Muhoozi ampa dhamana Besigye, mazungumzo ya kutafuta suluhu yaanza
Kampala, Uganda. Juhudi za kutafuta suluhu kuhusu hatima ya mwanasiasa mkongwe wa upinzani nchini Uganda, Dk Kizza Besigye, zimechukua mwelekeo mpya baada ya Jenerali Salim Saleh kufichua kuwa ameanza kushughulikia suala hilo kufuatia ombi la Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Muhoozi Kainerugaba, huku akitarajia matokeo ndani ya miezi mitatu hadi sita ijayo.
Saleh, ambaye ni mshauri mkuu wa Rais katika masuala maalumu na Mratibu Mkuu wa Operesheni ya Utajirisho (Operation Wealth Creation), amesema amerejea kuwasiliana na Besigye baada ya miaka kadhaa ya kutokuwa na uhusiano wa karibu kutokana na tofauti zao za kisiasa.
Akizungumza Oktoba 30, 2026, mbele ya viongozi wa kamati za Bunge, wabunge na viongozi wa chama tawala cha National Resistance Movement (NRM), katika kituo chake cha Kapeeka, Wilaya ya Nakaseke, Saleh alisema hatua yake ilianza baada ya kuona ujumbe uliowekwa na Muhoozi kwenye mtandao wa kijamii wa X, Agosti 25, 2026.
Alisema katika ujumbe huo, Muhoozi alielekeza kuwa suala la Besigye lishughulikiwe na Saleh, jambo lililomfanya awasiliane naye ili kuthibitisha kama alikuwa na nia ya kweli.
“Niliuona ujumbe huo Agosti 25 kutoka kwa kiongozi wa Patriotic League of Uganda (PLU), Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Muhoozi Kainerugaba.
“Alisema tatizo la Kizza Besigye ni langu. Kwangu mimi, hakujua kuwa alikuwa amenipa fursa nzuri sana ya kuungana tena na rafiki yangu wa zamani,” alisema Saleh.
Alisema baada ya kuwasiliana na Muhoozi na kuthibitishiwa ujumbe huo, alichukua hatua ya kumtafuta Besigye, ambaye alibaini kuwa hali yake ya kiafya ilikuwa mbaya sana.
“Nilipokwenda hospitalini, nilimkuta rafiki yangu karibu kufa akiwa gerezani. Kwa hiyo, hatua yangu ya kwanza ilikuwa kumtoa gerezani na kumpeleka kwenye kituo sahihi cha matibabu,” alisema.
Saleh alieleza kuwa aliratibu kuhamishwa kwa Besigye kutoka Gereza la Luzira kwenda Hospitali ya Joint Clinical Research Centre (JCRC), iliyopo Lubowa, kwa ajili ya kupata huduma za kibingwa.
Alisema kituo hicho kina uwezo wa kutoa huduma za matibabu alizozihitaji Besigye, akieleza kuwa ni hospitali ambayo hata yeye angependa kutibiwa endapo angehitaji huduma za wagonjwa mahututi.
Besigye alihamishiwa JCRC Agosti mwaka huu pamoja na aliyekuwa Meya wa Kampala, Erias Lukwago, baada ya hali zao za kiafya kuibua wasiwasi.
Miezi sita ya kutafuta mwafaka
Akizungumzia hatua zinazofuata, Saleh alisema juhudi hizo hazihusu tu hali ya afya na kesi ya Besigye, bali pia kutafuta mwafaka wa kisiasa utakaondoa tofauti za muda mrefu zilizojitokeza miongoni mwa viongozi waliokuwa pamoja katika harakati za kisiasa na kijeshi za Uganda.
Alisema ana matumaini kuwa mazungumzo yanayoendelea yanaweza kuzaa matokeo ndani ya miezi mitatu hadi sita, ingawa hakufafanua masharti ya makubaliano yanayoweza kufikiwa wala kutoa uhakika kwamba Besigye ataachiwa huru katika kipindi hicho.
“Usiniulize kama tuko kwenye mazungumzo ya amani au la. Kwangu mimi, nilipopata ujumbe huo nilisema, Mungu amenisaidia kuungana tena na mwenzangu wa zamani. Tunaendelea kushughulikia suala hilo na nina matumaini kuwa tutashawishiana ndani ya miezi mitatu hadi sita ili kuwa na mtazamo wa pamoja kuhusu Uganda tunayoitaka,” alisema.
Museveni aelekeza juhudi za kutafuta suluhu
Hatua za Saleh zinafanyika pia katika mazingira ambayo Rais Yoweri Museveni ameagiza mawasiliano na wadau mbalimbali ili kutafuta suluhu ya kisiasa kuhusu kesi za Besigye na Lukwago.
Waziri wa Sheria na Masuala ya Katiba, Norbert Mao, alithibitisha Oktoba 21, 2026 kuwa juhudi hizo zinafanyika kwa maelekezo ya Museveni, zikihusisha maofisa wa Serikali, familia na vyama vya kisiasa vinavyohusika na watu hao.
Mao alisema maelekezo ya Rais ni kuzungumza na wote wenye maslahi na maisha ya Besigye na Lukwago ili kutafuta maelewano kwa masilahi ya Uganda.
Alieleza kuwa mchakato huo una maeneo matatu yanayoendelea kwa wakati mmoja: kesi za mahakamani, huduma za matibabu na mazungumzo ya kisiasa yanayoongozwa na Saleh.
Alisisitiza kuwa mazungumzo hayo hayamaanishi kusitishwa kwa kesi mahakamani wala kutoa msamaha wa moja kwa moja kwa watuhumiwa.
Kwa mujibu wa Mao, mahakama zinapaswa kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria, huku madaktari wakiendelea kushughulikia afya za wahusika na juhudi za kisiasa zikiendelea kutafuta mwafaka mpana.
Hivyo, nafasi ya Museveni katika suala hilo imejitokeza kupitia maelekezo yake kwa wadau wa Serikali kushiriki katika juhudi za maridhiano, huku Saleh akiwa ndiye anayeongoza mazungumzo hayo.
Msimamo wa familia ya Besigye
Pamoja na juhudi hizo, bado haijathibitishwa kuwa Besigye amekubali kushiriki katika mazungumzo ya kisiasa yanayoongozwa na Saleh au kwamba amekubaliana na masharti yoyote ya kuachiwa.
Mkewe, Winnie Byanyima, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Ukimwi (UNAIDS), amekuwa akisisitiza kuwa afya na haki za mumewe hazipaswi kuwa sehemu ya majadiliano ya kisiasa.
Byanyima amepinga taarifa za kuwepo kwa mazungumzo ya siri kuhusu kuachiwa kwa Besigye, akisisitiza kuwa kipaumbele chake ni kuhakikisha anapata matibabu yanayostahili na haki yake ya kuomba dhamana kupitia mahakama.

