Manusura ajali ya treni Hispania asimulia alivyojikuta amerushwa hewani
Hispania. “Nilipozinduka, nilijikuta hewani.” Hiyo ni sehemu ya simulizi ya Josimar Medina, raia wa Peru mwenye umri wa miaka 31, aliyenusurika ajali ya treni ya mwendo kasi iliyoua watu 68 na kujeruhi wengine nchini Hispania.
Medina, aliyekuwa nchini humo kwa mapumziko na mpenzi wake, ameiambia France 24 kuwa alikuwa amelala ndani ya treni ya kampuni ya serikali ya Renfe wakati ajali hiyo ilipotokea Jumatano, Oktoba 28, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ajali hiyo ilitokea katika eneo la Castilla-La Mancha, katikati mwa Hispania, baada ya treni ya Renfe kugonga sehemu ya nyuma ya treni ya kampuni binafsi ya Iryo iliyokuwa imesimama.
Simulizi za manusura zinaeleza jinsi abiria walivyokumbwa na tukio hilo ghafla, huku wengine wakikumbuka vurugu zilizotokea ndani ya mabehewa baada ya mgongano.
Pablo Mejia, mwenye umri wa miaka 42, amesema kubadili kiti dakika za mwisho kulimsaidia kunusurika, ingawa alipata majeraha kichwani.
Akieleza hali aliyokutana nayo baada ya ajali hiyo, Mejia amesema alikuta abiria wakiwa wameanguka chini na wengine wakiwa wameangukiana, huku viti vikiwa vimevunjika na mizigo ikiwa imetawanyika.
Amesema mgongano huo ulikuwa mkali na kusababisha taharuki miongoni mwa abiria.
“Nadhani nimezaliwa upya,” amesema Mejia, akieleza alivyojisikia baada ya kunusurika katika ajali hiyo.
Wakati manusura wakisimulia walichopitia, ndugu wa waathirika wamekuwa wakikusanyika katika kituo cha msaada kilichoanzishwa katika shule moja katika kijiji cha Urda, takribani kilomita 130 kusini mwa Madrid, wakitafuta taarifa kuhusu wapendwa wao.
Baadhi yao wameonekana wakilia huku wakisubiri taarifa, wakati wafanyakazi wa Shirika la Msalaba Mwekundu wakitoa msaada wa kisaikolojia.
Mwanasaikolojia wa shirika hilo, Carmen Garcia, amesema familia na waathirika wanapitia kipindi kigumu, huku kila mmoja akikabiliana na msiba kwa namna yake.
Mamlaka zimefungua ofisi katika miji ya Madrid, Toledo, Cordoba na Seville kwa ajili ya kupokea sampuli za vinasaba (DNA) zitakazosaidia kutambua miili ya watu ambao utambulisho wao bado haujafahamika.
Wakati huohuo, waokoaji waliendelea kuchunguza mabaki ya treni usiku, wakitumia kreni kuinua vipande vya vyuma vilivyoharibika katika jitihada za kutafuta watu wengine ambao huenda walikuwa wamenasa.
Waziri aeleza mazingira ya ajali
Waziri wa Uchukuzi, Oscar Puente, amesema mfumo wa kudhibiti treni kiotomatiki ulisimama kufanya kazi katika kipande cha reli chenye urefu wa kilomita 69.
Amesema kituo cha udhibiti kiliamua kuruhusu usafiri kuendelea katika mazingira aliyoyataja kuwa yasiyoelezeka, licha ya kuwa na muda wa kutosha kubaini na kurekebisha hitilafu hiyo.
Kwa mujibu wa waziri huyo, treni ya Renfe ilisafiri takribani kilomita 25 kabla ya kugonga treni ya Iryo.
Hata hivyo, uchunguzi unahitajika kubaini kwa kina mazingira yaliyopelekea ajali hiyo na iwapo hitilafu ya mfumo wa udhibiti ilichangia kutokea kwake.
Kutokana na mkasa huo, Serikali ya Hispania imetangaza siku tatu za maombolezo kuanzia Alhamisi, Oktoba 29, 2026.
Ajali hiyo imetokea miezi kadhaa baada ya treni mbili za mwendo kasi kugongana katika eneo la Andalusia, kusini mwa Hispania, Januari mwaka huu, na kusababisha vifo vya watu 46.
Uchunguzi wa ajali hiyo ya awali bado unaendelea.
