Mvua ya mawe yabomoa nyumba zaidi ya 70 Kigoma, wananchi wakosa makazi
Kigoma. Zaidi ya nyumba 70 za makazi pamoja na makanisa mawili zimeezuliwa na kubomolewa na mvua ya mawe iliyoambatana na upepo mkali iliyonyesha katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, na kuwaacha baadhi ya wananchi bila makazi, chakula na mahitaji muhimu ya kibinadamu.
Wananchi walioathirika wameiomba Serikali na wadau mbalimbali kujitokeza kuwasaidia, wakieleza kuwa uharibifu huo umewaweka katika mazingira magumu, hasa familia zenye watoto ambazo hazina sehemu salama za kuishi.
Mvua hizo zilinyesha kwa nyakati tofauti, ikiwamo Alhamisi Oktoba 29, 2026, kuanzia jioni na kuendelea Ijumaa Oktoba 30 saa 6:30 mchana, ambapo upepo mkali na mawe viliongeza ukubwa wa athari.
Akizungumza kuhusu hali hiyo kupitia taarifa iliyotolewa Oktoba 30, 2026, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kigoma, Rusajo Mboli, amesema kikosi chake kilitembelea maeneo yote yaliyoathirika na kutoa msaada wa dharura kwa waathirika, huku tathmini ya kina ikiendelea kubaini ukubwa wa uharibifu.
Amesema tathmini ya awali imebaini kuwa nyumba 70 za makazi na makanisa mawili zimeezuliwa na upepo mkali.
“Miongoni mwa madhara yaliyotokea, nyumba nyingi ziliezuliwa na upepo. Nyumba zilizoezuliwa ni 70 za makazi, lakini nyumba mbili ni za ibada ambazo ni makanisa, nazo pia ziliezuliwa na upepo,” amesema.
Ameeleza kuwa maeneo yaliyoathirika zaidi ni Mtaa wa Gezaulole, ambako nyumba 30 zimeezuliwa, Mwenye nyumba 14, Masanga nyumba 14 na Kikunku nyumba tisa, huku makanisa mawili yakitajwa pia kuathirika.
Baadhi ya nyumba zilizoezuliwa na mvua ya upepo katika maeneo tofauti ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Katika tukio hilo, watu wawili walijeruhiwa na kwa sasa wanaendelea kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma Maweni.
Baadhi ya wananchi wa maeneo ya Masanga, Gungu na Kikunku wamesema mvua hizo zimeathiri maisha yao ya kila siku, huku wengine wakilazimika kuhama makazi yao na kwenda kuishi kwa ndugu na jamaa baada ya nyumba zao kuharibika.
Mkazi wa Kikunku, Juma Mfaume, amesema upepo mkali ulioambatana na mvua hizo umemlazimu kumhamisha mama yake kutoka nyumbani kwake na kumpeleka kwake ili kuhakikisha anakuwa katika mazingira salama.
Jengo la Kanisa la Waadventista Wasabato Nyamnyusi Halimashauri ya Wilaya ya Kasulu pamoja na madarasa shule ya msingi Kisuma ambayo pia yaliathiriwa na mvua ya Oktoba 28, 2026.
“Mvua hizi zimetuathiri kwa sababu zimekuja kwa upepo mkali na hapa nilipo ni kwa mama yangu, kwa sasa nimelazimika kumpeleka kwangu,” amesema.
Kwa upande wake, January Gervas, mkazi wa Masanga, amesema familia yake haina mahali pa kwenda baada ya nyumba yao kuathiriwa na mvua hizo, hali inayowapa hofu kuhusu mahali watakapopata hifadhi, hasa kwa kuzingatia uwepo wa watoto wachanga.
“Hatuna pa kwenda, tunafikiria tutalala wapi na tutapeleka wapi familia. Serikali ituangalie kwa jicho la huruma iweze kutusaidia, kwa sababu tuna watoto wadogo, wachanga hatuna pa kuwapeleka,” amesema.
Naye Hassan Ibrahim, mkazi wa Gungu, amesema athari hizo zimeongeza ugumu wa maisha kwa familia yake kutokana na nyumba kuwa sehemu ya makazi na shughuli zao za kiuchumi, ikiwamo ufugaji.
“Changamoto zilizotukuta sisi ni kubwa, kwa sababu hapa nyumbani tuna mifugo, tunaishi hapa hapa. Mpaka sasa hatujajua kwamba tunafanya nini kutokana na uchumi unakaba,” amesema.
Jengo la Kanisa la Waadventista Wasabato Nyamnyusi Halimashauri ya Wilaya ya Kasulu pamoja na madarasa shule ya msingi Kisuma ambayo pia yaliathiriwa na mvua ya Oktoba 28, 2026.
Akizungumzia hali ya waathirika, Mwenyekiti wa Mtaa wa Masanga, James Samwel, amesema mvua hizo zimesababisha baadhi ya nyumba kuanguka na kuwataka viongozi wa Serikali kuharakisha hatua za kuwasaidia wananchi walioathirika.
Amesema Serikali tayari imetenga fedha kwa ajili ya kukabiliana na majanga, hivyo ameiomba kuhakikisha wananchi waliopoteza makazi na mali wanapata msaada unaostahili.
“Kulingana na mvua ambayo imenyesha, hali si nzuri, imeleta athari kubwa, nyumba zimeanguka. Niombe Serikali, kwa kuwa imeshatenga fedha kwa ajili ya majanga haya, wananchi waweze kusaidiwa, kwa sababu wakati mwingine mtu anakuwa hana chochote ndani,” amesema.
Hata hivyo, athari za mvua zinazoendelea kunyesha zimekuwa zikijitokeza pia katika maeneo mengine ya Mkoa wa Kigoma tangu kuanza kwa msimu huu.
Oktoba 28, 2026, mvua iliyonyesha katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu ilisababisha nyumba 11 kuanguka, huku madarasa matatu ya Shule ya Msingi Kisuma, iliyopo Kata ya Nyamnyusi, yakiezuliwa. Aidha, kanisa la Waadventista Wasabato lililopo Nyamnyusi liliripotiwa kuanguka.

