Takukuru yabaini mapungufu miradi 49 ya Sh14.49 bilioni
2 mins read

Takukuru yabaini mapungufu miradi 49 ya Sh14.49 bilioni

Moshi. Ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma katika miradi 49 ya maendeleo yenye thamani ya Sh14.49 bilioni mkoani Kilimanjaro umebaini mapungufu katika miradi yote iliyokaguliwa, huku wahusika wakitakiwa kufanya marekebisho.

Miradi hiyo inahusisha sekta za elimu, afya, maji, usafirishaji na mawasiliano, kwa mujibu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kilimanjaro.

Akitoa taarifa ya mafanikio ya taasisi hiyo kwa kipindi cha Aprili hadi Septemba 2026, Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Sabas Salehe, amesema mapungufu yaliyobainika yamewasilishwa kwa wahusika ili wayafanyie kazi.

“Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro imefanya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma katika miradi ya maendeleo 49 yenye thamani ya Sh14.49 bilioni katika sekta za elimu, afya, maji, usafirishaji na mawasiliano. Katika ufuatiliaji huo, miradi yote 49 ilibainika kuwa na mapungufu,” amesema Salehe.

Amesema ufuatiliaji huo unalenga kuimarisha usimamizi wa fedha za umma na kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa na malengo yaliyokusudiwa.

Katika hatua nyingine, Takukuru imefanikisha kurejeshwa kwa ekari 21 za ardhi ya Kijiji cha Kitoghoto, Wilaya ya Mwanga, zilizokuwa zimeuzwa na viongozi watatu wa kijiji hicho kwa Sh12.6 milioni bila kufuata taratibu za uuzaji wa ardhi ya kijiji.

Salehe amesema ardhi hiyo imerejeshwa kwa Serikali ya kijiji baada ya Takukuru kushinda shauri lililofunguliwa dhidi ya viongozi hao katika Mahakama ya Wilaya ya Mwanga.

Amesema mahakama iliamua ardhi hiyo irejeshwe kwa kijiji baada ya kubaini kuwa mauzo hayo hayakutambuliwa na kijiji.

“Ofisi ya Takukuru Mwanga,  Aprili 2026, imefanikisha urejeshwaji wa ardhi ya ekari 21, mali ya Kijiji cha Kitoghoto, ambayo ilikuwa imeuzwa na viongozi watatu wa kijiji hicho kwa muwekezaji kwa Sh12.6 milioni bila kufuata utaratibu wa mauzo ya ardhi ya kijiji,” amesema Salehe.

Mkazi wa eneo hilo, Mathius Cornel amesema, “tunashukuru waliotoa taarifa hizi na jambo hili kushughulikiwa mapema na Serikali, kwani baadhi ya viongozi wamekuwa wabinafsi na kufanya mambo kienyeji. Tunaishukuru sana Serikali kwa kuturejeshea ardhi yetu.

Naye Theopista Mrema, mkazi wa Mkoa wa Kilimanjaro, amesema Serikali inapaswa kuendelea kuwachukulia hatua viongozi wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao na kusababisha hasara kwa umma.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *