BoT yasisitiza Vicoba, watoa huduma za fedha kujisajili
Mbeya. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imevitaka vikundi vya kuweka na kukopa (Vicoba) na watoa huduma nyingine za kifedha kuhakikisha wanasajiliwa na kufuata matakwa ya sheria, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha usimamizi wa sekta hiyo na kulinda wananchi dhidi ya huduma zinazoweza kuwaumiza kiuchumi.
Hatua hiyo inakuja wakati vikundi 100,000 vikiwa vimeingizwa kwenye mfumo nchini, huku BoT ikiendelea kutoa elimu kwa kushirikiana na halmashauri ili kuhakikisha huduma ndogo za kifedha zinaendeshwa kwa uwazi na kwa kufuata taratibu zilizowekwa.
Ofisa Mwandamizi Daraja la Kwanza wa BoT, Robert Mshiu amesema usajili wa vikundi hivyo unalenga kuhakikisha shughuli zao zinatambulika kisheria na kuweka utaratibu unaowawezesha wanachama kufahamu haki zao na mahali pa kuwasilisha malalamiko wanapokumbana na changamoto.
Amesema halmashauri, kupitia maofisa maendeleo ya jamii, zina jukumu la kusaidia mchakato wa kuingiza vikundi hivyo kwenye mfumo ili viweze kusimamiwa kwa mujibu wa sheria.
“Sheria iliyotungwa na Bunge inataka huduma ndogo za kifedha zitolewe kwa kufuata utaratibu rasmi badala ya kufanyika kiholela. Hii itasaidia wanaopata huduma kujua mahali pa kulalamikia wanapokumbana na changamoto,” amesema.
Ofisa Sarafu Benki Kuu ya Tanzania (BOT),Tawi la Mbeya, Kingson Baraka akitoa ufafanuzi kuhusuana na athari ya matumizi holela ya fedha za noti kwa kuhifadhi maeneo yasiyo sahihi na kuisababisha Serikali hasara. Picha na Hawa Mathias
Mshiu amesema BoT imetoa mwongozo kwa halmashauri kuhusu taarifa zinazopaswa kukusanywa kutoka kwenye vikundi hivyo, zikiwemo majina ya vikundi, michango ya wanachama na taratibu za uwekaji akiba.
Amesema taarifa hizi zitasaidia kubaini vikundi vinavyoendeshwa kwa kuimarisha uwazi katika masharti ya mikopo na uwekaji akiba, pamoja na kuipa BoT takwimu zitakazosaidia kuboresha sera za kifedha.
Amesisitiza kuwa vikundi vinavyotoa huduma za kifedha vinapaswa kutimiza matakwa ya sheria, ikiwemo kujisajili na kupata leseni pale inapohitajika, akionya kuwa wanaokiuka masharti wanaweza kuchukuliwa hatua za kisheria.
Waonya mikopo kausha damu
Kwa upande wake, Ofisa wa BoT, Francis Angesisye amewaonya wananchi wanaoanzisha na kuendesha huduma za kifedha bila kufuata taratibu za kisheria, akisema ni muhimu kuhakikisha shughuli hizo zinasimamiwa kwa mujibu wa sheria ili kulinda wateja.
Amesema watoa huduma za kifedha wanapaswa kuzingatia masharti yanayotakiwa katika uendeshaji wa shughuli zao, huku akisisitiza umuhimu wa kudhibiti vitendo vinavyoweza kuwaweka wananchi katika mazingira magumu ya kifedha, ikiwemo mikopo kausha damu.
“Tunatoa rai kwa wananchi wanaotaka kuanzisha huduma za kifedha kuhakikisha zinaendeshwa kwa kufuata sheria. Wanaofanya shughuli hizo bila kufuata taratibu wanakiuka sheria na wanaweza kukabiliwa na faini au vifungo watakapobainika,” amesema.
Angesisye amewataka wananchi wanaotaka kuingia katika biashara ya huduma za kifedha kutafuta elimu kuhusu masharti ya usajili na uendeshaji, akisema kufuata sheria kutasaidia kulinda maslahi ya wateja na kuimarisha uwajibikaji katika sekta hiyo.
Katika hatua nyingine, BoT imeonya kuhusu tabia ya kuhifadhi noti kwenye maziwa, soksi na kuzifunga ndani ya kanga, ikisema utunzaji huo unaweza kuchangia kuharibika kwa fedha kabla ya muda wake na kuongeza gharama za Serikali za kuchapisha noti nyingine.
Ofisa wa Benki Kuu ya Tanzania(BOT),Francis Angesisye anayesimama masuala ya huduma za kifedha zikiwepo Saccos, vikoba akieleza umuhimu wa kutumia mfumo maalumu wa kujisajili na kuweka taarifa zao.Picha na Hawa Mathias
Mkuu wa Kitengo cha Sarafu wa BoT, Kingson Baraka amesema noti zinapoharibika kutokana na utunzaji usiofaa zinaweza kushindwa kupita kwenye mashine na kuondolewa kwenye mzunguko wa matumizi kwa kufuata taratibu zilizowekwa.
Akizungumza na Mwananchi katika Banda la BoT, kwenye Maonyesho ya Biashara na Uwekezaji Kusini (KITF), katika Viwanja vya Shule ya Msingi Gombe, amesema kila noti inayoingizwa kwenye mzunguko ina gharama za uzalishaji, hivyo kuharibika mapema kunaweza kuilazimu Serikali kutumia fedha nyingine kuchapisha .
“Utunzaji mbaya wa fedha una hasara kubwa kwa Serikali kwa sababu noti ikiharibika kabla ya muda wake, inapofika kwenye mashine za BoT inaweza kukataliwa na kuondolewa kwenye mzunguko, hivyo kulazimika kuchapisha fedha nyingine,” amesema.
Baraka amesema baadhi ya wananchi wamekuwa na mazoea ya kuweka kwenye maziwa, soksi , kuzifunga ndani ya kanga na kutumia vibubu visivyofaa kuwa njia zinazoweza kuchangia noti kukunjamana, kuchakaa na kuharibika.
Amesema BoT inaendelea kutoa elimu kuhusu utunzaji sahihi wa fedha ili kupunguza uharibifu wa noti na gharama zinazoweza kuepukika sambamba na kuchukua hatua kwa watao bainika.
Katika hatua nyinyine amewahimiza wananchi kutumia taasisi rasmi za kifedha kuweka akiba zao ili kujilinda dhidi ya majanga kama moto na mafuriko ikiwepo kuachana na dhana na kufika maeneo yasiyo rasmi.
Naye, Mwenyekiti wa maandalizi ya maonyesho ya KITF, Ibrahim Mangula amesema elimu ya huduma kifedha ni nyenzo muhimu kwa jamii wakuwepo wafanyabiashara wadogo hususani mbogamboga na matunda kujua namna bora ya uhifadhi wa fedha.
“Asilimia kubwa wapo wanao hifadhi kwenye maziwa,kanga kuona kama ni sehemu sahihi hivyo ni vyema kufika katika banda ya BoT kupata elimu bora ili kupwepa mkono wa sheria,” amesema.
