TMA yasisitiza uwepo wa Elnino
4 mins read

TMA yasisitiza uwepo wa Elnino

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Ladslaus Chang’a, amewataka wananchi kuendelea kufuatilia utabiri wa hali ya hewa na kuuzingatia, huku akisisitiza umuhimu wa kufuata maelekezo ya Serikali ili kulinda maisha na mali.

Amesema wananchi wanapaswa kuendelea na shughuli zao za kiuchumi na kijamii, lakini wakizingatia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na mamlaka hiyo ili kupunguza hatari zinazoweza kujitokeza.

Dk Chang’a ameyasema hayo leo Jumatano, Oktoba 21, 2026, aliposhiriki mjadala wa Mwananchi Space ulioandaliwa na Mwananchi Communications Limited (MCL), wenye mada “Uwepo wa mvua za El Nino, nini kifanyike kujihadhari na athari zake?”

 “Ni muhimu kuendelea na shughuli zetu za kiuchumi na kijamii, lakini kwa kuzingatia taarifa ambazo tumetoa kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa,” amesema Dk Chang’a.

Amesisitiza kufuatilia taarifa hizo pamoja na kuzingatia maelekezo yanayotolewa na viongozi wa Serikali kutasaidia kulinda maisha na mali, kuongeza usalama na kuboresha ufanisi katika shughuli za kila siku.

Amesema wananchi wanapaswa kuepuka kufanya shughuli bila kuzingatia taarifa za hali ya hewa, hasa pale zinapotolewa tahadhari zinazoweza kuathiri shughuli za kijamii na kiuchumi.

Katika mjadala huo ulioanza saa 9 alasiri, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limesema limejiandaa kukabiliana na mafuriko yanayoweza kusababishwa na mvua za El Nino, likiwataka wananchi kupiga namba ya dharura 114 wanapokumbana na hatari inayohitaji uokoaji.

Msemaji wa jeshi hilo, Puyo Nzalayaimisi amesema maandalizi hayo yanahusisha kuimarisha uwezo wa kutoa huduma za uokoaji na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kujikinga na kukabiliana na majanga.

Amesema jeshi hilo pia lina wataalamu wa utafutaji na uokoaji wanaoweza kushughulikia matukio ya watu kupotea majini au kukwama katika maeneo mengine yenye hatari.

Amesema lina vifaa mbalimbali vinavyotumika katika shughuli za uokoaji, ikiwemo boti ndogo zinazoweza kupita katika maeneo yaliyokumbwa na mafuriko, kamba maalumu za uokoaji na maboya yanayosaidia watu waliozingirwa na maji.

Kwa mujibu wa Nzalayaimisi, namba hizo hutumika kuwafikia na kuwavuta watu waliozingirwa na maji, huku maboya na jaketi za kujiokoa zikisaidia kuimarisha usalama wa wahanga wakati wa operesheni za uokoaji.

Mbali na magari ya kuzima moto, Nzalayaimisi amesema jeshi lina magari maalumu yenye vifaa vinavyotumika katika shughuli za uokoaji wakati wa majanga mbalimbali.

“Wananchi wengi wanatambua magari yetu kama magari ya kuzima moto pekee, lakini tuna magari maalumu ya uokoaji yenye vifaa vinavyotumika katika shughuli hizo,” amesema.

Amesema jeshi limeelekeza nguvu kazi na maofisa wake katika maeneo yanayotambuliwa kuwa katika hatari ya kukumbwa na mafuriko, kwa kuzingatia uzoefu wa mvua za miaka iliyopita.

Ameeleza kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha huduma za uokoaji zinapatikana kwa wakati katika maeneo yaliyo hatarini.

Aidha, amewataka wananchi kutoa taarifa mapema wanapoona dalili za hatari, kushirikiana na jeshi hilo na kufuata maelekezo ya usalama ili kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mafuriko.

Nayo Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) umeweka mikakati ya kukabiliana na majanga yanayoweza kusababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa, ikiwamo kufanya tathmini ya maeneo hatarishi na kuandaa vifaa vya dharura ili kupunguza athari kwa barabara na madaraja.

Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mohamed Besta, amesema hatua hizo ni sehemu ya maandalizi ya kukabiliana na dharura zinazoweza kutokea, kwa kuimarisha ushirikiano kati ya viongozi wa mikoa, mameneja wa taasisi hiyo na watoa huduma mbalimbali.

Amesema timu maalumu zimeundwa kwa ajili ya kutathmini maeneo yaliyo katika hatari ya kukumbwa na majanga na kukagua mifumo ya mifereji ya maji ili kuhakikisha inapitisha maji vizuri bila kuzibwa na takataka au vifusi.

Amesema maandalizi hayo pia yanahusisha kuweka tayari vifaa na rasilimali muhimu, ikiwamo mitambo mizito, ili kuwezesha hatua za haraka pindi majanga yanapotokea.

Besta amesema uzoefu uliopatikana kutokana na matukio ya hali mbaya ya hewa katika maeneo mbalimbali, yakiwamo mikoa ya Lindi na Rukwa, umeimarisha umuhimu wa ushirikiano katika kukabiliana na changamoto hizo.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *