Tanzania kuongoza uhifadhi Ziwa Tanganyika
Dar es Salaam. Tanzania imechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kikanda ya Mkataba wa Usimamizi Endelevu wa Mazingira ya Bonde la Ziwa Tanganyika, hatua inayoiweka katika nafasi ya kuongoza juhudi za kukabiliana na changamoto za kimazingira zinazoongezeka katika ziwa hilo.
Uchaguzi huo ulifanyika leo Ijumaa, Oktoba 30, 2026, wakati wa kikao cha 14 cha Mkutano wa Mawaziri wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (LTA), unaozikutanisha Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Tanzania na Zambia.
Tanzania inachukua nafasi hiyo wakati takribani theluthi mbili ya bonde la Ziwa Tanganyika likiwa ndani ya mipaka yake, jambo linaloipa nafasi muhimu katika juhudi za kikanda za kulinda ziwa hilo na kusimamia rasilimali zake kwa uendelevu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (kulia), akipokea Uenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (LTA) kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu na Mazingira nchini Zambia, Dk Douty Chibamba katika Mkutano wa 14 wa Baraza hilo uliofanyika jijini Dar es Salaam leo Oktoba 30, 2026. Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais
Hata hivyo, jukumu hilo linakuja wakati kukiwa na ongezeko la kina cha maji, kupungua kwa akiba ya samaki na matukio ya hali mbaya ya hewa yanayozidi kutishia mfumo wa ikolojia wa ziwa hilo pamoja na maisha ya mamilioni ya watu wanaolitegemea.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika, Dk Emma Liwenga ameueleza mkutano huo kuwa:
“Changamoto mbili kubwa kwa sasa zinahitaji kupewa kipaumbele maalumu, ongezeko la kina cha maji na kupungua kwa kiwango cha kutia wasiwasi cha akiba ya samaki,” amesema.
Amesema mafuriko yaliyotokea mwaka 2023 na 2024 yaliwaathiri takribani watu 289,000, yakaharibu miundombinu na kuvuruga shughuli za kiuchumi katika jamii zinazoishi kandokando ya ziwa hilo.
Hali katika sekta ya uvuvi nayo inaashiria kuongezeka kwa shinikizo dhidi ya rasilimali za ziwa hilo.
Tathmini ya kikanda iliyofanyika mwaka 2025 na 2026 ilikadiria kuwa kiasi cha samaki wanaoishi kwenye tabaka la juu la maji kilikuwa tani 1,600, ikilinganishwa na tani 3,500 zilizorekodiwa mwaka 1998, sawa na upungufu wa takribani asilimia 62.
Wadau kutoka nchi nne zinazopakana na Ziwa Tanganyika, ambazo ni Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Tanzania na Zambia, wakifuatilia Mkutano wa 14 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri la Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (LTA), unaofanyika jijini Dar es Salaam, Oktoba 30, 2026, kujadili ushirikiano wa kikanda na usimamizi endelevu wa rasilimali za ziwa hilo. Picha na Said Powa
Tathmini hiyo ilikuwa ya kwanza kuhusisha ziwa lote tangu mwaka 1998, na kutoa takwimu mpya kuhusu changamoto zinazoikabili sekta ya uvuvi pamoja na jamii zinazotegemea samaki kwa chakula na kipato.
Akizungumzia hatua zinazoweza kuchukuliwa kukabiliana na ongezeko la kina cha maji, Dk Liwenga amesema utafiti wa upembuzi yakinifu ulifanyika kuchunguza uwezekano wa kuchimba na kuondoa tope na mashapo katika Mto Rusizi, ambao ndiyo njia pekee ya maji ya ziwa hilo kutiririka kuelekea Mto Congo.
Amesema ingawa utafiti huo umebaini kuwa uchimbaji huo unawezekana kitaalamu, ufanisi wake unaweza kuwa mdogo wakati wa mabadiliko makubwa ya hali ya mtiririko wa maji.
“Kuchanganya uchimbaji na upanuzi wa mkondo wa mto kunaweza kuongeza ufanisi wa upitishaji wa maji, huku usimamizi wa maeneo ya vyanzo vya maji ukiwa suluhisho la ziada muhimu, katika kupunguza mashapo yanayoingia ziwani na kuimarisha ustahimilivu wa muda mrefu,” amesema.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni amesema juhudi za uhifadhi katika ukanda huo zinapaswa kwenda sambamba na kuleta manufaa ya kiuchumi kwa jamii bila kuharibu mfumo wa ikolojia wa ziwa hilo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, akizungumza wakati wa kupokea Uenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (LTA), katika Mkutano wa 14 wa Baraza hilo uliofanyika jijini Dar es Salaam, Oktoba 30, 2026.
“Uhifadhi wa ziwa lazima uendane na maendeleo endelevu ya kiuchumi pamoja na fursa za uwekezaji rafiki kwa mazingira zinazochangia ajira na kuongeza kipato cha wananchi,” amesema.
Masauni amesema nchi hizo nne zinapaswa kusawazisha masilahi ya kila moja kitaifa na wajibu wa pamoja wa kuhakikisha ziwa hilo linasimamiwa kwa uendelevu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (wa pili kulia), akiwa na viongozi wengine wakati wa kupokea Uenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (LTA), katika Mkutano wa 14 wa Baraza hilo uliofanyika jijini Dar es Salaam, Oktoba 30, 2026.
Amezitaka nchi hizo kuongeza uwajibikaji, kutafuta rasilimali fedha na kuimarisha ushirikiano wa kisayansi, huku akisisitiza umuhimu wa kuweka majukumu bayana, muda wa utekelezaji na malengo yanayopimika katika kutekeleza maamuzi yanayofikiwa chini ya mamlaka hiyo.
Athari za mabadiliko ya tabianchi katika bonde hilo pia zimeibuliwa na Mwenyekiti wa Mkutano wa Mawaziri wa LTA, Dk Douty Chibamba, aliyeonya kuhusu hatari zinazoweza kusababishwa na hali kali ya El Niño.
“Tukio la El Niño kali lililotangazwa hivi karibuni linatoa changamoto kubwa kwa bonde la Ziwa Tanganyika,” amesema.
Dk Chibamba amehimiza kuboreshwa kwa mfumo wa kubadilishana taarifa za hali ya hewa, kuimarishwa kwa mifumo ya tahadhari za mapema na maandalizi bora ya kukabiliana na majanga, ili kusaidia jamii kukabiliana na hali mbaya ya hewa na uwezekano wa kutokea kwa mafuriko.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Yusuph Masauni (kulia), akifuatiwa na mwakilishi wa Zambia, Dk Douty Chibamba, mwakilishi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Jean-Pierre Tshimanga Bwana, na Balozi wa Burundi nchini Tanzania, Léontine Nzeyimana, wakisaini maazimio ya Mkutano wa 14 wa Baraza la Mawaziri la Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (LTA), uliofanyika jijini Dar es Salaam, Oktoba 30, 2026. Picha na Said Powa
“Upatikanaji wa fedha za kutosha na kwa uhakika ni muhimu kwa mamlaka kufanya kazi kwa ufanisi na kutekeleza majukumu yake,” amesema.
Waziri wa Uvuvi na Ufugaji wa DRC, Jean Pierre Tshimanga, pia ametoa wito wa kuwepo kwa mkakati wa pamoja wa kikanda, akisisitiza kuwa kulinda ziwa hilo kunahitaji dhamira na ushiriki wa nchi zote nne zinazopakana nalo.
