KONA YA MSTAAFU: Hivi ni nani anayehusika na masuala ya wastaafu?
Kuna jambo linalomfikirisha sana Mstaafu wetu tangu alipofikisha miaka 60 na sheria kumtaka achape yebo na aachie ngazi maana mchuma ulikuwa unaondoka na ajira yake aliyotumikia kwa miaka 40 ilikuwa ikihitaji vijana waliotoka vyuoni.
Hili limekuwa likimfikirisha mno Mstaafu, kwamba kwa nini mwajiriwa astaafu akiwa na miaka 60 akiwa hoi wa kupokea pensheni tu.
Ili mwajiriwa huyo aweze kusaafu kwa hiyari na miaka 45 na aachie mchuma kwa nguvu atake asitake, akiwa na miaka 50 akiwa bado na nguvu ya kuendelea na mitkasi mingine maisha
Sheria tuliitunga sisi wenyewe, sio sheria ya Mungu, ikimtaka mwajiriwa aachie ngazi anapofikisha miaka 60, japo kuna binadamu wanafikisha miaka 70 hata 80 na bado wapo tu wakiendelea kuhomola keki ya Taifa, huku mstaafu aliyeijenga nchi kwa miaka 60 akiishia kusikia tu harufu keki! Yaleyale ya shamba la wanyama.
Tunapoambiwa kuwa binadamu wote ni sawa, lakini wapo binadamu wengine wapo sawa zaidi kuliko sisi makapuku.
Ndio maana Mstaafu wetu alipofikisha miaka 60 tu akatakiwa achape yebo fasta astaafu, lakini kina ‘naniliu’ wa miaka 75 na 80 wapo tu, keki ya Taifa ikiendelea kuwahusu!
Haya, tangu Mstaafu awe mpokeaji wa kudumu wa kijipensheni chake miaka kadhaa nyuma, amekuwa akijiuliza ni nani anayepaswa kusimama kidete kuyashughulikia mambo muhimu yanaomhusu mstaafu wa kima cha chini hasa afya yake na kijipensheni chake. Bado hajapata jibu la kueleweka na anaona tu watu wakipishana na kukanyagana waonekane kumshughulikia Mstaafu.
Utakuwa unamtia aibu bure mstaafu wetu ukimuuliza hapa kama yupo mtu maalumu anayeshulikia mambo ya wastaafu na ni nani mtu huyo.
Mstaafu wetu ataishia kung’aa macho tu maana hamjui mtu wa namna hiyo, kama yupo!
Ndio maana pensheni ya Mstaafu ya Sh105,000 kwa mwezi iliganda naye miaka 20, rudia hapo.
Kwa msisitizo miaka 20, Mstaafu akipokea Sh105,000 na hakuna yeyote anayeshituka !
Watu wakawa wako bize kujiongeza mishahara mpaka Sh15,000,000 kwa mwezi, posho, marupurupu na marapurapu mengine kibao, lakini sio pensheni ya mstaafu ya Sh105,000!
Kumbe miujiza ya kulisha watu 5,000 kwa skonzi tano na visamaki viwili haikuishia kwenye Biblia tu.
Mstaafu ameweza kuishi miaka 20 kwa pensheni Sh105,000 tu kwa mwezi na ameweza kubaki hai. Ni muujiza wa karne ya 20!
Mstaafu anakumbuka kuna kibubu kiliwahi kutoa pendekezo kwamba Mstaafu anastahili pensheni ya Sh700,000 na chenji kadhaa kwa mwezi, pendekezo ambalo hajui hata liliishia wapi, tatizo la kukosa mtu maalumu wa kusimamia jambo!
Huu ulikuwa ni wakati ule vibubu vilipoanza kumea kama uyoga na kuwa rundo kila kibubu kikiwa na waajiriwa wake na watu wakianza kutafuta teuzi na zilipoanza, pendekezo la Sh700,000 na ushee likapotea hewanj ama gizani na hakulisikia tena!
Huu pia ulikuwa wakati ulee wastaafu wa kima cha kama sio cha cchizi, walikuwa wakipokea Sh105,000 kwa mwezi, iliyodumu kwa miaka 20, huku mishahara ikiongezwa kila baada ya miaka mitatu minne, huku hakuna hata mtu anayekohoa au kupaliwa kooni akamkumbuka Mstaafu.
Kuyaepuka haya, sasa ianzishwe wizara maalumu ya wazee na wastaafu kushughulikia mambo muhimu kibao yanayowahusu wastaafu, kubwa likiwa ni kupata pensheni Sh105,000 kwa mwezi na ili kupata matibabu ya bure kwa wazee yasiyoishia kwenye kanga.
Tuepuke miujiza ya skonzi tano na vipande viwili vya samaki karne ya 22 hii!

