Serikali yakana kuwalazimisha Machinga kuhamia eneo jipya
Dodoma. Halmashauri ya Jiji la Dodoma imekanusha kuwahamisha wafanyabiashara wadogo (Machinga) kutoka eneo la One Way kwenda Dodoma Inn kama ilivyoelezwa na wafanyabiashara hao siku ya jana.
Ufafanuzi huo unakuja kufuatia malalamiko yaliotolewa na wafanyabishara hao siku ya jana Ijumaa, 23, Agosti 2026 wakidai kuwa Halmashauri ya Jiji hilo imewafukuza katika eneo la One Way na kwenda Dodoma Inn ambapo walieleza kutokubaliana na uamuzi huo wakidai kuwa eneo hilo si rafiki kwa aina ya biashara zao.
Wafanyabiashara hao walienda mbali zaidi na kueleza kuwa eneo hilo lipo nje ya mji na ni njia ya magari makubwa yanayoenda mikoani, lakini pia halina miundombinu rafiki itakayowawezesha kufanya shughuli zao wakati wa mvua.
Akizungumzia malalamiko hayo leo Jumamosi, Oktoba, 24, 2026 Ofisa habari wa Jiji la Dodoma, Denis Gondwe amesema wafanyabiashara hao hajalazimishwa kuhama bali walielkezwa kwenda kuliangalia eneo hilo kama linawafaa ili kurudisha mapendekezo kwa serikali kuhusu maboresho au mapendekezo walionayo.
“Tulikubaliana na viongozi wa wafanyabiashara kwenda kulitembelea eneo hilo kabla ya kuhamia na wakatushauri ni vema zaidi wakaenda na wafanyabishara hao ili kama kuna mapendekezo wayalete kwetu ili tuyafanyie kazi kwa sababu tunatatua changamoto ya muda mfupi,” amesema Gondwe.
“Sisi Halmashauri tulikuwa tunatarajia kuwa jana walivyoenda kwenye lile eneo watakaa watatuambia mapungufu waliyoyaona watakuja kuonana na halmashauri, ila bado hawajafika,” ameongeza.
Gondwe amesema mchakato wote wa uhamishwaji wa wafanyabiashara hao umefanywa kwa ushirikiano baina ya Halmashauri ya Jiji na uongozi wa Machinga ngazi ya Mkoa kupitia vikao vilivyofanyika tangu mwezi wa tisa.
Baadhi ya askari polisi wenye silaha wakiimarisha ulinzi katika eneo la Jamatini Jijini Dodoma ambapo machinga walitaka kugawana maeneo ya kufanyia biashara.
Mwenyekiti wa Machinga Mkoa wa Dodoma, Christian Msumari, ameawaagiza machinga hao kuendelea kuwa watulivu na kuacha kujitokeza katika maeneo ambayo hawajaelekezwa kufika ili kupatiwa kwa ajili ya biashara.
Msumari ameongeza kuwa, wanafanyia kazi mapendekezo ya wafanyabiashara hao kuhusu kupatiwa eneo la Stendi ya Mkoa wa Dodoma ya zamani ambalo linamilikiwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa kuandika barua ya maombi kwa shirika hilo.
Kwa upande wake mfanyabiashara mdogo, Manguchwami Majuto ameiomba serikali kuharakakisha mchakato wa kuwapatia eneo la kufanyia biashara zao kwa muda ili kuondoa taharuki na misuguano baina ya serikali na wafanyabiashara hao.
Machungwami amesema hatua hiyo itawaondolea changamoto ya kufanya biashara kwa kujificha ili kuwakwepa maaskari na mgambo kama ilivyo sasa.
