Watatu mbaroni kwa tuhuma za kumtorosha mwanafunzi wa kidato cha nne
Morogoro. Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linawashikilia watu watatu na kumsaka mmoja kwa tuhuma za kumtorosha kwa dhamira ya kwenda kumwozesha binti ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha nne (jina limehifadhiwa) wa shule ya sekondari Sokoine Memorial iliyopo Dakawa, Wilaya ya Mvomero.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 30, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Andrew Kantimbo amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Kandolo Kiasi, Michael Shabala na Victoria Hagiro, wote ni wafugaji wa jamii ya kimaasai, wakazi wa Sokoine.
Kamanda Kantimbo amesema tukio hilo limetokea Oktoba 26, 2026 saa 9 alasiri katika eneo la Wami Sokoine ambapo mtuhumiwa anayesakwa, James Kopilato, walimtorosha mwanafunzi huyo akiwa anatoka shule na wanafunzi wenzake kufanya mitihani ya Taifa ya kumaliza kidato cha nne inayoendelea kote nchini.
“Akiwa anarudi shule na wanafunzi wenzake, watuhumiwa hao walimchukua kwa nguvu na kumpakia kwenye pikipiki kisha kutokomea naye kusikojulikana,” amesema Kamanda Kantimbo.
Amesema miongoni mwa waliokamatwa ni pamoja na mama mzazi wa kijana anayedaiwa kumchukua binti huyo, hata hivyo uchunguzi kuhusu tukio hilo unaendelea ili kumkamata mtuhumiwa aliyekimbia na kubaini mahali ambako mwanafunzi huyo amepelekwa.
“Kiini cha tukio hili kimebainika kuwa ni mila potofu za kabila hili la kimaasai ambalo wanaamini kuwa binti akikataa kuozeshwa kwa hiari, kinachofuata ni kuchukuliwa kwa nguvu na kisha familia zinakaa na kupatana kwa ajili ya mahali,” amesema Kantimbo.
Kufuatia tukio hilo, Kamanda Kantimbo amewataka wananchi hasa jamii ya wafugaji kuacha mila potofu za kuwatorosha watoto hasa wa kike chini ya himaya za wazazi wao na badala yake wasaidie wazazi hao kusimamia watoto hasa katika masomo ili watimize malengo yao.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Dakawa, Joshua Lugaso amesema binti huyo alinyakuliwa na vijana hao wa kimaasai alipokuwa akitoka shule kufanya mtihani wa kumaliza kidato cha nne na leo ni siku ya sita tangu atoroshwe na hajapatikana.
Lugaso ambaye ni mfugaji wa jamii ya kimaasai na kiongozi wa vijana wa kimaasai, amelaani kitendo hicho na kusema Serikali haiwezi kukubaliana nacho huku akiliahidi Jeshi la Polisi kulipa ushirikiano katika kuwasaka wote waliohusika kwenye tukio hilo.
“Kitendo hiki kilichofanywa na vijana hawa wa kimaasai hakikubaliki na mimi kama diwani ninayetoka kwenye jamii hiyo nimesikitishwa na sasa tunaendelea na uchunguzi nadhani siku si nyingi binti huyu atapatikana,” amesema Lugaso.
Ameongeza: “Kupitia vikao vyetu vya kimila tumekuwa tukielezana na kuelimishana ni marufuku binti yeyote kukatishwa masomo kwa sababu ya kuozeshwa ama kwa sababu nyingine yoyote ile. Kila mtoto anayetoka kwenye jamii hii ya kimaasai lazima asome.”

