Tanzania yaweka vipaumbele vinne kuelekea COP31
3 mins read

Tanzania yaweka vipaumbele vinne kuelekea COP31

Dar es Salaam. Tanzania imeweka vipaumbele vinne vya kimkakati itakavyovisisitiza katika mkutano wa 31 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), utakaofanyika Antalya, Turkiye, Novemba 9 hadi 20, 2026.

Vipaumbele hivyo ni kuimarisha ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, upatikanaji wa fedha za tabianchi, kujenga uwezo wa taasisi na upatikanaji wa teknolojia, pamoja na kukabiliana na hasara na uharibifu unaotokana na mabadiliko hayo.

Akizungumza leo Oktoba 28,2026  jijini Dar es Salaam, katika warsha ya kitaalamu na ya kitaifa ya ngazi ya juu ya maandalizi ya COP31, Mkurugenzi wa Mazingira katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Kemilembe Mutasa, amesema Tanzania itashiriki mkutano huo ikiwa na msimamo unaolenga kuhakikisha hatua za tabianchi zinachangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesema kaulimbiu ya Tanzania ni “Tanzania’s Inclusive Climate Action for Dira 2050: Building a Resilient, Green and Prosperous Nation”, inayosisitiza hatua jumuishi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa ajili ya kujenga taifa imara, la kijani na lenye ustawi na utekelezaji wa Dira 2050.

Mutasa amesema maandalizi hayo pia yanalenga kuiwezesha Tanzania kushiriki mazungumzo ya pande mbili na mikutano ya pembeni ya ngazi ya juu, ili kutetea maslahi ya nchi na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.

Alitaja nishati safi ya kupikia kuwa miongoni mwa masuala yatakayopewa kipaumbele, akisema Tanzania inalenga kuendeleza juhudi za kuhamasisha taasisi zinazohudumia zaidi ya watu 100 kutumia nishati safi.

Kwa upande wake, Ghaamid Abdulbasat Hatibu, Ofisa wa Mawasiliano ya Bahari wa Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (IUCN), amesema kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kunapaswa kwenda sambamba na uhifadhi wa mazingira na bayoanuai.

“…dunia haikosi sera za utekeleji. Dunia inakosa utekelezaji” amesema akisisitiza ushirikiano kwenye kulinda mazingira na kauli moja kama nchi.

Pia, alitaja umuhimu wa kuweka jamii katikati ya juhudi za uhifadhi, kutambua maeneo yanayosimamiwa na jamii na kuendeleza urejeshaji wa mifumo ya ikolojia.

Amesema Tanzania imechangia juhudi hizo kupitia urejeshaji wa zaidi ya hekta 110,000 za maeneo ya pwani.

Baadhi ya wadau kutoka sekta mbalimbali nchini wakifuatilia majadiliano wakati wa warsha ya kitaifa ya maandalizi ya COP31 iliyofanyika Dar es Salaam, Oktoba 2026. Warsha hiyo ilijadili vipaumbele vya Tanzania kuhusu fedha za tabianchi, ustahimilivu, teknolojia na kukabiliana na hasara na uharibifu unaotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Naye Naibu Katibu Mkuu (Muungano) katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Latifa Mohammed Khamis, amesema maandalizi ya COP31 yanatoa fursa ya kuweka maelekezo ya kisera na kimkakati yatakayolinda na kuendeleza maslahi ya Taifa.

Amesema, “ uenyekiti wa Tanzania katika Kundi la Afrika la Wajadili wa Mabadiliko ya Tabianchi (AGN) wakati wa COP30 uliimarisha nafasi ya nchi katika diplomasia ya tabianchi”.

Ametaja mafanikio yaliyopatikana kupitia ushiriki huo kuwa ni pamoja na kuanzishwa kwa kituo cha kujifunzia kwa vijana, kuandaliwa kwa kitabu cha historia ya AGN na kuanzishwa kwa kituo cha mtandao wa Santiago nchini.

Ameongeza kuwa, “Tanzania imeendelea kupata ufadhili wa miradi inayolenga kuimarisha ustahimilivu wa jamii na mifumo ya ikolojia, ikiwamo miradi ya kukabiliana na ukame katika mikoa ya kati, usimamizi wa Bonde la Usangu na kuendeleza nishati safi kupitia ushirikiano na Norway na TaTEDO”.

Khamis amesema Serikali pia imewasilisha ombi la Dola za Marekani milioni 15 kwa ajili ya kulinda na kufuatilia hasara na uharibifu unaotokana na mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kuomba msaada wa kiufundi kupitia Mtandao wa Santiago ili kufanya tathimini.

Akizungumza katika warsha hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa, amesema, “diplomasia ya Tanzania inapaswa kuzingatia ushirikiano wa kimataifa, utekelezaji wa Dira 2050 na mahitaji ya wananchi”.

Amesisitiza umuhimu wa uzalendo, mshikamano na kujitolea kwa wadau wote, akisema hatua zinazochukuliwa katika majadiliano ya tabianchi zinapaswa kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *