RC James aeleza nafasi ya wauguzi katika jamii
2 mins read

RC James aeleza nafasi ya wauguzi katika jamii

Iringa. Wakati wagonjwa wanapokabiliwa na maumivu, hofu na nyakati ngumu za kiafya, wauguzi ni miongoni mwa watoa huduma wanaokutana nao katika hatua mbalimbali za maisha yao, hali inayoonesha nafasi muhimu ya kada hiyo katika jamii.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amesema wauguzi ni watu muhimu katika maisha ya binadamu kutokana na nafasi yao katika kumhudumia mtu kuanzia anapozaliwa hadi anapofariki.

James amesema hayo usiku wa kuamkia Oktoba 26, 2026, wakati akizungumza katika usiku wa heshima wa wauguzi ulioandaliwa na waandishi wa habari wanawake mkoani Iringa, uliofanyika katika ukumbi wa Royal Palm.

“Mwanadamu yeyote anapozaliwa yaani kuingia dunia lazima akutane na muuguzi na pia anavyotoka duniani yaani kufariki lazima akutane na muuguzi hivyo tuwaheshemu,” amesema James.

Ofisa Muuguzi Mkuu Mkoa wa Iringa, Moses Tawete, akizungumza katika Usiku wa Wauguzi Gala 2026 uliofanyika Iringa. Picha na Wauguzi Gala.

Ofisa Muuguzi wa Mkoa wa Iringa, Moses Tawete amesema wauguzi ni watoa huduma wanaopaswa kupewa faraja na heshima kutokana na majukumu yao ya kuwahudumia wananchi.

Amesema umuhimu wa kada hiyo unapaswa kuambatana na kutambuliwa kwa mchango wao, ili wauguzi waone kuwa kazi wanayoifanya kwa jamii inathaminiwa.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Waandaaji wa Wauguzi Gala, Tukuswiga Mwaisumbe amesema waliandaa hafla hiyo kwa lengo la kutambua na kuthamini mchango wa wauguzi katika jamii.

Amesema hafla hiyo ilikuwa na nafasi ya kuwakutanisha wauguzi katika mazingira ya heshima na kuonesha kutambua kazi wanayoifanya katika kuwahudumia wananchi.

Mwaisumbe amesema kaulimbiu ya hafla hiyo ilikuwa “Wauguzi tunao na tunatamba nao,” ikiwa na lengo la kuonesha umuhimu wa wauguzi na nafasi yao katika jamii.

Mwenyekiti wa Kamati ya Wauguzi Gala 2026, Tukuswiga Mwaisumbe, akizungumza katika hafla ya Wauguzi Gala iliyofanyika Iringa. Picha na Wauguzi Gala.

Hafla hiyo iliyofanyika Iringa iliwakutanisha wauguzi zaidi ya 200 kutoka hospitali na vituo vya afya mbalimbali mkoani Iringa kwa ajili ya usiku wa heshima uliolenga kutambua mchango wao.

Wakizungumza na Mwananchi Digital leo, Oktoba 26, 2026, wananchi mkoani Iringa wamesema wauguzi wana nafasi muhimu katika jamii kutokana na huduma wanazotoa kwa wagonjwa, zikiwemo kuwafariji na kuwapa msaada wanapopitia hali ngumu za kiafya.

Aidha, wananchi hao wamepongeza kufanyika kwa Wauguzi Gala, wakieleza kuwa hafla hiyo ni fursa ya kutambua na kuthamini mchango wa wauguzi katika kuwahudumia wananchi.

Naye Sophia Mpunga kutoka mkoani Iringa ameeleza jinsi wauguzi wanavyoweza kuwa kama wazazi kwa wagonjwa waliolazwa hospitalini, akisimulia namna alivyopata msaada wa muuguzi baada ya kumpoteza mama yake mzazi.

“Mimi nililazwa nikiwa mjamzito, baada ya siku nne kujifungua mama yangu mzazi alifariki, ila muuguzi mmoja alihakikisha ninakuwa salama na aligeuka kuwa mzazi kwangu kweli,” amesema Sophia.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *