Kenya, Russia wakubaliana kusitisha uandikishaji Wakenya jeshini
3 mins read

Kenya, Russia wakubaliana kusitisha uandikishaji Wakenya jeshini

Dar es Salaam. Rais wa Russia, Vladimir Putin, amekubaliana na Rais wa Kenya, William Ruto, kusitisha uandikishaji wa raia wa Kenya katika jeshi la Russia, huku serikali ya Nairobi ikianza kufuatilia fidia kwa walioathirika na kurejeshwa salama kwa raia wake waliokwenda nchini humo kwa ajili ya kazi za kijeshi.

Makubaliano hayo yalitangazwa na Ruto baada ya mazungumzo yake na Putin yaliyofanyika katika Ikulu ya Kremlin, mjini Moscow, Ijumaa, Oktoba 30, 2026.

Ruto alisema Kenya imemteua mwanadiplomasia wa kijeshi, anayejulikana kama Defence Attaché, katika ubalozi wake mjini Moscow ili kushirikiana moja kwa moja na Wizara ya Ulinzi ya Russia katika kushughulikia masuala ya Wakenya walioandikishwa kwa shughuli za kijeshi.

Kwa mujibu wa Ruto, ofisa huyo ataratibu madai ya fidia kwa Wakenya walioathirika na kusaidia juhudi za kuhakikisha wanarejea nchini kwa usalama.

Hata hivyo, serikali haijatangaza kiwango cha fidia kitakacholipwa, vigezo vya wanaostahili kupata malipo hayo wala muda wa kukamilisha mchakato huo.

Akieleza makubaliano ya kusitisha uandikishaji huo, Ruto alisema Putin amethibitisha kuwa Wakenya hawataendelea kuandikishwa katika jeshi la Russia baada ya Kenya kuainishwa kuwa nchi isiyopaswa kuwa chanzo cha uandikishaji wa wanajeshi.

Hatua hiyo inafuatia kuongezeka kwa taarifa za Wakenya wanaoandikishwa kwenda kupigana katika vita vya Russia dhidi ya Ukraine, huku baadhi wakiuawa na wengine wakiripotiwa kutopatikana.

Uchunguzi uliofanywa na taasisi ya Journalists for Justice ulibaini kuwa Wakenya wasiopungua 841 waliandikishwa katika jeshi la Russia kati ya Oktoba 2022 na Juni 2026.

Ripoti hiyo ilitambua Wakenya wasiopungua 76 waliouawa wakipigana upande wa Ruusia. Katika uchunguzi huo, jumla ya Waafrika 3,066 kutoka nchi 40 walibainika kuandikishwa, huku vifo 502 vikithibitishwa kufikia Juni 2026.

Kwa upande mwingine, Shirika la Ujasusi la Kenya (NIS) liliambia Bunge la nchi hiyo kuwa zaidi ya Wakenya 1,000 walikuwa wameandikishwa.

Taarifa za uchunguzi huo zinaeleza kuwa baadhi ya Wakenya walivutiwa kwa kuahidiwa ajira za kiraia katika sekta za ulinzi na usafirishaji wa vifaa, lakini walipofika Russia waliombwa kusaini mikataba ya kijeshi.

Wakati Rais Ruto akikubaliana na Putin, baadhi ya familia na wananchi nchini Cameroon wameandamana katika mji mkuu wa nchi hiyo, wakishinikiza serikali zao na mamlaka za Russia kusaidia kurejeshwa kwa vijana wanaodaiwa kushawishiwa kujiunga na jeshi la Russia na kupelekwa kupigana katika vita dhidi ya Ukraine.

Maandamano hayo ya amani yalifanyika mbele ya Ubalozi wa Russia mjini Yaoundé, chini ya kampeni inayojulikana kama Bring Back Our Sons and Brothers (Waruudisheni Wana na Kaka Zetu), kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari.

Waandamanaji hao wanataka vijana wao walioko katika maeneo ya mapigano warejeshwe nyumbani, huku familia ambazo hazijui walipo ndugu wao zikidai kupatiwa taarifa za uhakika kuhusu hatima yao.

Sababu kubwa ya maandamano hayo ni madai kuwa baadhi ya vijana waliondoka Cameroon baada ya kuahidiwa fursa za ajira za kiraia nchini Russia, zikiwemo kazi za upishi na ulinzi au nafasi za masomo.

Waandamanaji hao wanataka serikali ya Cameroon ishirikiane na mamlaka za Russia kubaini namna vijana hao walivyoajiriwa na kuhakikisha wale wanaotaka kurejea nyumbani wanapata msaada unaohitajika.

Pia, kuna wasiwasi kuhusu idadi ya raia wa Cameroon wanaodaiwa kujiunga na jeshi la Russia na waliofariki dunia katika vita dhidi ya Ukraine.

Taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari zimeeleza kuwa serikali ya Cameroon iliwahi kuthibitisha vifo vya raia wake 16 waliokuwa wakipigana upande wa Russia.

Hata hivyo, uchunguzi uliohusishwa na mashirika ya All Eyes on Wagner na INPACT umetaja makadirio makubwa zaidi ya idadi ya Wacameroon waliojiunga na jeshi hilo na waliouawa.

Baadhi ya ripoti zinadai idadi ya vifo kuwa zaidi ya 95.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *