Waziri Ulega awataka watendaji kutumia madaraka kwa uadilifu
3 mins read

Waziri Ulega awataka watendaji kutumia madaraka kwa uadilifu

Babati.  Waziri wa Katiba na Sheria, Abdallah Ulega, amewataka viongozi na watendaji wa mamlaka za Serikali za mitaa kutumia madaraka waliyopewa kwa uadilifu, kuzingatia sheria na kuheshimu haki za binadamu ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Ulega ametoa wito huo leo Jumatatu, Oktoba 26, 2026, mjini Babati, Mkoa wa Manyara, alipofungua mafunzo ya elimu ya uraia na utawala bora yanayolenga kuwajengea uwezo viongozi na watendaji kuhusu Katiba, matumizi sahihi ya madaraka na uwajibikaji katika utumishi wa umma.

Amesema viongozi na watendaji wanapaswa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora zinazostahili.

Pia, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia mahitaji ya makundi maalumu katika jamii, wakiwamo watu wenye ulemavu na wazee, pamoja na kuhakikisha malalamiko ya wananchi yanapokelewa, yanashughulikiwa na mrejesho unatolewa kwa wakati.

“Ukosefu wa mrejesho kuhusu malalamiko ya wananchi umekuwa chanzo cha kero kwa wananchi, hivyo ni muhimu kwa watendaji kuboresha mifumo ya mawasiliano na uwajibikaji ili kujenga imani kati ya wananchi na Serikali,” amesema.

Ulega amewataka watendaji kuheshimu mamlaka za kisheria zilizopewa uwezo wa kutoa maamuzi, akieleza kuwa kufanya hivyo ni muhimu katika kulinda amani, utulivu na misingi ya utawala wa sheria.

Waziri wa Katiba na Sheria Abdallah Ulega, akizungumza na Viongozi na Watendaji wa Serikali za Mitaa Mkoa wa Manyara, juu ya uraia na utawala bora, mjini Babati. Picha za Joseph Lyimo

“Mafunzo haya yanawajengea uwezo wa kuifuata Katiba, utawala wa sheria na haki za binadamu. Tujenge imani kwa wananchi, tumieni madaraka kwa uadilifu na kuwatumikia wananchi,” amesema.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dk Seif Shekhalaghe amesema utawala bora ni msingi muhimu wa kudumisha amani, kuimarisha uwajibikaji na kuongeza ufanisi wa kiutendaji katika ngazi zote za Serikali.

Amesema Mkoa wa Manyara ni wa kwanza kupokea mafunzo hayo, yanayolenga kuwajengea viongozi na watendaji uwezo wa kuelewa na kuzingatia misingi ya Katiba, utawala wa sheria na haki za binadamu wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.

Amesema mada zitakazofundishwa ni pamoja na haki na wajibu wa binadamu, demokrasia na utawala bora, matumizi ya madaraka ya umma kwa kuzingatia sheria za nchi, pamoja na ulinzi na usalama.

“Miongoni mwa mada zitakazofundishwa katika mafunzo hayo ni haki na wajibu wa binadamu, demokrasia na utawala bora, matumizi ya madaraka ya umma kwa kuzingatia sheria za nchi, pamoja na ulinzi na usalama,” amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Martine Shigella, ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuupa kipaumbele mkoa huo na kuuchagua kuwa wa kwanza kuzindua kampeni hiyo katika mwaka wa fedha 2026/27.

Baadhi ya Viongozi na Watendaji wa Serikali za Mitaa mkoani Manyara, wakijengewa uwezo juu ya uraia na utawala bora na Waziri wa Katiba na Sheria Abdallah Ulega mjini Babati. Picha na Joseph Lyimo

Shigella amesema anaamini mafunzo hayo yakifuatiliwa na kueleweka vizuri na washiriki yatasaidia kupunguza changamoto za kiutendaji na migogoro inayoweza kutokea kutokana na kutokuzingatiwa kwa sheria na taratibu zilizowekwa.

“Ni matumaini yangu kuwa mafunzo haya tukiyafuatilia vizuri na kuondoka hapa tukiwa na uelewa wa kutosha, tutapunguza changamoto zilizojitokeza kwa kuzisimamia na kuzirekebisha. Pia, tutaweza kuzuia kwa kiwango kikubwa changamoto ambazo zingeweza kutokea kutokana na kutokuzingatia sheria,” amesema Shigella.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Naisinyai, Valentine Tesha, amesema mafunzo hayo yanalenga kuongeza uelewa wa viongozi na wananchi kuhusu haki na wajibu wao.

Amesema kupitia mafunzo hayo, viongozi na watendaji wataimarisha uwajibikaji katika utoaji wa huduma, kupunguza migogoro na kuendeleza amani, utulivu na maendeleo katika jamii.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *