Wananchi Moshi walalamikia uhaba wa maji, Muwsa yaeleza chanzo
Moshi. Baadhi ya wananchi wa kata za Longuo B, Msaranga na Ng’ambo, Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wamelalamikia uhaba wa maji safi na salama unaowalazimu kununua ndoo moja kwa Sh500 hadi Sh1,000, huku wengine wakiamka usiku kutafuta huduma hiyo.
Wamesema hali hiyo imewaathiri katika shughuli za nyumbani, ikiwemo kupika, kuoga na kutumia vyoo vya ndani, huku fedha walizopanga kutumia kwa mahitaji mengine zikielekezwa kununua maji.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (Muwsa), Kija Limbe, amesema tatizo hilo limesababishwa na kuziba kwa bomba na kwamba wataalamu wanaendelea kulishughulikia ili kurejesha huduma.
“Kuna changamoto ya bomba kuziba na imeshajulikana. Naifanyia kazi na maji yatapatikana,” amesema Limbe.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi katika maeneo hayo Oktoba 26, 2026, umebaini baadhi ya kaya kukosa maji, huku wakazi wa Longuo B wakisema tatizo limechukua takribani wiki tatu na baadhi ya wakazi wa Msaranga wakieleza kukosa huduma hiyo kwa siku kadhaa mfululizo.
Akizungumza na Mwananchi, mkazi wa Longuo B, Marry Mbowe, amesema hali hiyo imeathiri kipato chake kwa kuwa sehemu ya fedha anazopata kupitia biashara huitumia kununua maji.
“Changamoto tunayopata hapa ni maji, yanasumbua sana. Tuna muda mrefu maji hayatoki. Wakati mwingine tunanunua maji kwa Sh500 kwa ndoo, na kwa siku naweza kununua ndoo tatu au nne,” amesema.
Amesema tatizo hilo hujitokeza mara kwa mara katika kipindi kama hicho cha mwaka, akiiomba Serikali kuhakikisha huduma inapatikana kwa uhakika.
“Mabomba hayatoi maji, kwa hiyo tunapata shida. Tunaomba Serikali ituletee maji, maana kila mwaka kipindi kama hiki maji yanakuwa shida. Faida ninayopata kwenye biashara yangu ndiyo ninayotumia kununua maji,” amesema.
Mkazi mwingine, Happy Joseph, amesema hata maji yanapopatikana, hutoka kwa kiwango kidogo kisichokidhi mahitaji ya kaya.
Amesema kwa takribani mwezi mmoja wamekuwa wakikabiliwa na changamoto hiyo, hali inayowalazimu kununua maji au kutafuta maeneo mengine.
“Changamoto ya maji ni kubwa. Hata yakitoka, yanatoka tone kwa tone. Wakati mwingine hata kuoga inakuwa shida kwa sababu hakuna maji,” amesema.
Kwa upande wake, Mercy Msaki, mkazi wa Msaranga, amesema wamekuwa wakiamka saa nane usiku kutafuta maji hadi saa 11 alfajiri bila uhakika wa kuyapata.
“Tuna changamoto ya maji, ni wiki ya pili sasa hatuna maji. Tumekuwa tukiamka saa nane usiku kutafuta huduma hiyo hadi saa 11 alfajiri, na hatujapata taarifa yoyote kutoka kwa mamlaka ya maji kuhusu changamoto iliyopo,” amesema.
Naye Lucy Mmary amesema ukosefu wa maji unasababisha familia kushindwa kutekeleza mahitaji muhimu, ikiwemo kupika na kutumia vyoo vya ndani.
“Tunakwenda kuomba maji kwa watu wenye visima. Wakati mwingine tukikosa maji tunashindwa hata kupika chakula, kwa sababu ukipata ndoo mbili tu haitoshi kuhudumia familia,” amesema.
Mkazi mwingine, Agatha Joseph, amesema hali huwa mbaya zaidi mwishoni mwa wiki, wananchi wanapolazimika kutembea na ndoo kutafuta maji katika maeneo mbalimbali.
“Maji ni shida sana, hasa Jumamosi na Jumapili. Watu wanatembea na ndoo barabarani kutafuta maji, lakini mamlaka hazisemi chochote mpaka sasa,” amesema.
Diwani wa Kata ya Longuo B, Benedict Mwashambwa, amesema eneo hilo limekuwa na changamoto ya maji kwa takribani wiki tatu, licha ya kuwepo kwa miundombinu ya kusambaza huduma hiyo.
Amesema amekuwa akiwasiliana na Muwsa kutafuta suluhisho, lakini wananchi wameendelea kukabiliwa na adha hiyo.
“Nimewasiliana na Mkurugenzi wa Muwsa, ambaye aliniambia kuwa wataalamu wako eneo la tukio kushughulikia tatizo. Wananchi wamefikia hatua ya kununua maji kwa watu wenye visima kwa hadi Sh1,000 kwa ndoo ya lita 20,” amesema.
Mwashambwa amesema ukosefu wa maji unaweza kuhatarisha afya za wananchi, hasa kaya zenye vyoo vya ndani vinavyohitaji maji. Ameongeza kuwa wanafunzi wa shule ya msingi katika eneo hilo hulazimika kutembea umbali wa mita 900 hadi kilomita moja kutafuta maji.
Ameiomba Serikali kulichukulia suala hilo kuwa la dharura na kurejesha huduma haraka.
“Wananchi hawahitaji maneno mengi, wanahitaji huduma. Kukaa karibu mwezi mzima bila maji ni hatari kwa afya na maisha yao. Tunaomba hatua zichukuliwe haraka,” amesema.
Diwani wa kata ya Longuo B, Benedict Mwashambwa akizungumzia changamoyo ya maji katika kata yake.
Naye Diwani wa Kata ya Msaranga, Alhaji Ally Pendo (Dunga), amesema baadhi ya maeneo ya kata hiyo yamekosa maji kwa takribani siku nne. Amesema amewasiliana na mamlaka husika na kuambiwa kuwa tatizo linafanyiwa kazi.
Amewataka wananchi kutunza vyanzo vya maji kwa kuhifadhi miti, kuepuka ukataji ovyo wa misitu na kufanya usafi katika maeneo yao.
Katika hatua nyingine,Kamanda Jongo amesema kuanzia Oktoba 17 hadi 26, 2026, yameripotiwa matukio matatu ya vifo vya watu kujinyonga mkoani Geita.Miongoni mwa matukio hayo ni tukio la Oktoba 17,2026 lililomhusisha mwanaume aliyefahamika kwa jina la Isack Ibrahimu(36), mkazi wa Makurugusi, Kata ya Makurugusi, Wilaya ya Chato, alikutwa amefariki baada ya kujijeruhi mwenyewe maeneo ya shingoni na tumboni kwa kutumia kitu chenye ncha kali,huku chanzo cha tukio hilo kikitajwa kuwa msongo wa mawazo uliotokana ugumu wa maisha.
Aidha katika tukio jingine ni Oktoba 21, 2026 ambapo Timotheo Chande(21), aliyekuwa dereva wa bajaji na mkazi wa Mtaa wa Moringe, Kata ya Kalangalala, Manispaa ya Geita, aliyekutwa amefariki nyumbani kwao baada ya kujinyonga, ambapo chanzo cha tukio hilo kikitajwa kuwa ni msongo wa mawazo uliotokana na mapenzi.
Pia Oktoba 26, 2026 Japhet Ladislaus(19), aliyekuwa akiishi Mtaa wa Mbabani, Kata ya Mtakuja,ambaye alikutwa amefariki baada ya kujinyonga nje ya nyumba yao, chanzo cha tukio hilo kikiwa ni msongo wa mawazo uliotokana na changamoto za mahusiano.
Miili ya marehemu ilifanyiwa uchunguzi wa kitaalamu na kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya taratibu za mazishi.Pia Kamanda Jongo ametoa rai kwa wananchi kuacha kuchukua uamuzi binafsi wanapokuwa wanapitia changamoto na badala yake washirikishe wanafamilia na jamii inayowazunguka.
