Heche: Katiba Mpya iwezeshe wananchi kuwawajibisha viongozi
Arusha. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Heche amesema Tanzania inahitaji Katiba Mpya itakayowapa wananchi mamlaka ya kuwawajibisha viongozi wasiotimiza wajibu wao.
Heche aliyasema hayo jana, Jumatano, Oktoba 21, 2026, akizungumza katika kongamano la Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) Mkoa wa Manyara lililofanyika Haydom, mkoani humo.
Alisema Katiba Mpya inapaswa kuweka mfumo utakaowawezesha wananchi kuwawajibisha viongozi, hasa wale wanaoshindwa kutekeleza ahadi walizotoa.
“Tanzania ina vyanzo vikubwa vya maji, lakini kuna wananchi wanakosa maji. Kuna watu wanaishi jangwani katika nchi nyingine, lakini wanapata maji. Hapa kwetu wananchi wanahangaika kutafuta maji,” alisema.
“Tunahitaji Katiba Mpya itakayowapa uhuru wananchi na kuhakikisha viongozi wanawajibika. Kama mnamweka kiongozi, lazima awajibike kweli. Akisema ataleta maji, alete. Asipoleta, uchaguzi unaofuata aende nyumbani. Nenda ukaangalie familia yako, anawekwa mwingine anayefaa,” amesema.
Akizungumzia mfumo wa vyama vingi vya siasa ulioanzishwa mwaka 1992, Heche alisema lengo lake ni kuwapa wananchi fursa ya kuchagua viongozi na vyama wanavyoona vinaweza kuwaletea maendeleo.
“Kwa hiyo, mfumo wa vyama vingi ulianzishwa ili wananchi muwe na chaguo. Kama Chadema haiwezi kuwaletea maendeleo, waondoe, wekeni watu wengine. Kama CCM wameshindwa, waondoe, wekeni watu wengine,” amesema.
Heche azungumzia changamoto za siasa
Akizungumzia nafasi ya wanawake, Heche amesema wanawake walikosa fursa nyingi miaka ya nyuma, lakini kwa sasa wana nafasi zaidi za kushiriki katika shughuli mbalimbali. Aliwataka kuendelea kupambana na umaskini na kudai haki zao.
Pia, amezungumzia changamoto zinazowakabili wanaosema ukweli, akitoa mfano wa Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, ambaye alisema anajaribiwa kunyamazishwa kwa nguvu.
Heche amesema licha ya changamoto hizo, chama hicho hakitakata tamaa na kitaendelea kusimamia kile kinachoamini kuwa ni ukweli.
“Kufanya shughuli za siasa, hasa za upinzani, si kazi rahisi. Kuna udhalilishaji mwingi na maumivu makubwa. Hii ni kazi ambayo umeutoa uhai wako wakati wowote, na unaweza kukuta watoto wako wanakuwa yatima,” amesema.
Ameongeza: “Ndugu zangu wanaosema ukweli wanakumbana na matatizo, ndiyo maana watu kama Lissu wanajaribiwa kunyamazishwa kwa nguvu zote. Lakini neno la Mungu linasema ukweli utatuweka huru. Sisi tuendelee kusema ukweli.”
Bawacha yaendelea kudai Katiba Mpya
Awali, Mwenyekiti wa Bawacha Kanda ya Kaskazini, Lucy Owenya, amesema chama hicho kitaendelea kupaza sauti kudai Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi.
Owenya amesema kwa mtazamo wake, matatizo mbalimbali yanayowakabili Watanzania yanatokana na Katiba iliyopo, hivyo akawataka wananchi kuendelea kushinikiza mabadiliko hayo.
“Tunaendelea kupaza sauti kudai Katiba Mpya. Haya yote tunayopita, matatizo yote tunayoyapitia, ni kutokana na Katiba ambayo siyo mbili. Tunaomba tuendelee kupiga kelele tupate Katiba Mpya,” amesema.
Amesema Chadema pia kitaendelea kudai Tume Huru ya Uchaguzi, huku akiwataka wananchi kukumbuka yaliyotokea katika chaguzi zilizopita na kuendelea kudai mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi.
Bawacha Manyara yakusanya fedha za ofisi
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bawacha Mkoa wa Manyara, Regula Mtei amesema baraza hilo limeanza kukusanya fedha kwa ajili ya kununua eneo na kujenga ofisi za mkoa huo, mradi unaokadiriwa kugharimu Sh30 milioni.
Amesema fedha zitakazopatikana kupitia michango na juhudi za wanachama zitatumika kununua ardhi na kujenga ofisi hizo, hatua aliyosema inalenga kukiimarisha chama mkoani humo.
Mtei ameongeza kuwa wanawake wa Chadema mkoani Manyara wameendelea kujitokeza na kushiriki katika shughuli za chama licha ya mazingira ya kisiasa ambayo alisema hayakuwa rafiki kwa kipindi cha nyuma.

