Angola yashukuru kupewa eneo Mtumba kujenga ubalozi
4 mins read

Angola yashukuru kupewa eneo Mtumba kujenga ubalozi

Dar es Salaam. Rais wa Angola, Joao Lourenco, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuipatia nchi yake eneo katika Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma, kwa ajili ya kujenga ubalozi mdogo, akisema hatua hiyo ni ishara ya urafiki na itaimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo.Lourenco amesema uwepo wa ubalozi huo katika mji unaokusanya ofisi za Serikali utarahisisha mawasiliano na ushirikiano kati ya Tanzania na Angola.Rais huyo ambaye aliwasili nchini Oktoba 28, 2026 kwa ziara ya siku tatu alikuwa mgeni maalumu kwenye hafla ya uzinduzi wa mji huo wa Serikali.“Tunathamini sana hatua hii iliyochukuliwa na Serikali ya Tanzania, kutenga eneo kwa ajili ya kujenga ubalozi wa Angola ni heshima kubwa kwetu na inaimarisha ushirikiano wetu,”

Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akikata utepe pamoja na mgeni wake João Manuel Conçalves Lourenço, Rais wa Jamhuri ya Angola kuashiria ufunguzi wa majengo ya ofisi za wizara na taasisi za serikali katika Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma, Oktoba 30, 2026.

Mbali na kupewa eneo hilo la kujenga ofisi ya ubalozi, Angola imeta heshima ya mojawapo ya barabara katika Mji wa Serikali Mtumba kupewa jina la mwasisi wa taifa hilo Agosthino Nato.Hili linafanyika ikiwa imepita miezi minne tangu Angola kuzindua hospitali ya majeraha ya moto na kuipa jina la muasisi wa Taifa la Tanzania Julius Nyerere.Katika hatua nyingine, Tanzania inatarajia kupata soko jipya la bidhaa zake za kilimo nchini Angola, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji, kupanua fursa za biashara na kutengeneza ajira kwa Watanzania.Rais Lourenco amesema nchi yake imepokea pendekezo la Tanzania la kuingiza bidhaa za kilimo katika soko la Angola na kwamba Serikali yake itafanya kila linalowezekana kuwezesha ushirikiano huo.Amesema hatua hiyo ni miongoni mwa maeneo yanayoweza kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi hizo mbili, kuongeza uzalishaji na kutengeneza ajira, huku biashara ikipanuka katika ukanda wa Kusini mwa Afrika na soko la kimataifa.“Napenda kukaribisha kipekee wazo la Tanzania la kuleta bidhaa za kilimo katika nchi ya Angola. Lengo ni kuhakikisha bidhaa hizi zinafikia soko letu na tutafanya kila linalowezekana kuchagiza uhusiano huu,” amesema.Mbali na biashara ya mazao ya kilimo, Rais Lourenço amesema nchi hizo zimekubaliana kuimarisha sekta ya utalii kupitia kuanzisha safari za moja kwa moja za ndege kati ya Dar es Salaam na Luanda, hatua itakayorahisisha usafiri wa watu na bidhaa.Pia, amesema kuna mpango wa kuunganisha reli ya Tazara na reli ya Benguela ya Angola, kupitia Tanzania na Zambia, ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kuimarisha biashara katika ukanda huo.Ushirikiano huo wa miundombinu unatajwa kuwa na nafasi ya kupunguza vikwazo vya usafirishaji, kupanua masoko ya bidhaa za nchi hizo na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi.Katika hatua nyingine, amesema nchi hizo zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta ya mawasiliano na teknolojia, hususan teknolojia ya anga, akitaja satelaiti ya Angosat inayomilikiwa na Angola kuwa eneo linaloweza kutumika kubadilishana uzoefu na utaalamu.Amesema ushirikiano huo unaweza kuongeza uwezo wa mataifa hayo kutumia teknolojia katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za maendeleo.Rais Lourenco ameishukuru Tanzania kwa hatua zinazochukuliwa kufungua upya ubalozi wake nchini Angola, akisema hatua hiyo itasaidia kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na kurahisisha utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano.Katika masuala ya kikanda na kimataifa, Rais huyo amesema Tanzania na Angola zina dhamira ya kuendelea kushirikiana katika kulinda amani na utulivu barani Afrika.Amesema nchi hizo zinapaswa kutumia majukwaa ya kikanda na Umoja wa Afrika kutafuta suluhu za migogoro inayolikabili bara hilo, ikiwamo Sudan na maeneo mengine yenye changamoto za kiusalama.Amesisitiza umuhimu wa kutafuta suluhu za migogoro kwa njia za mazungumzo na kutumia mifumo ya Kiafrika badala ya kuacha migogoro hiyo kuendelea kuathiri maendeleo na ustawi wa wananchi.Amesema ushirikiano huo unaendana na dhamira ya Angola ya mwaka 2030 na Tanzania ya Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050, ambazo zinaweka mkazo katika maendeleo ya mataifa hayo.Amebainisha umuhimu wa ushiriki wa wanawake katika maendeleo endelevu, akitaja mikutano ya wanawake wabunge katika ukanda wa Maziwa Makuu kuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha mchango wao.Amesema Angola itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kujenga utengamano wa Afrika na kuhakikisha bara hilo linakuwa na amani, ustawi na maendeleo.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *