Dk Bashiru ataka tafiti, teknolojia kupunguza gharama za ufugaji
3 mins read

Dk Bashiru ataka tafiti, teknolojia kupunguza gharama za ufugaji

Iringa. Matumizi ya tafiti za kisayansi na teknolojia katika sekta ya mifugo yanaweza kuwasaidia wafugaji kupunguza gharama za uzalishaji, kuboresha afya ya mifugo na kuongeza uzalishaji wa maziwa na nyama, imeelezwa.

Hata hivyo, mafanikio ya juhudi hizo yanategemea uwezo wa wataalamu kugeuza matokeo ya tafiti kuwa suluhisho zinazoweza kutumika na wafugaji katika shughuli zao za kila siku.

Hayo yamesemwa jana Jumatano, Oktoba 28, 2026, mkoani Iringa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Bashiru Ally wakati akifungua Mkutano wa 49 wa Mwaka wa Kisayansi na Mkutano Mkuu wa 50 wa Mwaka wa Chama cha Uzalishaji wa Mifugo Tanzania (TSAP).

Dk Bashiru amewataka wataalamu kutumia maarifa ya kisayansi, weledi na maadili ya taaluma zao kuboresha huduma kwa wafugaji na wavuvi, kuongeza uzalishaji na kuimarisha mchango wa sekta hizo katika uchumi wa Taifa.

Amesema matokeo ya tafiti hayapaswi kubaki kwenye maandiko, bali yatumike kutatua changamoto zinazowakabili wananchi na kuleta matokeo yanayoweza kupimika katika uzalishaji.

“Maarifa ya kitaalamu na matokeo ya tafiti yanapaswa kutumika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi na kuleta matokeo yanayopimika katika uzalishaji wa mifugo na mazao ya uvuvi,” amesema.

Kakurwa amesema bado kuna malalamiko kuhusu huduma zinazotolewa na baadhi ya wataalamu, akiwataka kujitathmini na kuwajibika ili kurejesha imani ya wafugaji na wadau wengine.

“Katika kupunguza gharama za uzalishaji, tafiti zinaweza kusaidia kubaini malisho yenye virutubisho vinavyohitajika na yanayopatikana kwa gharama nafuu, kuboresha lishe ya mifugo na kutafuta njia za kuzuia magonjwa kabla hayajasababisha hasara.

“Teknolojia pia inaweza kusaidia kuboresha uhifadhi wa malisho, kufuatilia afya ya mifugo na kukusanya taarifa za uzalishaji, hivyo kuwawezesha wafugaji kufanya maamuzi yanayozingatia gharama na tija.”

Kakurwa amesisitiza kuwa suluhisho hizo zinapaswa kuzingatia uwezo wa kifedha wa wafugaji wadogo, upatikanaji wa huduma za ugani na mazingira wanamofanyia shughuli zao.

Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania, George Msalya amesema mkutano huo unatoa nafasi kwa wataalamu kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto na kuweka mikakati ya kuboresha sekta ya mifugo na uvuvi.

Ofisa Mifugo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Rombo amesisitiza umuhimu wa watafiti kukutana moja kwa moja na wananchi ili kubaini mahitaji yao na kufanya tafiti zinazotoa majibu yanayotekelezeka.

Amesema kuunganisha watafiti na wafugaji kutasaidia kuhakikisha teknolojia zinazobuniwa zinaendana na mazingira halisi ya ufugaji na uwezo wa kifedha wa walengwa.

Mwenyekiti wa TSAP, Zabron Nziku, ameiomba Serikali kuimarisha ushirikiano na chama hicho ili matokeo ya tafiti yatumike kuboresha sera na kutatua changamoto zinazowakabili wafugaji.

Amesema ushirikiano kati ya Serikali, wataalamu na sekta binafsi unaweza kuimarisha upatikanaji wa teknolojia, kuongeza thamani ya bidhaa za mifugo kupitia uchakataji na uhifadhi, pamoja na kuboresha upatikanaji wa masoko.

Mkutano huo pia umewakutanisha wadau wa sekta ya umma na binafsi, wakiwamo Asas Dairies na INADES-Formation Tanzania, kwa kushirikiana na Brooke East Africa, kujadili tafiti, ubunifu na mikakati ya kuendeleza sekta hizo.

Kakurwa amesema Serikali inalenga kuhakikisha Tanzania inafikia utoshelevu wa protini inayotokana na nyama, maziwa, mayai na samaki kabla ya mwaka 2050.

Ameitaka TSAP kuimarisha weledi wa wanachama wake na kuhimiza matumizi ya tafiti, teknolojia na ubunifu katika kuboresha afya na lishe ya mifugo, uhifadhi wa malisho na uzalishaji.

Pia, amewataka wataalamu kujifunza kutokana na uzoefu wa Iringa katika tasnia ya maziwa na kujiandaa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wao, wafugaji mkoani Iringa wamesema teknolojia na tafiti zinaweza kuongeza tija iwapo matokeo yake yatawafikia na kuzingatia changamoto wanazokutana nazo kila siku.

Mfugaji Joshua Sinde amesema upatikanaji wa elimu ya kisasa ya ufugaji na teknolojia zinazomudu uwezo wa kifedha wa wafugaji ni muhimu katika kuboresha usimamizi wa mifugo na kuongeza uzalishaji.

Amesema ushirikiano kati ya wafugaji, watafiti na maofisa ugani unaweza kusaidia kupata suluhisho zinazolingana na mazingira halisi ya ufugaji.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *