Wahitimu Shule ya Aboud Jumbe wajutia kauli zao, waomba msamaha
Dar es Salaam. Baadhi ya wahitimu wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Aboud Jumbe, Kigamboni, Dar es Salaam, wameomba radhi kwa walimu, wazazi, Serikali na Watanzania kufuatia kauli zao zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii na kuzua mjadala.
Wahitimu hao (majina yao yanahifadhiwa kutokana na kutotimiza umri wa miaka 18) wameeleza masikitiko yao kuhusu kauli hizo, wakikiri kuwa vitendo vyao vimeidhalilisha shule yao na kuibua maswali kuhusu malezi wanayopata nyumbani na shuleni.
Mmoja wa wanafunzi hao amesema kauli walizotoa zimeacha taswira kwamba wazazi na walimu wao hawawapi malezi yanayostahili, hivyo ameiomba jamii iwasamehe kwa makosa waliyoyafanya.
Mwanafunzi mwingine ameomba msamaha kwa walimu, Serikali na uongozi wa shule hiyo, akisema wanatambua kuwa walifanya vitendo vya utovu wa nidhamu vilivyoichafua taswira ya shule yao.
Baadhi ya video zilizotumwa mitandaoni zikiwaonyesha wahitimu hao wa kidato cha nne
“Tumeidhalilisha sana shule yetu, hatukujua kitakachotokea, tunaomba mtusamehe,” amesema.
Mwanafunzi wa tatu ameomba radhi kwa makosa waliyofanya wakiwa mtaani, huku akiwataka vijana wengine wa rika lao kujiepusha na vitendo kama walivyofanya wao.
“Tunaomba msamaha kwa walimu na wazazi, tunajua tumekosea lakini hatutarudia tena, na Tanzania nzima mtusamehe, tunajua mitandao ni chombo rahisi ambacho kinafikisha ujumbe, tunaomba mtusamehe sana,” amesema.
Hatua hiyo imekuja baada ya video zinazowaonyesha wahitimu hao kusambaa kwenye mitandao ya kijamii na kukosolewa na baadhi ya watumiaji wa mitandao hiyo.
Baadhi ya video zilizotumwa mitandaoni zikiwaonyesha wahitimu hao wa kidato cha nne
Oktoba 25, 2026, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Doroth Gwajima, alikemea vikali mwenendo wa baadhi ya mabinti wanafunzi wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii, akieleza kuwa vitendo vyao ni ujinga.
Kupitia ukurasa wake rasmi wa Instagram, Dk Gwajima alieleza kusikitishwa kwake na video zilizosambaa zikiwaonyesha mabinti hao, huku akitaka kufahamu shule wanazosoma ili hatua stahiki zichukuliwe kwa kushirikiana na walimu na wazazi wao.
“Haya, hawa ni wa shule gani ili tutete jambo na walimu, tufahamu wazazi wao wako wapi ili tuwafikie na kushirikiana kuwakomboa mabinti hawa kwenye fikra hizi mbaya kwa elimu, malezi na makuzi endelevu maana naona mabinti hawa wanajiandalia ajali ya maisha yao bila bima,” alisema Dk Gwajima.
Baadhi ya video zilizotumwa mitandaoni zikiwaonyesha wahitimu hao wa kidato cha nne
Aliongeza: “Kifupi huu ni ujinga na ni huzuni sana mabinti kama hawa kugeuza ujinga kuwa mtaji wa maendeleo na ustawi.”
Akizungumza katika kikao kilichofanyika Jumatatu, Oktoba 26, 2026, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Mikaya Dalmia alisema wamekutana na wahitimu hao, wazazi na walimu kwa lengo la kuwakumbusha wazazi wajibu wao katika malezi na kuwasaidia vijana kujifunza kutokana na kilichotokea.
“Tunapaswa kutoa muda wetu kwa malezi, kujua mtoto anapotoka nyumbani anaenda wapi na anakutana na nani, pamoja na kufuatilia maendeleo yake ya shule,” alisema Dalmia.
Alisema mitandao ya kijamii huhifadhi kumbukumbu za mambo yanayochapishwa, hivyo vijana wanapaswa kuzingatia athari za kauli na vitendo vyao kwa maisha yao ya baadaye, ikiwamo wanapotafuta ajira au kujenga mahusiano ya kibiashara.
Dalmia alisema jukumu la malezi huanzia katika familia na kuendelea shuleni na katika jamii, akiwataka wazazi kushirikiana na walimu kufuatilia tabia, mahitaji na changamoto zinazowakabili watoto wao.
Alifafanua kuwa lengo la hatua zilizochukuliwa si kuwaadhibu vijana pekee, bali pia kuwaelimisha na kuwaongoza ili wajifunze kutokana na kilichotokea na kuepuka kurudia makosa hayo.
Aliwataka wahitimu hao kutumia kipindi wanachosubiri matokeo ya mitihani kwa shughuli zenye manufaa, ikiwamo kujifunza matumizi ya kompyuta, kushiriki shughuli za kijamii na kujifunza stadi za kujitegemea.

