Wahitimu wagombania msichana, mmoja atuhumiwa kumuua mwenzake
2 mins read

Wahitimu wagombania msichana, mmoja atuhumiwa kumuua mwenzake

Bukombe. Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linamshikilia na kumhoji Lameck Isack, mhitimu wa Kidato cha nne mwaka 2026, kwa tuhuma za kumuua David Lucas, aliyekuwa mwenzake kwa kumchoma kwa kitu chenye ncha kali shingoni na ubavuni upande wa kulia.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari leo Ijumaa, Oktoba 30, 2026, na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo, tukio hilo lilitokea Alhamisi, Oktoba 29, 2026, saa 8 mchana Kijiji cha Mhama, Kata ya Namonge, Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita.

Kamanda Jongo amesema kabla ya tukio hilo, mtuhumiwa, marehemu na vijana wengine watatu walikutana katika kijiwe kwa mazungumzo.

Wote walikuwa wahitimu wa Kidato cha nne mwaka 2026 Shule ya Sekondari Said Nkumba.

Amesema muda mfupi baada ya kukutana, kulitokea mabishano kati ya mtuhumiwa na marehemu, ambayo yaligeuka ugomvi baada ya kila mmoja kudai kuwa na uhusiano wa kimapenzi na msichana mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa.

Msichana huyo pia ni mhitimu wa Kidato cha nne katika shule hiyo.

Katika ugomvi huo, mtuhumiwa anadaiwa kumchoma marehemu kwa kitu chenye ncha kali shingoni na ubavuni upande wa kulia, hali iliyosababisha kifo chake muda mfupi baadaye.

Kamanda Jongo ametaja wivu wa kimapenzi kuwa chanzo cha tukio hilo.

Amesema mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi wa kitaalamu na kukabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili ya mazishi, huku polisi wakiendelea na uchunguzi ili mtuhumiwa afikishwe mahakamani.

Katika hatua nyingine, Kamanda Jongo ametoa wito kwa wazazi na walezi kuimarisha malezi, maadili na uangalizi wa watoto wao, ikiwemo kufuatilia makundi wanayoshirikiana nayo na kuwapa mwongozo na ushauri sahihi.

Wivu wa kimapenzi wachangia mauaji

Takwimu za hali ya uhalifu na matukio ya usalama barabarani zilizotolewa na Jeshi la Polisi na kuchapishwa kwenye tovuti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonyesha kuwa mauaji nchini yaliongezeka katika kipindi cha Januari hadi Juni 2026.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, jumla ya makosa 936 ya mauaji yaliripotiwa katika kipindi hicho, ikilinganishwa na makosa 926 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2025. Hilo ni ongezeko la makosa 10, sawa na asilimia 1.1.

Katika matukio hayo, jumla ya watu 970 waliuawa, wakiwemo wanaume 722 na wanawake 248.

Ripoti hiyo inaonyesha ugomvi majumbani ulikuwa chanzo kilichohusishwa na vifo vya watu 284, huku wivu wa kimapenzi au kushikwa ugoni ukihusishwa na vifo vya watu 174.

Kwa Mkoa wa Geita, takwimu zinaonyesha matukio 27 ya mauaji yaliripotiwa katika kipindi cha Januari hadi Juni 2026, yakiwahusisha wanawake 14 na wanaume 13.

Kati ya matukio hayo, vifo vya watu sita vilihusishwa na wivu wa kimapenzi, ikilinganishwa na vifo vinane vilivyoripotiwa kutokana na sababu hiyo katika kipindi kama hicho mwaka 2025.

Ingawa takwimu hizo zinaonyesha kupungua kwa vifo vinavyohusishwa na wivu wa kimapenzi mkoani Geita, matukio kama hayo yanaendelea kuibua umuhimu wa kuimarisha malezi, utatuzi wa migogoro na uhamasishaji wa jamii kuhusu madhara ya wivu unaogeuka kuwa vurugu.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *