Maonyesho ya Sido yafungua soko kwa wajasiriamali
3 mins read

Maonyesho ya Sido yafungua soko kwa wajasiriamali

Kahama. Maonyesho ya Tano ya Kitaifa ya Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (Sido) yanayoendelea wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, yameendelea kuwa fursa kwa wajasiriamali wadogo na wa kati kutoka ndani na nje ya nchi kutangaza bidhaa zao na kutafuta masoko.

Maonyesho hayo yanayofanyika katika Viwanja vya Magufuli yamewakutanisha wazalishaji na wanunuzi katika eneo moja, yakitoa nafasi kwa wajasiriamali kuonyesha bidhaa zinazozalishwa nchini, kubadilishana uzoefu na kuonesha matumizi ya teknolojia katika kukuza viwanda vidogo.

Washiriki kutoka maeneo mbalimbali wamejitokeza kutembelea viwanja hivyo, ambako wanapata fursa ya kuona bidhaa tofauti, kuzilinganisha na kufanya manunuzi.

Miongoni mwa washiriki ni Kasimbagu Kacha, mbunifu wa mapambo yanayotengenezwa kwa kutumia magamba ya viumbe wa baharini, aliyesafiri kutoka Dar es Salaam kushiriki maonyesho hayo kwa lengo la kutangaza bidhaa zake na kutafuta fursa za masoko.

Kacha ni miongoni mwa wajasiriamali wanaoongeza thamani ya malighafi za asili kwa kuzibadilisha kuwa bidhaa za mapambo, zikiwemo mikufu, bangili, mapambo ya picha, fremu na vishikio vya funguo.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Oktoba 23, 2026, amesema alianza kwa kukusanya magamba ya viumbe wa baharini na kujaribu kuyatumia kutengeneza mapambo, kabla ya kupanua wigo wa bidhaa zake na kupata fursa za kushiriki maonesho mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Kacha, maonyesho ya Sido ni jukwaa muhimu kwa wajasiriamali kwa kuwa yanawawezesha kutambulisha bidhaa zao, kukutana na wateja wapya na kujifunza kutoka kwa wabunifu wengine.

“Maonyesho kama haya ya Sido ndiyo anuani yetu ya utambulisho. Mimi nikiwa hapa sasa hivi watu wengi wamenijua kwa sababu nipo hapa, lakini ningekuwa Dar es Salaam wasingenijua,” amesema.

Amesema jukwaa hilo ni muhimu kwa wajasiriamali wanaoziamini bidhaa zao, kwa kuwa linawapa nafasi ya kuonesha namna ubunifu unavyoweza kugeuza malighafi za asili kuwa bidhaa zenye thamani ya kibiashara.

Kwa upande wake, Wambi Ibrahim aliyefika katika maonesho hayo kununua bidhaa mbalimbali, amesema yamewawezesha wananchi wa Kahama kupata bidhaa anazozitaja kuwa bora na za bei nafuu, bila kulazimika kuagiza kila kitu kutoka Dar es Salaam.

“Ninashukuru sana Serikali kwa kutuletea maonesho ya Sido hapa Kahama. Tunapata bidhaa nzuri kwa bei nafuu. Kuna nguo kama hizi ambazo Kahama tulikuwa hatuzipati, tunaagiza Dar es Salaam,” amesema.

Ibrahim ameishauri Sido kuandaa maonesho ya aina hiyo mara nyingi zaidi kwa mwaka na kuyapeleka katika maeneo mbalimbali ya nchi ili kuongeza fursa za masoko kwa wajasiriamali.

“Ningeomba kama inawezekana, Sido isisubiri maonesho ya kitaifa mara moja kwa mwaka. Iandae maonesho kama haya walau hata mara tano kwa mwaka yafanyike kikanda, ili wajasiriamali wapate fursa ya kukua zaidi,” amesema.

Amewahimiza wananchi ambao bado hawajatembelea viwanja hivyo kutumia nafasi hiyo kujionea bidhaa zinazotengenezwa na wajasiriamali wa ndani ya Tanzania.

“Kwa wateja ambao hawajafika kwenye viwanja hivi, wanakosa mambo mengi. Hapa unapata bidhaa tofauti na nzuri zilizotengenezwa na wajasiriamali wa ndani ya Tanzania. Waje, bidhaa zipo,” ameongeza.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *