Nondo amwangukia Ndejembi kuhusu bayoteknolojia
Dar es Salaam. Ngome ya Vijana ya ACT-Wazalendo imeshauri Serikali kuunda bodi ya kitaaluma ya bayoteknolojia na kuboresha mitaala ya vyuo vikuu ili kuendana na mahitaji ya sekta za afya, kilimo na viwanda.
Mwenyekiti wa ngome hiyo, Abdul Nondo, amesema chama hicho kinapanga kuwasilisha mapendekezo hayo katika Ofisi ya Makamu wa Rais, inayoongozwa na Makamu wa Rais Deogratius Ndejembi, huku kikiomba kukutana naye kujadili mustakabali wa taaluma hiyo nchini.
Akizungumza katika Makao Makuu ya ACT-Wazalendo, Magomeni, Dar es Salaam, leo Alhamisi Oktoba 22, 2026, Nondo amesema nakala ya barua ya mapendekezo hayo pia itapelekwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa suala hilo linahitaji uamuzi wa kisera na uratibu wa Serikali.
“Bayoteknolojia si tishio, bali ni fursa ya kulinda afya, kuongeza tija ya kilimo na viwanda na kuimarisha usalama wa taifa,” amesema Nondo.
Amesema hatua ya kwanza inayopaswa kuchukuliwa ni kuanzisha bodi ya kitaaluma ya bayoteknolojia chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais, ikiwa na vitengo vinavyosimamia maeneo ya afya ya binadamu, kilimo na viwanda.
Kwa mujibu wa Nondo, bodi hiyo itakuwa na jukumu la kusajili wataalamu wenye sifa, kutoa leseni, kusimamia maadili na nidhamu ya kitaaluma, pamoja na kuishauri Serikali kuhusu mahitaji ya wataalamu na maendeleo ya kada hiyo.
Amesema kutokuwepo kwa chombo hicho kunawaacha wahitimu bila mfumo maalumu wa utambuzi na usimamizi wa kitaaluma, hali inayoweza kuwanyima fursa za ajira katika taasisi za umma na sekta binafsi.
Nondo amesema Tanzania imekuwa ikizalisha wataalamu wa bayoteknolojia tangu mwaka 2001, programu hiyo ilipoanzishwa katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
Vyuo vingine vilivyoanzisha programu zinazohusiana na bayoteknolojia ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Hata hivyo, amesema baadhi ya programu hizo zimekuwa zikifundisha maeneo mengi ya bayoteknolojia kwa pamoja, hali inayofanya iwe vigumu kubainisha utaalamu mahususi wa wahitimu na kuandaa mifumo inayotambua maeneo yao ya ajira.
Ili kukabiliana na changamoto hiyo, Ngome ya Vijana ya ACT-Wazalendo imependekeza Serikali ipitie upya mitaala ya vyuo vikuu na kugawa programu za bayoteknolojia katika maeneo ya afya ya binadamu, kilimo na viwanda.
Ngome hiyo imeitaja UDSM kuwa mfano wa kuigwa kwa kutenganisha programu hizo katika maeneo maalumu ya kitaaluma, ikipendekeza vyuo vingine kuchukua hatua zinazofanana kwa kuzingatia mahitaji ya nchi.
Nondo amesema katika sekta ya afya, bayoteknolojia inaweza kutumika kufanya utafiti wa magonjwa, kuchunguza vimelea, kufuatilia milipuko ya magonjwa na kufanya utafiti wa dawa na chanjo.
Katika kilimo, amesema taaluma hiyo inaweza kusaidia kuboresha mbegu, kutambua magonjwa ya mimea na kuongeza tija ya uzalishaji, huku katika viwanda wataalamu wakishiriki kudhibiti ubora wa bidhaa na kutumia viumbe hai katika michakato ya uzalishaji.
Kwa mujibu wa mapendekezo hayo, Sera ya Taifa ya Bayoteknolojia ya mwaka 2010 inalenga kuiwezesha Tanzania kunufaika na taaluma hiyo katika afya, kilimo, viwanda na mazingira, huku ikilinda usalama wa jamii na mazingira.
Ngome hiyo pia imehusisha mapendekezo yake na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, ikisema dira hiyo inatambua umuhimu wa sayansi na teknolojia katika kuongeza ufanisi na tija katika sekta muhimu za uchumi.

