Marekani yafuta picha mkutano wa G-20, Afrika Kusini yakosa mwaliko
4 mins read

Marekani yafuta picha mkutano wa G-20, Afrika Kusini yakosa mwaliko

Dar es Salaam. Mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa kundi la nchi 20 zenye uchumi mkubwa duniani (G-20) umeingia katika mvutano wa kidiplomasia baada ya Marekani kufuta picha ya pamoja iliyokuwa imepangwa kufungua mkutano huo, kufuatia upinzani wa nchi kadhaa kushiriki picha moja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergei Lavrov.

Hatua hiyo iliyochukuliwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, mjini Atlanta, Georgia, Oktoba 30, 2026, inadhihirisha mgawanyiko wa kimataifa kuhusu vita vya Ukraine na namna ya kuishughulikia Russia, huku mvutano mwingine ukizuka kutokana na uamuzi wa utawala wa Rais Donald Trump kutoialika Afrika Kusini kwenye shughuli za G-20 mwaka huu.

Marekani ilifuta picha hiyo baada ya wajumbe kadhaa, wakiwemo kutoka Uingereza, Australia na nchi za Umoja wa Ulaya, kuonyesha kutokuwa tayari kupigwa picha pamoja na Lavrov.

Mwanadiplomasia wa Magharibi alinukuliwa akisema takribani theluthi moja ya washiriki walikuwa wameonyesha kupinga kushiriki picha hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari vya kimataifa, Washington iliamua kuondoa kipengele hicho kwenye ratiba ili kuepusha shughuli ya kawaida ya kidiplomasia kugeuka kitovu cha mabishano na kufunika ajenda kuu ya mkutano.

Sababu kuu ni vita vya Ukraine vilivyoanza baada ya Russia kuivamia nchi hiyo kwa kiwango kikubwa Februari 2022, hatua iliyozua upinzani kutoka kwa mataifa mengi ya Magharibi na kusababisha vikwazo dhidi ya Moscow.

Nchi zilizopinga picha hiyo zinaona kuwa kushiriki picha rasmi pamoja na mwakilishi wa Russia katika mazingira ya sasa kunaweza kutafsiriwa kama ishara ya kurejea kwa mahusiano ya kawaida, licha ya kutokuwepo kwa suluhu ya vita vya Ukraine.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Johann Wadephul, alieleza msimamo huo akisema hakutakuwa na picha ya pamoja ya washirika wa Ulaya na Lavrov kwa sababu, kwa mtazamo wao hakuna hali ya kawaida katika mahusiano na Russia.

Kwa upande wa Uingereza, Waziri wa Mambo ya Nje, Ed Miliband, alisisitiza kuwa nchi yake haitabadilisha msimamo wake wa kutoshiriki shughuli za aina hiyo na maofisa wa Russia, sera ambayo London imekuwa ikiifuata tangu uvamizi wa Ukraine.

Australia nayo iliunga mkono kufutwa kwa picha hiyo. Waziri wake wa Mambo ya Nje, Penny Wong, alikosoa uvamizi wa Russia, akiuelezea kuwa wa kikatili na usio na uhalali, huku akieleza kuwa vita hivyo vinaathiri masoko ya kimataifa na kuongeza changamoto za usalama wa chakula.

Kwa nini Afrika Kusini haikualikwa?

Wakati mzozo kuhusu Russia ukiendelea, uamuzi mwingine ulioibua mjadala ni wa Marekani kutomwalika Afrika Kusini kwenye mkutano wa G-20 chini ya uenyekiti wake wa mwaka 2026.

Afrika Kusini ni mwanachama mwanzilishi wa G-20 na ndiyo nchi pekee ya Afrika iliyokuwa mwanachama wa kundi hilo kabla ya Umoja wa Afrika kujiunga.

Kutokuwepo kwake katika mkutano wa Atlanta kumeibua maswali kuhusu uhusiano wa Washington na Pretoria, pamoja na nafasi ya bara la Afrika katika majadiliano ya uchumi wa dunia.

Sababu muhimu ya kuelewa uamuzi huo ni mvutano wa muda mrefu kati ya Rais Trump na serikali ya Rais Cyril Ramaphosa.

Mvutano huo uliongezeka wakati wa uenyekiti wa Afrika Kusini wa G-20 mwaka 2025, ambapo Trump na maofisa wakuu wa Marekani, akiwemo Rubio, walisusia mikutano kadhaa iliyoandaliwa na Pretoria.

Trump amekuwa akiikosoa Afrika Kusini kuhusu sera zake za ndani, ikiwemo masuala ya umiliki wa ardhi na madai kuhusu namna raia weupe wanavyotendewa nchini humo.

Serikali ya Afrika Kusini imekataa madai hayo, ikiyataja kuwa ya uongo na yenye kupotosha.

Mwishoni mwa Novemba 2025, Trump alitangaza kuwa Afrika Kusini haitaalikwa kushiriki G-20 nchini Marekani mwaka 2026.

Serikali ya Pretoria ilipinga hatua hiyo, ikisisitiza kuwa uanachama wake unatokana na hadhi yake ndani ya kundi hilo, si mwaliko wa nchi inayokuwa mwenyeji.

Katika taarifa yake, Rais Ramaphosa alisema Afrika Kusini ni mwanachama mwanzilishi wa G-20 na ina haki ya kushiriki kama mwanachama kamili.

Alieleza pia kuwa nchi hiyo itaendelea kutafuta mazungumzo na Marekani kwa misingi ya kuheshimiana.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *