.

“Tumekuwa tukishirikiana na mama wa watoto, wamekuwa wakilelewa. Wametoka kwenye oksijeni na wanaendelea na huduma tunaita Kangaroo Mother Care ili waweze kuongeza uzito,” amesema.

Zengo Lutego, Baba mzazi wa watoto mapacha wanne akiwa hospitali ya Manispaa ya Geita baada ya mkewe kujifungua.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa, watoto hao walizaliwa wakiwa na uzito tofauti, hali inayohitaji ufuatiliaji wa karibu wa afya na ukuaji wao.

Wadau wanaotaka kusaidia familia hiyo wanaweza kutuma fedha au mahitaji kupitia namba 0766182959, kwa jina la Zengo Lutego.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *