Sirro aagiza uchunguzi moto ulioteketeza vibanda 13 Kigoma
Kigoma. Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, ameagiza uchunguzi kufanyika kubaini chanzo cha moto ulioteketeza vibanda 13 vya biashara katika Soko la Mwandiga, huku baadhi ya wafanyabiashara wakihofia huenda tukio hilo limetokana na hujuma.
Moto huo uliozuka usiku wa kuamkia Oktoba 28, 2026, umeteketeza vibanda vilivyokuwa vikitumika kwa biashara za tiba asili, vitenge, dawa za binadamu, nafaka na stoo ya mazao ya chakula na kusababisha hasara kwa wafanyabiashara.
Akizungumza baada ya kukagua eneo la tukio leo Jumatano, Oktoba 28, 2026, Sirro amewapa pole wafanyabiashara walioathirika, akisema Serikali ya mkoa itafikiria hatua za kuwasaidia baada ya uchunguzi kubaini chanzo cha moto huo.
Amewataka wafanyabiashara kuchukua tahadhari dhidi ya vitu vinavyoweza kusababisha moto, ikiwemo mishumaa na udi unaowashwa na kuachwa kwa muda mrefu ndani ya maduka.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, akizungumza na wafanyabiashara soko la Mwandiga, halimashauri ya Wilaya ya Kigoma, baada ya vibanda 13 kuteketea usiku wa kuamkia leo Oktoba 28, 2026.
“Kama ni ajali nyingine ya kawaida na hakuna mtu aliyehusika, basi sisi kama Serikali ya mkoa tutaona tunafanya nini ili kusaidia. Huu si wakati wa kulaumiana. Naomba tupeane ushirikiano na vyombo vya usalama ili kujua chanzo ni nini,” amesema Sirro.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kigoma, Mrakibu Mwandamizi Agastine Magere, amewapongeza wananchi kwa kushirikiana na jeshi hilo kuzima moto na kuokoa vibanda vingine, pamoja na soko la ndani ambalo halikuteketea.
Hata hivyo, amesema chanzo cha moto huo bado hakijafahamika, huku akizitaka halmashauri na wadau wanaohusika na ujenzi wa masoko kuhakikisha miundombinu inazingatia mahitaji ya huduma za dharura.
Magere amesema kutokuwepo kwa njia za kutosha za kupitisha magari ya zimamoto kunaweza kuchelewesha huduma wakati wa matukio ya moto.
“Changamoto iliyojitokeza kwanza ni miundombinu ya soko. Ninashauri wananchi wa Kigoma na wakurugenzi, wanapojenga masoko, zile njia za dharura na milango mikubwa iachwe wazi, isijengwe vibanda, kwa sababu inaweza kusababisha ucheleweshaji wa gari la zimamoto kupita,” amesema.
Baadhi ya bidhaa za tiba asili zilizoteketea kwa moto usiku wa kuamkia leo Oktoba 28, 2026 kwenye soko la Mwandiga mkoani Kigoma.
Baadhi ya wananchi na wafanyabiashara wa Soko la Mwandiga wameiomba Serikali kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha moto huo, wakieleza kuwa ni tukio la tatu la moto kutokea katika soko hilo.
Wamesema katika matukio mawili yaliyopita, moto ulianzia katika vijiwe vya kuuzia tangawizi vilivyo jirani na soko.
Mmoja wa wafanyabiashara hao amedai huenda moto huo haukusababishwa na hitilafu ya umeme, akieleza kuwa vibanda vingi havikuwa na huduma hiyo.
“Hili tukio si kwamba ni umeme, haya mabanda yetu yote hatujafunga umeme isipokuwa banda moja tu. Hapa kutakuwa na watu binafsi wenye chuki zao binafsi, labda ndiyo walikuja kuchoma,” amesema.
Hata hivyo, madai ya wafanyabiashara kuhusu uwezekano wa hujuma bado hayajathibitishwa, huku uchunguzi ukiwa muhimu kubaini chanzo halisi cha moto huo na kama kuna mtu aliyehusika.

